Jumatano, 4 Julai 2012

DECI NYINGINE YAWALIZA WATU HUKO SUMBAWANGA

VILIO na simanzi vimetawala miongoni mwa baadhi ya wakazi ya Manispaa ya Sumbawanga katika Mkoa wa Rukwa wakiwamo wafanyabiashara, watumishi wa Serikali, wastaafu waliokwishalipwa stahiki zao na viongozi wa dini baada ya kutapeliwa mamilioni ya fedha katika mchezo wa upatu.
Habari za uhakika zinaeleza kuwa watu zaidi ya 20 waliopanda mbegu kati ya Sh milioni 1.5 hadi milioni 30 katika mchezo huo wa upatu, wametapeliwa zaidi ya Sh milioni 300.

Kutokana na kutapeliwa huko, jana asubuhi baadhi ya waliopanda mbegu na kutegemea kuvuna Julai 2, walijikuta katika wakati mgumu baada ya kufika ofisini na kukuta imefungwa, hali iliyosababisha baadhi yao kuzirai kwa muda, kuangua vilio na baadhi kusikika kutishia kukatisha uhai kutokana na hasara.Miongoni mwa waliokutwa na kadhia hiyo ni Kasisi mmoja wa Kanisa Katoliki mjini hapa na mtawa wa kike wanaodaiwa kuchota fedha katika moja ya taasisi za kanisa hilo na kuzitumbukiza katika upatu.

Mchezo huo wa upatu ulikuwa ukiendeshwa na Sadiki Kinyogoli ambaye alikuwa akitumia jina jingine la Johnson Zambi ambaye ni mkazi wa Mbeya kupitia kampuni yake, Amte yenye makao yake makuu Mbeya; lakini ilikuwa na ofisi ya muda katika kitongoji cha Chanji mjini hapa na kuvutia watu wengi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa masharti ya majina yao kutoandikwa gazetini, baadhi ya akinamama waliojitambulisha kuwa ni wafanyabiashara ya mpunga, wamekiri kupanda mbegu na hatimaye kutapeliwa mamilioni ya fedha.

“Mimi pekee nilipanda mbegu zaidi ya Shilingi milioni 20 katika mchezo huo wa upatu na sasa natamani nijinyonge baba……….Nimepoteza fedha nyingi sana naumia sana hata sina pa kushika kwani fedha zenyewe nilikopa na sasa sijui nitarudishaje,” alihoji mmoja wa wafanyabiashara hao wa mpunga mjini hapa.

Mwathirika mwingine, Crispine Mwaruanda maarufu kwa jina la Fundi Cris, alieleza kuwa alivutiwa na mchezo huo baada ya kuelezwa ukiweka fedha unapata mara mbili ya uliyoweka ndani ya siku 10.
Alisema baada ya kupanda kiasi hicho cha fedha, alipewa ofa ya siku 10, hali iliyomvutia na kumshawishi rafiki yake, Frank Mlowezi kuweka kiasi kama hicho cha fedha kama mbegu katika mchezo huo.

“Basi jana (Julai 2) ilikuwa siku yetu tuliyoahidiwa kuwa tungeanza kuvuna, lakini wakati nikiwa kazini ghafla nikataarifiwa kuwa ofisi imefungwa hivyo nilikodi pikipiki na kukimbilia huko baada ya kukaa kwa zaidi ya saa kumi ndipo walipotokea wasichana wawili waliojitambulisha kuwa ni watumishi wa kampuni hiyo,’‘ alieleza Fundi Cris.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni