Jumamosi, 18 Mei 2013

UNAJUA ALIPOZALIWA YESU, MJINI BETHLEHEM KULIVYO SASA


Zaidi ya hapa unaonekana msururu mrefu wa watu unazunguka kuelekea sehemu ambayo imepambwa zaidi ya nyingine. Ungana na DATIVA MINJA aliyekuwa Hija hivi karibuni akieleza uzuri wa Mji Mtakatifu alikozaliwa Yesu Kristo. UKIINGIA sasa ndani unapokelewa na miziki ya nyimbo au kengele za kwenye taa.

Tena unashuka ngazi tatu hivi ndio ufike ambako kumetengenezwa mithili ya pango lenye taa kila kona, chini kuna marumaru nzuri na zenye kuvutia. Ukiingia ndani ili kujua kulikoni, utaona ‘dekoresheni’ ya marumaru mithili ya nyota na katikati yake kuna shimo la mduara.

Juu kwenye paa kuna taa kubwa na ndogo zinaning’inia usawa wa kugusa kichwani mwa mtu endapo atasimama. Yaani yote ilimradi kuongeza nakshi. Uzuri wa pale huwezi kusimama kwa kuwa hata kuingia kwake unaingia kwa magoti. Hapa si pengine bali ni pale horini mahali alikozaliwa Yesu Kristo, Mkombozi wa Ulimwengu.

Ukiingia Mji wa Bethlehem, Mji Mkuu wa Palestina, upande wa Kusini umepakana na Yerusalem. Mji huo unakadiriwa kuwa na watu 25,000 na hali ya hewa ni baridi kiasi. Tuliambiwa Bethlehem maana yake ni nyumba ya mkate “House of bread” au “House of meat”. Ni ndani ya jengo linalomilikiwa na Shirika la Wafransisko (Franciscan) wa kanisa Katoliki.

Nyumba hiyo ya ghorofa inatumika kwa shughuli mbalimbali za kiroho kama vile mikutano ya injili, ibada za misa, sehemu yakulala mahujaji na kadhalika. Kwanza mpaka kufika lango la kuingia ni foleni na msongamano mkubwa. Sehemu yenyewe iko ndani kwa ndani. Mizunguko mingi hadi kufika hapo.
Ukisoma Luka 2:7 utaona kuwa Mariam alimzaa mwanawe kifungua mimba, akamvika nguzo za kitoto, akamlaza katika hori la kulia ngo’ombe kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya kulala wageni. Panaitwa ‘House of the Lord’. Kwa wakati ule ilikuwa vigumu kupata mahali pa kulala wageni lakini leo hii huduma zote za kijamii zinapatikana.

Achilia mbali nyumba nzuri yenye mvuto na wahudumu wachangamfu wenye kukufanya uendelee kufurahia huduma zao, ambayo ndani mwake niko kwenye hori/pango mahali alikozaliwa Yesu . Mita chache kidogo kufika jengo alimozaliwa masiha, watu wanaendelea na biashara zao, sehemu kubwa ya maduka ya eneo hilo yakiwa yanauza vitu vya asili ya hapo kwao.

Kama huku kwetu basi utasema tulifika kwenye maduka yanayouza vinyago vya mpingo wa kimasai na mambo kama hayo. Kumbe basi wao wanachonga na kuuza vitu mbalimbali kama vile misalaba ya staili tofauti tofauti, picha za familia Takatifu, karamu ya mwisho, Yesu akiwa msalabani, vifaa maalum vya kuwekea mishumaa, vituo vya njia ya msalaba, picha za wanyama, horini alikozaliwa na nyinginezo nyingi.
Umungu wa pale unaonekana zaidi unapoingia ndani ya jengo. Ukiwa kwa nje utaona tu kama ni sehemu ya kawaida japo kuna vibao vinavyoelekeza. Kwa mazingira ya pale wageni ndio wanaonekana kupata mshangao lakini kwa wenyeji wameshapazoea. Hiyo ilikuwa siku ya tano ya hija yetu katika nchi ya Israel.
Safari ya kuzaliwa Yesu ilianza pale Malaika Gabriel alipotumwa na Mungu kwenda mji wa Galilaya ya huko Nazareti kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na Yusufu, mwana wa Daudi; na jina lake aliitwa Mariamu.

Malaika alipoingia nyumabni kwa bikira huyo akamwamkia akisema “Salamu uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Mariam alifadhaika sana na kuwaza moyoni salamu hiyo ina maana gani kwake. Malaika hali akijua kuwa amehofu akamwambia “Usiogope Mariamu kwa maana umepata neema kwa Mungu.
Tazama utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume na jina lake utamwita Yesu, huyo atakuwa mkuu, ataitwa mwana wa aliye juu na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake. Kwa kuwa hakuna nenwo lisilowezekana kwa Mungu Mariamu akasema: “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema,” kisha malaika akaondoka akaenda zake. Tunasoma katika Lk 1:26-38.
Ukiendelea kusoma Biblia, Luka 1: 39 – 56 utaona anaelezea baada ya kupata taarifa hizo alifunga safari kwenda hadi mlimani katika mji wa Yuda kwa Zakaria kumsalimia shangazi yake, Elizabeth.

Baada ya kuzaliwa Yesu malaika wa Bwana akawatokea wachungaji na kuwaambia “Msiogope kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daud amezaliwa kwa ajili yenu, Mwpokozi ndiye Kristo Bwana, na hii ndiyo ishara kwenu mtamkuta mtoto mchanga amevishwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe.

Nini kinachofanya wakristo kwenda kuhiji Yerusalem? Ni kiini cha nchi takatifu. Mji ulioshikamana. Wayahudi wanatafsiri Yerusalem kwa maana ya mji wa Amani. Walitumaini ya kuwa masiha ataleta salamu kamili na Mungu huwalinda katika hatari zote. Safari ya kwenda Yerusalem ilikuwa mfano wa safari ya hapa duniani kwenda mbinguni, Yerusalem mpya.

Zab 122 : Nalifurahi waliponiambia na twende nyumbani kwa Bwana. Ee Yerusalem uliyejengwa kama mji ulioshikamana, Utakieni Yerusalem amani na wafanikiwe wakupendao. Leo hii tunaposherehekea sikukuu ya Noel tutafakari sisi katika jamii tunayoishi tuko tayari kupokea nakupeleka ujumbe wa Mungu kwa watu wote?

Safari hiyo ya Mariamu kwa Elizabeth ilikuwa ya kimisionari, kwenda kumtambulisha Yohane mbatizaji kuwa atazaliwa. Nasi pia tunatakiwa tuwe tayari kumbeba Yesu huyu na kuweza kupeleka habari njema ulimwenguni.


chanzo cha habari mwanachi
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni: