Jumanne, 11 Machi 2014

MASHABIKI WAMHITAJI MALOPE TAMASHA LA PASAKA 2014

 

JINA la Rebecca Malope si geni masikioni na machoni mwa wengi, hasa kwa wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa Injili.
Rebecca aliyezaliwa mwaka 1968, yu miongoni mwa waimbaji wa kimataifa wa muziki wa Injili kutoka nchini Afrika Kusini, aliyewahi kuja nchini mara moja kwa mwaliko wa Kampuni ya Msama Promotions kupamba Tamasha la Pasaka.
Kupitia tamasha hilo ambalo lilifanyika jijini Dar es Salaam Aprili 8, Rebecca akishirikiana na wengine mahiri wa ndani na nje ya Tanzania, walikuwa baraka katika tamasha hilo lililofanyika mara ya kwanza Uwanja wa Taifa mbele ya mgeni rasmi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Umahiri wa Rebecca katika uimbaji na uchangamfu jukwaani, umewafanya wadau wengi watamani awe miongoni mwa waimbaji katika Tamasha la Pasaka la mwaka huu Aprili 20, jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamia katika mikoa itakayopata kura nyingi za wadau.
Shauku ya kumtaka Rebecca ni ishara ya wazi ya wadau hao kuvutiwa na waimbaji wa Afrika Kusini kwani mbali ya mwanadada huyo, wengine waliowahi kualikwa na Msama Promotions ni Sipho Makhabane (Pasaka ya 2013) na Solly Mahlangu (Krismasi ya 2013).
Pamoja na wadau wengi kutamani kumwona mwanadada huyo kama Anna Ferdinand wa Yombo Vituka, Innocent Gregory wa Pugu-Kwa Mustapha, Mkomwa Meshack na Dotto Mnyemvua wa Lumo-Machimbo, kwa mujibu wa waratibu wa tamasha hilo, waimbaji wataalikwa kwa kigezo cha wingi wa kura.
Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, alisema



kuwa kama Rebecca atapata kura nyingi za wadau wataketi kujadili jambo hilo kama inawezekana au vipi, kwani ni miongoni mwa waimbaji mahiri aliyewahi kupamba tamasha la mwaka 2012.
Rebecca ni nani?
Mwanadada huyu shupavu anayejulikana kwa wengi kama malkia wa muziki wa Injili Afrika, ni mzaliwa wa Kijiji cha Lekazi, nje kidogo ya mji wa Nelsprut, Mpumalanga, nchini Afrika Kusini.
Ukiangalia historia yake, Rebecca ni kipaji kilichochomoza katikati ya maisha na mazingira magumu kiasi cha kushindwa kupata elimu ya kutosha, lakini Mwenyezi Mungu akimuinua kupitia kipaji cha uimbaji wa nyimbo za Injili akitamba kimataifa.
Katika mazingira hayo magumu kimaisha, Rebecca akiwa mtoto alipatwa na ugonjwa uliomfanya ashindwe kutembea kiasi cha madaktari kudhani kuwa asingetembea tena katika maisha yake.
Kutokana na ufukara wa familia yake, yeye na dada yake (Cynthia) walikimbilia katika kitongoji cha Everton, nje kidogo ya  Jiji la Johannesburg kwa lengo la kutafuta kazi ya kujikimu kimaisha.
Mwaka 1986, wakati huo Rebecca akiwa na umri wa miaka 21,  alishiriki shindano la kutafuta vipaji vya uimbaji maarufu kama ‘Shell Road to Fame,’ lakini alishindwa kwa mbali.
Lakini hakukata tamaa kwani mwaka uliofuata alishiriki tena na kuibuka mshindi kupitia wimbo wake wa ‘Shine On,’ ukiwa mwanzo wa mwanga wa mafanikio yake kwani kibao hicho kilimsogeza mbali.
Kibao hicho ndicho kilimwezesha kukutanishwa na muandaaji mashuhuri wa muziki, Sizwe Zako na kupata meneja wake wa kwanza aliyejulikana kwa jina la Peter Tladi.
Albamu yake ya kwanza ya Rebecca ambayo ilikuwa na nyimbo za kidunia, haikufanya vizuri sokoni, hivyo akageukia muziki wa Injili kudhihirisha kuwa karama yake ni katika muziki huo na si vinginevyo.
Kutokana na mvuto wa vibao vyake vya awali, Rebecca akajikuta akipata sapoti kubwa kutoka kwa radio mbalimbali kwa kupiga vibao vyake, kitu ambacho kwa Afrika Kusini hakikuwa cha kawaida.
Mwaka 1990, Rebecca alishinda tuzo ya mwanamuziki bora wa kike wa Afrika Kusini na hadi kufikia mwaka 1993, ilikadiriwa kuwa watu zaidi ya milioni moja walimpigia kura kama mwanamuziki bora wa kike katika shindano la Coca Cola Full Blast Music Award Music Show na kushinda tena mwaka 1994.
Kwa upande wa mauzo, albamu zake zote kumi za kwanza zilikuwa moto wa kuotea mbali sokoni zikiingia kwenye hadhi ya dhahabu, ambapo kwa kipindi hicho alikuwa ameuza nakala zaidi ya milioni mbili.
Mwaka 1995 kupitia CD yake ya Shwele Baba, aliuza nakala zaidi ya milioni moja ndani ya wiki tatu tangu ulipozinduliwa, ikiweka rekodi ya aina yake katika historia ya soko la muziki Afrika Kusini.
Mwaka 1996, haukuwa mwaka mzuri kwa Rebecca kwani alimpoteza baba yake mzazi, kaka yake na dada yake. Wote walifariki dunia kwa kufuatana, tena katika mazingira ya kutatanisha, jambo ambalo lilimtikisa kwa kiasi kikubwa mwanadada huyo.
Lakini, Rebecca  alijipa moyo mkuu akimwachia Mwenyezi Mungu kwa yote yaliyotokea na kamwe hakutoa nafasi mkasa huo uwe kikwazo kwake cha kumtumikia Mungu kwa karama ya uimbaji.
Mwanadada huyo anakiri kuwa, siri ya mafanikio yake ni kujituma, kuwa na malengo na kufanya kazi kwa bidii, akimshirikisha Mungu, kiasi cha kutawazwa kuwa malkia wa muziki wa Injili Afrika, huku wengi wakimfananisha na Brenda Fassie, ambaye kwa sasa ni marehemu..
Kati ya mwaka 1995 na 2004 Rebecca amezunguka ulimwenguni akiwa na bendi ya Pure Magic akimtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji.
Mwaka 2003, Rebecca alitunukiwa udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Natal kutokana na  mchango wa kutukuka kwa jamii na muziki nchini Afrika Kusini na Desemba mwaka huo alishinda tuzo ya Kora kama mwanamuziki bora wa Injili.
Katika wanamuziki ambao alishirikiana nao kwa karibu sana na wamekuwa na mchango mkubwa kwake ni pamoja na marehemu Vuyo Mokoena.
Mwaka 2004, Rebecca alianzisha kipindi chake katika runinga kikiitwa ‘Gospel time’ ambacho kinafanya vizuri.
Februari 25, 2012, Rebecca amerekodi nyimbo za ‘live’ katika Jiji la Pretoria, hiyo ikiwa ni albamu ya 32.
Baadhi ya tuzo ambazo Rebecca Malope amewahi kutunukiwa ni mwaka 1994 mwimbaji bora, mwaka 1997 albamu bora sokoni iliyoitwa ‘Uzube Nam’, mwaka 1998 muimbaji bora wa nyimbo za Injili Afrika na albamu bora katika mauzo iliyoitwa ‘Angingedwa.’
Nyingine ni mwaka 1999 mwimbaji bora wa kike na mwimbaji bora wa Injili Afrika kupitia albamu ya ‘Somlandela’, mwaka 2002 msanii bora wa nyimbo za Injili akishinda na wimbo wa ‘Sabel Uyabizwa’, mwaka 2003 msanii bora Afrika kupitia wimbo wake wa ‘Iyahamba Lenqola’ na mwaka 2004 msanii bora wa mwaka kwa wimbo wake, ‘Hlala Nami’.
Rebecca aliyekuwa kipenzi cha Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, marehemu Nelson Mandela na Rais wa sasa, Jacob Zuma, amepitia maisha ya taabu, dhiki kubwa na changamoto nyingi.
Cha kufurahisha kwa mwimbaji huyu nguli,  ni kuwa mpaka sasa ameachia albamu zipatazo 32 ndani ya miaka 27.
“Watu hawana amani, kuna vita kila sehemu, hata kanisani, nataka watu wawe pamoja tena cha muhimu wawe na amani katika maisha yao, ili tuwe na amani duniani, anasema Rebecca.
ORODHA YA ALBAMU
Ma G Man (1986); Six of the best (1989); Saturday Nite (1990); Buyani (1991); Rebecca Sings Gospel (1992); Ngiyikeleni (1993); Umoya Wami (1994); Shwele Baba (1995); Uzube Nam (1996); Live at the State Theatre (1996) na Angingedwa (1997).
Nyingine ni Free at Last (1997);  Somlandela (1998); Ukholo lwam (1999); Siyabonga (2000); Christmas with Rebecca and Friends (2000); Sabel’Uyabizwa (2001); Iyahamba Lenqola (2002); Hlala Nami (2003); The Queen of Gospel and the Village Pope (2004); Qaphelani (2005) na  The Greatest Hits (2005).
Albamu nyingine ni Umthombo (2006); Live in Soweto (DVD) (2006); Live in Soweto (CD)  (2007); Amakholwa (2007); Ujehova Ungu’madida (2008); African Classics (2009); My Hero (2009); Live at the Lyric Theatre (DVD);  (2010) Uzohamba Nami (2010); Ukuthula (2011); Rebecca Live Concert ft Tshwane Gospel Choir (CD)(2012); Rebecca Live Concert ft Tshwane Gospel Choir (DVD)(2012); na Bayos’ khomba (2013).

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni: