Jumatano, 31 Julai 2013

KANISA LA TAG LATEKEREZWA NA MOTO HUKO BIHARAMULO

 Kanisa la TAG, katika kijiji cha Nihongola Kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo, mkoani Kagera limeteketezwa kwa moto na kusalia majivu, usiku wa manane wiki iliyopita na watu wasiojulikana, huku wachomaji wakiacha ujumbe mkali uliojaa  matusi.
 
Akiongea na chanzo cha habari hii, Mchungaji wa kanisa hilo, Samwel Baguma, alisema tukio hilo, lilitokea wakiwa wamelala, lakini walishtushwa na mwanga uliosababishwa na moto uliokuwa ukiteketeza viti na meza zilizokuwa ndani ya kanisa hilo.

Mchungaji Baguma alieleza kuwa, walipoona moto umepamba moto huku ukiwa umekwisha kuharibu kila kitu, walitoka nje na kuita watu ambao walitoka na kuzima licha ya kuwa ulishafanya uharibifu wa kutosha.
 
“Ilikuwa majira ya saa nane hivi, tulihisi kuna kitu kinachoungua kanisani, tulipokurupuka na kutoka nje ndipo tukaona moto mkubwa ukimalizia kuunguza jengo la kanisa na vitu kadhaa vilivyokuwemo ndani,” alisema na kuongeza: 

“Tulipiga kelele na watu walitoka kutusaidia kuuzima ingawa ulikwisha teketeza vitu karibu vyote, baada ya kumaliza kuuzima huku kukiwa kumepambazuka niliona tofali moja likiwa limeegesha karatasi nyeupe na nilipoichukua na kuiangalia nilishtushwa na ujumbe wake.”Alisema alipoisoma ilikuwa imeandika maneno ya kumtukana vikali yakiambatana na vitu vilivyoashiria ushirikina kwa kumtaka aache eneo hilo alilojenga kanisa kwa madai lina wenyewe.

 Alisema, barua hiyo amekwisha iwasilisha Polisi, huku akieleza kuwa ana vielelezo vya kutosha juu ya upatikanaji wa eneo hilo la kuabudia ambapo alibainisha kwamba aliuziwa kihalali na sheria zote zilizingatiwa.
 
 “Kwa sasa tunaabudia kwenye boma letu lingine, hatuna mpango wowote wa kuogopa kile kilichotendeka, siwezi kushtushwa na mambo ya kichawi kwa kuwa Yesu ni zaidi ya wachawi wote, tutaendelea kukaa hapa hadi Yesu anarudi,” alisema. 

 Aidha alilaani kitendo hicho, kwa kuwa kinarudisha nyuma maendeleo, huku akibainisha kwamba ni vema kama mtu ana jambo akaliweka mezani, watu wakalijadili kuliko kufanya uharibifu ndani ya nyumba ya Mungu.

 Akiongea na chanzo cha habari hii Askofu wa Jimbo la Kagera, Julius Bibuhinda alidhibitisha kutokea kwa tukio hilo na kulaani kitendo hicho, huku akieleza kuwa wameiachia Polisi kuwasaka wahusika.
 
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, ACP Philipo Karange, akiongea na chanzo cha habari hii alidhibitisha kutokea kwa tukio hilo nyakati za usiku mnene na kuongeza kuwa, wameshawakamata watu watatu na upelelezi bado unaendelea.

“Hii ni kesi ya jinai, waliokamatwa hadi sasa ni watu watatu wakiwemo ndugu wawili, Bw. James Bugarukanyi na Fabian Bugarukanyi, waliouza kiwanja hicho kwa Mchungaji muda mrefu.Kamanda huyo alimtaja mtuhumiwa mwingine  kuwa ni Rinus Nikodemo, na watafikishwa mahakamani.

 Katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na matukio ya uchomwaji moto wa nyumba za kuabudia, kushambuliwa kwa watumishi na hata kumwagiwa tindikali,Hayo yanatokea, wakati zipo juhudi kubwa ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi wa dini kuleta suluhu baina yao.
 
KWA HISANI YA  http://gospelvisiontz.blogspot.com 
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Chapisha Maoni