Jumatano, 24 Aprili 2013

VIONGOZI WA KIKRISTO TEC,CCT,SDA,PCT WAKUTANA NA RAIS KIKWETE IKULU




Juu na chini anaonekana Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam leo ambapo amekuwa na mazungumzo nao ikiwa ni mojawapo ya jitihada za Rais Kikwete kutafuta muafaka na kutafuta utatuzi wa hali ya sintofahamu ambayo inanyemelea nchi yetu katika kipindi hiki.




Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam jana

Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam leo. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano) Mhe Steven Wassira.
----

Viongozi wa dini wamewataka waumini kote nchini kulinda amani na umoja uliopo ili nchi isije ikaingia kwenye mgawanyiko wa kidini na kuleta machafuko hapa Tanzania.


Wito huo umetolewa na viongozi wa dini leo Ikulu ya Dar-Es-Salaam mara baada ya kikao cha pamoja baina ya viongozi wa dini na Rais Jakaya Kikwete.


Viongozi hao wa dini wamefika leo wakiongozwa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).


Viongozi wengine wametokea Baraza la Kikristo Tanzania (CCT) Seventh Day Advertist (SDA) na Baraza la Pentekoste Tanzania (PCT).


Mkutano huo umeanza kwa Askofu Ngalalekumtwa kusoma tamko lao la pamoja kwa Rais Kikwete ambalo ndilo limetoa muongozo wa mazungumzo hayo ya leo ambayo yamehusu Amani na Usalama wa Taifa na migogoro ya kidini ndani ya jamii.


Mkutano wa viongozi wa dini ya Kikristo Tanzania ni mojawapo ya jitihada za Rais Kikwete kutafuta muafaka na kutafuta utatuzi wa hali ya sintofahamu ambayo inanyemelea nchi yetu katika kipindi hiki.


“Nataka tuzungumze ni namna gani tunaweza kutoka kwenye hali hii na tunakwendaje mbele zaidi na kuhakikisha nchi yetu bado inakua ya amani na umoja kama ilivyozoeleka” Rais amesema na kutoa nafasi kwa viongozi wa dini kutoa maoni yao.


Viongozi hao wa dini wamemueleza Rais Kikwete kuwa wanaunga mkono jitihada zake za kutafuta amani na kwa pamoja wamekubaliana uandaliwe mkutano wa pamoja baina ya viongozi wa dini zote ambapo masuala ya amani na umoja wa nchi utajadiliwa kwa kirefu.


Katika kikao cha leo pande zote zimekubaliana kuwa kuna changamoto zilizoko sasa zinahitaji kutatuliwa haraka iwezekanavyo ili kuepusha nchi kutumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi, na pia kukubaliana kuwa pande zote, kwa maana ya serikali na taasisi za dini, zinawajibu mkubwa wa kuhakikisha amani inadumu.


Kabla ya kikao cha leo , Rais amewahi kukutana na viongozi wa dini ya kiislamu na kikristo mmoja mmoja ambapo alikua akitafuta maoni na ushauri wa pande zote kabla ya pande zote hazijakaa pamoja na kuwa na msimamo wa pamoja.


Kikao cha leo kimehitimisha jitihada hizo na kinachofuata ni mkutano mmoja ambapo Rais Kikwete atakutana na viongozi wa dini zote kwa pamoja hivi karibuni.


KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: