Jumamosi, 12 Januari 2013

WAINJILISTI WA KKKT WAINGIA KAZINIArusha Magharibi katika Dayosisi ya Kaskazini Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wameapa kuendeleza mapambano kwa walichokiita ufisadi wa viongozi wa Dayosisi hiyo, hadi kieleweke.  

Ili kufanikisha azma yao hiyo, wainjilisti hao zaidi ya 180 kutoka sharika 12 za Jimbo hilo wameazimia kuunda umoja ili ‘kushughulikia’ mafisadi hao katika Dayosisi yao.
Wakizungumza baada ya kukutana jana katika Usharika wa Ngateu kujadili hatma ya maandamano yao yaliyozuiwa na Polisi, wainjilisti hao ambao walidai kuwa wao ndio ‘roho’ ya Kanisa hilo, walisema hawatanyamaza wakiona waumini wao wakivurugwa na mafisadi.

“Sisi ndio roho ya Kanisa na ndio tunaotafuta waumini, hivyo kamwe hatutakaa kimya waumini wetu wanapovurugwa na baadhi ya viongozi mafisadi wa Dayosisi,” alisema Mwinjilisti mmoja huku akiungwa mkono na wenzake katika kikao hicho.

Aliongeza: “Ufisadi hasa wa mali za Kanisa ni hatua ya kuvuruga waumini wetu ambao sasa hata mahudhurio katika ibada za sharika mbalimbali yamepungua na hilo hatutalinyamazia hata kama wote tutafukuzwa. “Hata maandiko matakatifu yanasema mwanadamu akinyamaza, Mungu hatanyamaza na katika hili tuna hakika tutashinda, kwani tunasimamia Neno la Mungu,” alisisitiza huku akinukuu maneno katika Biblia.
Alisema kesho watatangaza rasmi kuundwa kwa umoja wao baada ya ibada ya Jumapili na pia hatua nyingine kali watakazochukua dhidi ya Dayosisi hiyo, baada ya maandamano waliyopanga kufanya jana kuzuiwa na Polisi.

Polisi walizuia maandamano hayo ya amani yaliyokuwa na nia ya kutaka kurejeshwa kwa Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Ngateu, Philemon Mollel na pia kumlazimisha Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Israel ole Karyongi awajibike kutokana na mgogoro unaoendelea ndani ya Kanisa.

Mchungaji Mollel alisimamishwa kutoa huduma za kiroho na kisha kufukuzwa kabisa mwishoni mwa mwaka jana, kutokana na kile viongozi wa Dayosisi hiyo walichodai kuwa ni kutenda makosa yasiyovumilika.
Hata hivyo, hatua hiyo ilitokana na msimamo wa Mchungaji Mollel kusimamia kidete uwajibikaji kwa viongozi wa Dayosisi wanaotuhumiwa kuhusika katika ufujaji wa mali za Kanisa hilo katika vikao halali vya Kanisa hilo.

Mgogoro unaoendelea katika Dayosisi hiyo unatokana na madeni makubwa inayodaiwa Dayosisi kutokana na mikopo inayofikia Sh bilioni 11 zilizokopwa kwa ajili ya ujenzi wa Hoteli ya kitalii ya Arusha Corridor Springs na Hospitali ya Rufaa ya Selian zilizopo jijini hapa.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni