Mtume mwingira |
WANANCHI wenye hasira ambao wanadaiwa kuwa wakazi wa kijiji cha Sikaunga wilayani hapa, wamevamia kambi kwenye shamba lililonunuliwa na Nabii Josephat Mwingira wa Kanisa la Efatha Tanzania na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 228.
Wakazi hao walifanya uharibifu mkubwa ambapo inadaiwa kuwa wameteketeza kwa moto matrekta mawili makubwa aina ya New Holland, nyumba kadhaa kubomolewa na shehena ya mahindi kuchomwa moto wakimtaka mwekezaji huyo kuwaachia ardhi yao ambayo wanadai amewapora.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amekiri kutokea kwa tukio hilo hivi karibuni ambapo watu 11 wanaotuhumiwa kuongoza wenzao kufanya uvamizi huo wamekamatwa na juzi walifikishwa mahakamani.
Inadaiwa kuwa, tangu Nabii Mwingira auziwe shamba hilo lililokuwa la taifa la mifugo la DAFCO–Malonje lenye ukubwa wa ekari 10,000 na uongozi wa Halmashauri ya Manispaa miaka zaidi ya mitano iliyopita kwa bei ya Sh milioni 600 huku mwekezaji wake akituhumiwa kukiuka mkataba wa mauziano.
Hivyo, Serikali baada ya kupokea taarifa kuwa mwekezaji huyo ameanza kulima mazao mbalimbali tofauti na mkataba unaomtaka kufuga, iliuagiza uongozi wa mkoa wa Rukwa kuupitia upya mkataba.
Licha ya kukiukwa kwa mkataba huo, lakini pia watumishi wa shamba hilo wamekuwa wakituhumiwa kukamata na kutesa wananchi wanaoishi pembeni mwa shamba, ikiwa pamoja na baadhi yao kudai kukatwa masikio na wanawake kubakwa, hali iliyoibua uhasama baina ya watumishi wa shamba hilo na wakazi wa vijiji jirani.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi kijijini humo, wamedai kuwa wamevumilia kiasi cha kutosha, ndiyo maana wameamua kuchukua sheria mkononi, ikiwa ni jitihada za kumlazimisha mwekezaji huyo kuwaachia ardhi wanayodai ni mali yao.
Akizungumzia sakata hilo la uvamizi uliofanywa katika kambi hiyo ya Sikaunga, Mchungaji Kiongozi Michael Meela wa Kanisa hilo la Efatha mkoani Rukwa alikiri kuwa mmiliki wa shamba hilo amepata hasara ya zaidi ya Sh milioni 228 kutokana na uharibifu uliofanywa na wananchi hao.
Akifafanua, alisema uvamizi huo ulitokea mara tu baada ya Mbunge wa Jimbo la Kwela, Ignas Malocha kuhutubia mkutano wa hadhara kijijini hapo na kuwahamasisha wananchi watumie nguvu ya umma kuyakomboa mashamba yao yaliyochukuliwa na mwekezaji huyo.
Hata hivyo, alikiri kuwa katika risala yao iliyoandaliwa na Mtendaji wa kijiji cha Sikaunga, R. Mkangwa kwa niaba ya Serikali ya kijiji hicho na kusomwa mbele yake pamoja kueleza changamoto kadhaa zinazowakabili, lakini pia wakazi wa kijiji hicho walitaka kujua hatima ya shamba hilo kama watarudishiwa.
Hata hivyo Mbunge Malocha amekanusha kuhusika na suala hilo, akisema taarifa hizo zimepikwa ili kumchafulia jina, akisisitiza hazina msingi wowote na kuongeza alikwenda hapo kufanya mikutano ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza kutoa maoni ya Katiba mpya mbele ya tume ya kuratibu maoni hayo.
Hata hivyo Kamanda Mwaruanda alikanusha na kueleza kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuwa mbunge huyo alihamasisha matumizi ya nguvu ya umma kuyakomboa mashamba hayo. Juhudi za kumpata Nabii Mwingira hazikufanikiwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni