Alhamisi, 14 Machi 2013

WAZIRI PINDA KUWA MGENI RASMI TAMASHA LA PASAKA



                                                     Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Pasaka litakalofanyika Machi 31 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
 
Taarifa kwa vyombo vya habari, iliyotolewa jana na mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, ilieleza kuwa tayari Ofisi ya Waziri Mkuu imethibitisha kuhusiana na ujio wake kwenye tamasha hilo.
 
“Tunafurahi kwamba katika tamasha letu mwaka huu jijini Dar es Salaam, mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda... mwaka jana alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
 
Waimbaji mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania wanatarajiwa kutumbuiza katika tamasha hilo, ambapo wasanii wa nje ya nchi ni Ephraim Sekeleti wa Zambia, Sipho Makhabane wa Afrika Kusini na Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anayeishi Kenya, pamoja na kwaya ya Ambassadors of Christ ya Kigali nchini Rwanda.
 
Waandaajia wamewataja wasanii wenyeji watakaotumbuiza wakati wote wa tamasha hilo kuwa ni Upendo Kilahiro,  Rose Muhando, Upendo Nkone na John Lissu. Makundi ya kwaya ya Kinondoni Revival na Glorious Celebration pia yatakuwapo.
 
Baada ya kufanyika jijini Dar es Salaam Machi 31, tamasha la pasaka litaendelea Aprili Mosi kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Aprili 3 kwenye Uwanja wa Samora, Iringa na Aprili 6 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. 
 
CHANZO: NIPASHE
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: