Alhamisi, 5 Julai 2012

MADAKTARI BINGWA WAREJEA MUHIMBILI

UONGOZI wa Kitengo cha Mifupa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) umesema mgomo wa madaktari uliokuwapo kwa zaidi ya siku tano umekwisha baada ya madaktari wake 61 kurejea kazini.
Taarifa ya kurejea kwa madaktari hao ilitolewa hospitalini hapo jana na Mwenyekiti wa Bodi ya MOI, Balozi Charles Mtalemwa na kusisitiza kwamba hospitali hiyo haipo katika mgomo kwa sasa.
Mgomo wa madaktari hao ulianza Juni 23 mwaka huu na kushirikisha madaktari waliokuwa chini ya Jumuiya wakati waliokuwa chini ya Chama cha Madaktari (MAT) wakiendelea na kazi.

Hata hivyo, siku nne baada ya kuanza kwa mgomo huo, madaktari bingwa nao waligoma kufuatia kutekwa, kupigwa na kutupwa kwenye msitu wa Pande uliopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Steven Ulimboka.

Mtalemwa alisema Juni 29 mwaka huu bodi hiyo ilikutana na menejimenti ya MOI na kujadili kuhusu kusitishwa kwa mgomo huo, na kwamba madakari waliitikia wito wa kurudi kazini na kuendelea kuwahudumia wagonjwa ambapo kati ya madaktari hao wamo pia madaktari bingwa 18 waliorejea kazini licha ya wengine kutangaza mgomo.

Kwa mujibu wa Balozi Mtalemwa, huduma za upasuaji zinaendelea kutolewa ingawa muitikio wa wagonjwa unasuasua kutokana na kupotoshwa kuwa kitengo hicho kiliingia kwenye mgomo.
Akizungumzia suala hilo kiongozi wa timu ya madaktari bingwa, Dk. Catherine Mng’ong’o, alisema hayupo kwenye nafasi nzuri ya kufanya hivyo kwa kuwa hajafika kazini hivyo hana taarifa za kurejea kwa madaktari hao.

“Leo nashindwa kutoa taarifa kwa sababu ninauguliwa, na sijaenda kazini na sijapata taarifa zozote, labda kesho nitakapopokea taarifa rasmi,” alisema Dk. Mng’ong’o.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: