Jumatano, 4 Julai 2012

MADAKTARI WAANZA KUREJEA POLEPOLE MUHIMBILI

MADAKTARI wameanza kurejea polepole katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuhudumia wagonjwa wanaofika hapo na waliolazwa.Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema jana kuwa kurugenzi za hospitali hiyo, zilifanya kazi kwa kiwango cha kati kutokana na kuwapo wagonjwa wachache.
Kwa mujibu wa Aligaesha taarifa za utendaji kazi zilipatikana baada ya tathmini katika kurugenzi za Tiba, Upasuaji, Tiba Shirikishi na Uuguzi.
Kuhusu Kurugenzi ya Tiba, alisema huduma ziliendelea kutolewa kwa kiwango cha kati kwa kuwa wagonjwa ni wachache wakati katika Idara ya Tiba madaktari bingwa wote na wasajili wote walifika na kufanya kazi.
“Madaktari walio katika mafunzo kwa vitendo (interns) 11 walifanya kazi, wodi muhimu zilihudumiwa na kliniki zote za jana ziliendelea kufanya kazi na kliniki za mchana zilifanyika,” alisema Aligaesha.

Katika Idara ya Watoto, Aligaesha alisema madaktari bingwa wote walikuwapo na walifanya kazi ingawa walikuwa na changamoto ya kufanya kazi pia katika kliniki za wagonjwa wa nje.
Alisema katika Idara ya Magonjwa ya Nje, wahudumu wa usajili na madaktari bingwa walikuwapo wote na walifanya kazi pamoja na Idara ya Magonjwa ya Afya ya Akili kwani wagonjwa wote walikuwa wodini na walionwa na madaktari.
Alisema katika Idara ya Magonjwa ya Dharura, wasajili wote walisaini lakini waliofanya kazi ni wawili na daktari bingwa alikuwapo na Idara ya Mazoezi ya Viungo pia wafanyakazi wote walihudhuria na walifanya kazi.

Katika Kurugenzi ya Upasuaji, alisema huduma za upasuaji zilifanyika lakini si sawa na jinsi ilivyokuwa kabla ya mgomo, kwani wagonjwa ni wachache katika baadhi ya kliniki na kliniki zingine wagonjwa walikuwa wengi.
Aligaesha alisema wagonjwa wa upasuaji waliokuwa wodini walihudumiwa ingawa ni wachache ikilinganishwa na hali ilivyokuwa wakati wa mgomo na baadhi ya huduma za upasuaji zilifanyika ingawa wagonjwa ni wachache.
Kuhusu huduma za tiba shirikishi, alisema vipimo vya maabara na vya uchunguzi wa radiolojia viliendelea kufanyika kama kawaida ingawa idadi ilipungua ikilinganishwa na kabla ya mgomo. Alisema Idara ya Famasia pia ilifanya kazi kama kawaida.
Madaktari wa Vitendo watimuliwa

Wakati madaktari wakirejea kazini taratibu na kuhudumia Watanzania, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilidaiwa jana kufukuza madaktari walio katika mafunzo kwa vitendo.
Msemaji wa madaktari hao, Frank Kagoro alidai jana kuwa madaktari hao walipewa barua za kufukuzwa, lakini walizikusanya na kuzirejesha kwa Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Alisema waliutaka uongozi wa Muhimbili kuzipeleka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kuwa wao wako chini ya Wizara.
Hata hivyo, Aligaesha alipohojiwa kuhusu kufukuzwa kwa madaktari hao, alisema hawezi kulizungumzia na kusisitiza kuwa halipo katika taarifa hiyo.
Waitwa wizarani

Wakati madaktari hao wakitaka Muhimbili iwarudishe serikalini, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imewaagiza madaktari hao waripoti wizarani kabla ya keshokutwa.
Msemaji wa Wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja alisema madaktari hao wote nchi nzima, wanatakiwa kufika wizarani siku hiyo ili kuelezwa taratibu zingine.
Hospitali nyingine Huduma katika Hospitali ya Amana iliendelea kutolewa huku wagonjwa wakifika kwa wingi hospitalini hapo.

Amina Abdallah, mkazi wa Tabata alisema alifika hospitalini hapo kumpeleka baba yake lakini hali haikuwa mbaya alipokewa Mapokezi na madaktari walikuwapo wakihudumia.
Dk Mwinyi akazia Naye Veronica Mheta anaripoti kutoka Arusha kwamba, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema msimamo wa Serikali uko pale pale kwa madaktari kuwa anayeona hawezi kufanya kazi serikalini kwa mshahara wa Sh 957, 700 atafute sehemu nyingine.
Alisema huduma kwenye hospitali nchini zimerejea hali ya kawaida na baadhi ya madaktari wamekubaliana na Serikali na wengine wasiokubaliana watatafuta pa kwenda.
Akifungua mkutano wa siku tatu wa Watafiti wa Magonjwa ya Binadamu ulioshirikisha watafiti, madaktari na maprofesa kutoka nchi mbalimbali duniani, Dk Mwinyi alisema tamko alilotoa Rais Jakaya Kikwete, linaeleweka.

Wanahabari wazushi
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki amekemea tabia ya baadhi ya vyombo vya habari kuvumisha kuwapo mgomo wa madaktari kwenye hospitali za mkoa huo, jambo ambalo si sahihi na limekuwa likiumiza wananchi, anaripoti Hellen Mlaky.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Sadiki alisema hali inayovumishwa si sahihi na madaktari katika hospitali za mkoa huo ikiwamo Temeke, Amana na Mwananyamala wanaendelea na kazi kama kawaida.

Muhimbili kutathiminiwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma, Celina Kombani, wakati akijibu hoja za wabunge jana, alisema katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kuna watumishi wengi na hivyo Serikali itafanya tathimini ya kazi ya kila mtumishi ili kufahamu kama wote wanahitajika au la.
Alisema baada ya kutathimini kazi za watendaji wote, wataangalia sifa zao kama zinawaruhusu kuendelea kufanya kazi katika hospitali hiyo na kama haziwaruhusu, watahamishwa.
Naye Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, alisema anaunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya kuwaruhusu madaktari kwenda kwa mwajiri atakayewalipa Sh milioni 7.7.
Cheyo ambaye alitaka vyama vyote vya siasa kuunga mkono hotuba hiyo, alisema fedha kamwe haiwezi kununua maisha ya mwanadamu na kuwataka madaktari kurudi kazini.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni