Jumatano, 18 Julai 2012

KOVA ASHINDWA KUJIBU MADAI YA MCH GWAJIMA

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaa, limeshindwa kujibu madai ya Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo, Josephati Gwajima, ya kulitaka liwakamate watu waliohusika kumteka na kumtesa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Ulimboka.

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya jeshi hilo, kumkamata na kumfikisha mahakamani raia wa Kenya Joshua Mhindi (21), akidaiwa kuhusika na tukio hilo, madai ambayo mchungaji Gwajima, alihoji ni kwa nini watuhumiwa waliotajwa moja kwa moja na Dk. Ulimboka mwenyewe hawakamatwi na kuhojiwa.

Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juu ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo wiki iliyopita, alilihusisha kanisa la Ufufuo na Uzima akidai Mulundi ni muumini wao, jambo ambalo lilipingwa vikali na mchungaji Gwajima na kuanika mkasa mzima.Hata hivyo jana katika mkutano wake na vyombo vya habari, Kova alikwepa kabisa kuzungumzia madai ya mchungaji Gwajima na badala yake akadai kuwa jeshi hilo halina haja ya kuingia kwenye malumbano na viongozi wa dini.
Kova alifafanua kuwa kwa sasa suala la Mhindi na mlalamikaji Dk. Ulimboka, halizungumziki nje ya utaratibu wa mahakama.

“Ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujadili jambo ambalo liko mahakamani kama ilivyo katika shauri hili,” alisema Kova.
Kuhusu madai ya mchungaji Gwajima kuwa mtuhumiwa ni kichaa au mwendawazimu, Kova alisema kuwa kisheria ni suala ambalo daktari ndiye mwenye uwezo wa kumpima kitaalamu.
Alibainisha kuwa hata kichaa au mwendawazimu anamilikiwa na sheria ambapo kama akifanya makosa ya jinai, anashughulikiwa kama mhalifu mwingine.

Vile vile alisema jeshi hilo haliwezi kuingia katika mtengo wa malumbano na taasisi za dini iwe ni ya Kikristu au Kiislamu ama madhehebu mengine. Kova alisema jeshi hilo lina wajibu wa kudumisha amani ili viongozi wa dini na waumini wao wawe huru bila hofu katika kufanya ibada zao usiku na mchana. Mchungaji Gwajima katika mkutano wake juzi, alisisitiza kuwa analishangaa jeshi hilo kwani mtu wa kwanza ambaye alipaswa kukamatwa na kuhojiwa kutokana na tukio ni Afisa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi, ambaye alitajwa na Dk. Ulimboka.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: