Jumatatu, 3 Septemba 2012

SERIKALI IMEFADHAISHWA NA KIFO CHA ASKOFU

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali imefadhaishwa na msiba wa Askofu wa Kwanza wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Mhashamu Pascal Kikoti ambao ulitokea ghafla.

Waziri Mkuu alisema hayo jana wakati akitoa salamu za rambirambi kwenye ibada ya maziko ya Askofu huyo kwenye Kanisa la Mtakatifu Maria Imakulata mjini hapa.
 
Mhashamu Askofu Kikoti alifariki dunia Agosti 28 katika hospitali ya Bugando, Mwanza na amezikwa kwenye Kanisa hilo yaliko makao makuu ya Jimbo Katoliki Mpanda. Waziri Mkuu alisema:
 
“Rais Jakaya Kikwete na viongozi wote wa Serikali kwa jumla, tumefadhaishwa sana na msiba huu mkubwa, tena uliotokea kwa ghafla. Lakini kwa kuwa haya ni mapenzi yake Mungu ambaye ndiye Muumba wetu sote tumelazimika kuipokea taarifa hii kwa majonzi makubwa.”
Aliongeza kuwa:“Mhashamu Askofu Kikoti, ametutoka akiwa na umri mdogo sana wa kichungaji wa miaka 55, baada ya kulitumikia jimbo hili kwa miaka 11. Kabla ya kifo chake alikuwa na malengo mengi mazuri yakiwamo ya kufungua Seminari Ndogo ya Jimbo, kujenga Kituo cha Kichungaji na Kijamii na kupanua sekondari ya Mtakatifu Maria hapa Mpanda.
 
“Hivyo basi ni dhahiri kwamba kifo hiki ni pigo kubwa si kwangu, au kwa waumini wa Kanisa Katoliki au Wanampanda tu, bali wananchi wote nchini,” alisema.
 
Mapema akitoa salamu za Baba Mtakatifu katika ibada hiyo, Balozi wa Baba Mtakatifu nchini, Mhashamu Askofu Francisco Montecillo Padilla alisema Askofu Kikoti hatasahaulika kwa mema aliyotenda Iringa akiwa Padri na Mpanda akiwa Askofu.
 
Ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ilihudhuriwa na maaskofu 28 kutoka majimbo mbalimbali ya Tanzania isipokuwa Askofu Renatus Msonganzila wa Musoma na Askofu Aloycius Balina wa Shinyanga ambao walitajwa kuwa wagonjwa. Maaskofu wa Mbulu na Moshi waliwakilishwa na wasaidizi wao.
 
Wakati huo huo, katika ibada hiyo, Askofu Damian Kyaruzi wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga alitangazwa rasmi kuteuliwa na Baba Mtakatifu Benedict XIV kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Mpanda hadi atakapotangazwa Askofu mwingine. Uteuzi wake ulianza juzi.
 
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni