Jumanne, 24 Julai 2012

RAIS JK ASEMA KIPENGELE CHA DINI HAKITAINGIZWA KWENYE MASWALI YA SENSA

RAIS Jakaya Kikwete amesisitiza kuwa kipengele cha dini hakitaingizwa kwenye maswali ya Sensa ya Watu na Makazi kwa sababu lengo ni kutaka kufahamu idadi ya Watanzania isaidie katika kupanga mipango ya maendeleo ambayo haipangwi kwa misingi ya dini.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa swali kuhusu dini halijapata kuwepo katika maswali katika sensa zote zilizopita.

“Halipo na halijawahi kuwepo,” alisema.
Alisema hayo jana kwenye mkutano wa wananchi katika eneo la Swaya, nje kidogo ya Mji wa Mbeya wakati akizindua mradi mkubwa wa maji kwa Jiji la Mbeya na vitongoji vyake.
“Nafahamu kuwepo madai ya baadhi ya watu kutaka swali la watu kuwa na dini gani liingizwe. Swali hili halipo na halikuwahi kuwepo kwa nia njema kabisa,” alisema na kuongeza: “Hatupangi mipango yetu ya maendeleo kwa misingi ya dini au rangi za watu bali kwa kuzingatia maeneo na shughuli, mambo ambayo hunufaisha watu wa dini zote”.
Alifafanua zaidi kwamba siyo kwamba serikali inapuuza dini za watu bali shabaha ya Sensa ni maendeleo ya wote.

Rais Kikwete aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa na kutoa taarifa sahihi kwenye siku ya Sensa ambayo ni Agosti 26, mwaka huu.
Rais Kikwete pia amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwenye Tume ya Katiba ambayo imeanza kazi ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya.
Rais alitumia nafasi hiyo kufafanua tena nafasi ya Rais katika mchakato mzima wa Katiba akisema kuwa kuna wakati baadhi ya watu walisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania asihusike katika mchakato huo.

“Sasa utamweka vipi pembeni Rais katika mchakato kama huu? Rais ndiye mwakilishi wa Watanzania wote. Rais ndiye kielelezo cha mahitaji ya Watanzania wote. Ni kweli anachaguliwa kutoka kwenye chama, lakini anachaguliwa na Watanzania wote na akishachaguliwa basi anakuwa Rais wa wote.”

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni