Alhamisi, 5 Julai 2012

WIZARA KUZIKAGUA NGO, MAKANISA NA TAASISI ZINGINE ZA DINI

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, inaanza zoezi la kutembelea na kuhakiki taasisi zisizo za kiserikali (NGO) ambazo zimesajiliwa na Wizara hiyo ili kuhakikisha kuwa vyama hivyo vinafanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria.Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Vyama vya Kijamii katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Numbilya Mpolo amesema jana, zoezi hilo litaanza mwezi Agosti mwaka huu.

Akizungumza katika Banda la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo Maonyesho ya 36 ya Biashara ya Kimataifa yanaendelea, Mpolo alisema, mambo yatakayokaguliwa ni uhai wa vyama hivyo na utekelezaji wa Katiba zake kama zilivyosajiliwa.

“Mambo mengine yatakayokaguliwa ni kama vyama hivyo vinalipa ada ya kila mwaka kwa mujibu wa Sheria na pia utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya kufanya vikao vya chama na kuandaa taarifa za fedha ambazo zinapaswa kuwasilishwa kwa Msajili wa vyama kila mwaka,”alisema Mpolo.
Amesema hatua za kisheria zitachukuliwa kwa vyama vitakavyobainika kukiuka masharti ya sheria za uendeshaji wake, ikiwa ni pamoja na kupewa notisi za kusudio la kufuta chama husika.

“Kwa mujibu wa Sheria za Vyama, chama kitapewa notisi ya kusudio ya kukifuta, na ikiwa hakitatoa hoja kwa nini kisifutwe, ndani ya siku 21, basi Msajili wa Vyama anaweza kutoa notisi ya kukifuta chama, na baadaye kutoa tangazo la kukifuta chama hicho, katika gazeti la Serikali,”alisema.
Akizungumzia kuhusu malalamiko yanayopokelewa na Msajili wa Vyama, Mpolo alisema ni pamoja na taarifa za migogoro inayotokana na kugombea madaraka na pia ubadhirifu wa fedha katika baadhi ya vyama.

Kuhusu Vyama ambavyo vinabadilisha Katiba zao bila mabadiliko hayo kukubaliwa na Msajili, amesema Katiba kama hizo hazitambuliki kisheria.

Alisema hadi sasa jumla ya Vyama vya Kijamii 6,469 vimesajiliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani na kati ya hivyo 875 ni taasisi za kidini.
Mpolo alisema zoezi la kusajili Vyama vya Kijamii bado linaendelea na wananchi wenye mahitaji ya kusajili hivyo wanaweza kuwasiliana na Wizara wakati wowote ili kupata huduma hiyo.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: