Jumatatu, 25 Februari 2013

TAMASHA LA PASAKA KUANZA MKOANI DAR


MKOA wa Dar es Salaam umeshinda katika mchakato wa kuchagua mkoa wa kwanza ambao Tamasha la Pasaka mwaka huu litaendeshwa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama alisema kamati yake ilikuwa ikiendesha kura za maoni kwa mashabiki wao wa eneo lipi tamasha hilo lifanyike.

“Tulifanya kura za maoni kwa njia ya simu za mkononi, pia tulikuwa na vipindi maalum kwenye baadhi  ya redio kwa mashabiki kutoa maoni yao.

“Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Dodoma na Mwanza ilikuwa ikichuana vikali katika kupata mahali ambapo tamasha litafanyika, maana tulikuwa bado hatujatangaza.

 tumechagua Dar es Salaam, ambapo zaidi ya mashabiki 15,000 walichagua tamasha lifanyike Dar es Salaam, mashabiki 13,000 walitaka lifanyike Mbeya, mashabiki 7,000 walitaka Mwanza na mashabiki 3,000 walitaka Dodoma,” alisema Msama.

Alieleza kuwa hivi sasa wanatazama mkoa upi lifanyike Jumatatu ya Pasaka na siku zingine zitakazofuata.

“Siku yenyewe ya pasaka tushapata kwamba ni Dar es Salaam, sasa tunajipanga kwa siku zingine maana mwaka huu tunataka mikoa saba tufanye tamasha letu,” alisema Msama na kuongeza kuwa kwa Dar es Salaam litakuwa Machi 31 mwaka huu.

Pia alisema bado wanaendelea na mazungumzo na wasanii mbalimbali  kwa ajili ya kushiriki tamasha la mwaka huu.

Baadhi ya wasanii walioshiriki tamasha la mwaka jana ni Rose Muhando, Rebecca Malope, Christina Shusho, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro,

Atosha Kissava, Ephraim Sekeleti na kundi la Glorious Celebration.

Pia kwaya mahiri ya Kinondoni Revival, Mwinjilisti Faraja Ntaboba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zilikuwa miongoni mwa burudani zilizokuwepo siku hiyo.



KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: