Jumatano, 15 Agosti 2012

MATAPELI WALIOJIFANYA NI ASKOFU NA WACHUNGAJI WAKE WAKAMATWA KWA UTAPELI

UTAPELI mpya umeibuka Dar es Salaam, kwa watu wanaojiita viongozi wa dini wanaovaa mavazi ya kidini kuibia wananchi fedha wakijifanya kuuza mali za Kanisa zilizotolewa msaada na kubaki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, David Misime alisema jana kuwa anashikilia watu watatu kwa tuhuma hizo.

Alitaja watuhumiwa hao kuwa ni Juma Mtumingu (48) mkazi wa Mbagala Kiburugwa ambaye hujifanya Askofu wa Kanisa la Mtoni Mtongani na wachungaji wake wawili; Patrishad Humyobi (42) wa Tandika Kilimahewa na Erasto Robert (50) wa Mbagala ambaye anadaiwa huvaa shati lenye ukosi wa kichungaji.

Kwa mujibu wa Kamanda Misime, baada ya kushawishi wananchi, watu hao hufuatana na wanunuzi hadi katika nyumba ambayo hutumika kama Kanisa katika Manispaa ya Temeke ambako mazungumzo zaidi hufanyikia ndani na baada ya kupokea fedha, hutokea mlango wa nyuma wakidai kuwapo kifaa husika na kwenda kukichukua na badala yake kutumia muda huo kutokomea.

Katika ushawishi wao, Kamanda Misime alisema watuhumiwa hao hujifanya wachungaji wakidai vitu wanavyouza ni mali ya Kanisa ambavyo walipewa msaada na baada ya kubaki huamua kuviuza.
Kamanda Misime alisema miongoni mwa vitu wanavyouza ni magari, pikipiki za matairi matatu-Bajaj na madini na tayari watu wengi wametapeliwa.

Watapeliwa Kamanda Misime alisema Aprili vijana wawili walitapeliwa kwa nyakati tofauti kila mmoja kitoa Sh milioni nne kwa ahadi ya kuuziwa bajaj.

Alisema watu hao waliwaambia vijana hao kuwa Bajaj inayouzwa ni mpya na kwamba ni miongoni mwa iliyobaki kati ya Bajaj 12 ambazo zilitolewa kwa Kanisa hilo kwa ajili ya kusaidia wenye ulemavu.

Kamanda Misime alisema watuhumiwa hao waliwaeleza vijana hao kuwa Bajaj moja ilikwenda kwa Mchungaji na aliamua kuiuza na walipotoa fedha, wakaibiwa ndani ya Kanisa hilo.

“Siku hiyo Bajaj iliyotakiwa kuuzwa iliegeshwa nje ya nyumba hiyo, huku mazungumzo yakifanyika ndani na baada ya kupokea fedha, walitokea mlango wa nyuma wakidai kuwapo kifaa wanachokwenda kuchukua lakini wakatokomea,” alisema Misime.

Kadhalika, alisema mtu mwingine pia aliripoti kutapeliwa Sh milioni 16 kwa ahadi ya kuuziwa gari aina ya Toyota Prado mali ya Kanisa hilo.

Kamanda Misime alitoa hadhari kwa wananchi dhidi ya kundi la aina hiyo kwani ni waongo wenye nia ya kuwaibia fedha.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni