Jumatatu, 28 Mei 2012

KANISA NA GARI LA ASKOFU LACHOMWA MOTO ZNZ WABARA WATAKIWA KUONDOKA

Askofu wa Madhehebu ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God la Kariakoo, Dickson Kaganga amesema watu wasiojulikana wamechoma moto jengo la Kanisa hilo jana usiku majira ya saa 3.30 usiku na kusababisha hasara kubwa.

Amesema mnamo saa hizo, watu wasiojulikana walivamia Kanisa hilo huku wakitoa lugha chafu zenye kuashiria uvunjifu wa amani, ambapo walinzi wa Kanisa hilo ilibidi wajifiche kuokoa maisha yao.

Amefahamisha kuwa vitu vilivyoungua ni pamoja na gari dogo aina ya Corrola, Viti vya plastiki, Vyombo vya muziki, Kuta za kanisa pamoja na Vifaa vingine.

Askofu Kaganga amefahamisha, Jengo la Kanisa nalo halifai kwamatumizi ya sala na linahitaji matengenezo makubwa ikiwemo viungio vya umeme kwani hadi sasa hawajaweza kufanya tathmini kujua hasara kamili iliyopatikana.

Ameongeza kuwa, wahalifu hao waliofanya vitendo vya kuchoma moto Kanisa hilo, walidhamiria kufanya mauaji kwani zana walizokuwa nazo ni visu, mawe na silaha nyingine za kienyeji.

Amesema kuwa, aliwaelekeza walinzi wa Kanisa hilo kujificha katika sehemu ambayo isingekuwa rahisi kuonekana kutokana na nyimbo za maneno waliyokuwa wakisema yaliashiria kabisa kufanya uhalifu mkubwa.

Askofu Kaganga ameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuviangalia kwa makini vikundi vyenye kuashiria shari ili kuitunza na kuienzi amani ya Taifa hili.

Picha Kanisa lachomwa moto Zanzibar
Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) liliopo mtaa wa Kariakoo mjini Unguja limechomwa moto jana usiku wa kuamkia leo (picha: Salma Said)
Picture
Gari la Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Bishop Dickoson Kaganga lililochomwa moto usiku wa jana katika eneo la Kariakoo nje ya kanisa hilo ambapo uharibifu wote unaelezwa kuwa umegharimu shilingi millioni 120 (picha: Salma Said)
Picture
Katibu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) Sheikh Abdallah Said Ali ambaye ni miongoni mwa wanaotafutwa na jeshi la polisi akizungumza na Radio DW asubuhi mapema kabla ya taarifa ya kutafutwa kwao kutolewa kwa vyombo vya habari (picha: Salma Said)


JUMUIYA YA UAMSHO NA MIHADHARA YA KIISLAMU

(JUMIKI)

للجنة الدعوة الإسلامية

THE ASSOCIATION FOR ISLAMIC MOBILISATION AND PROPAGATION

P. O. BOX: 1266 -Tel: +255-777-419473 / 434145- FAX +255-024-2250022 E-Mail: jumiki@hotmail.com

MKUNAZINI ZANZIBAR


Tarehe 27MAY2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Kila sifa njema anastahiki ALLAH (S.W) na Rehma na Amani zimuendee Mtume Muhammad (S.A.W), ahli zake, Maswahaba zake na walio wema katika Uislamu.

Jumuia ya UAMSHO inatoa taarifa rasmi kwa umma wa Wazanzibari na Watanzania wote kwa ujumla kwamba haihusiki na vitendo vyote vya uvunjaji wa amani vilivyotokea usiku wa tarehe 26 Mei 2012. Kama alivyosema Mtume (S.A.W) katika Hijatul Wadaa, kwamba ni haramu kumwaga damu zenu, kuharibiana mali zenu, kuvunjiana heshma zenu ila kwa haki ya Uislamu (maana yake pale mtu anapofanya kosa na likathibitika atahukumiwa kwa hukmu ya Kiislamu). Vile vile Uislamu unaheshimu nyumba za ibada (Makanisa, Mahekalu na n.k) zisivunjwe wala zisiharibiwe.

Jumuia inatoa wito kwa Waislamu na Wazanzibari wote kuendelea kudumisha amani na utulivu wa nchi na kutoharibu mali za serikali, mali za wananchi, mali za taasisi za dini zenye imani tofauti, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislamu. Jumuiya inayachukulia matukio yaliyotokea usiku wa jana, na yanayoendelea tangu alfajiri leo, kama ni njama za makusudi za wale wasioipendelea amani nchi hii, pamoja na kutaka kuipaka matope jumuiya na kutaka kuzuia lengo la Wazanzibari kudai nchi yao.

Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na Vyombo vyote vya Dola wafanye kazi zao kama wanavyotakiwa kwa mujibu wa muongozo wa haki za binadamu kwa Polisi na vikosi vingine unaosema kwamba polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu. Kila mtu anayo haki ya kuwekewa mazingira muafaka ya kitaifa na kimataifa yatakayomuwezesha kupata haki zake za binadamu.

Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu isipokuwa tu kwa minajil ya kulinda haki za wengine.

Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kuheshimu, kulinda na kutetea haki za binadamu kwa watu wote.
WABILLLAH TAWFIQ

Source: http://www.wavuti.com/4/post/2012/05/picha-kanisa-gari-la-askofu-vyachomwa-moto-zanzibar-jumiki-yakunanusha-kuhusika.html#ixzz1w8PO1zlU

MAKANISA YACHOMWA, WABARA WATAKIWA KUONDOKASalma Said, Zanzibar
ZANZIBAR imechafuka. Baada ya kuwapo kwa amani kwa takribani mwaka mmoja tangu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, vurugu na hali ya wasiwasi zimeibuka tena baada ya wanaharakati wa Kiislam kufanya maandamano kutaka uhuru wa visiwa hivyo.
Zanzibar ilijikuta katika hali tete kiusalama tangu mwaka 1995 baadaya kutangazwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Rais, ambayo Chama cha Mapinduzi (CCM) kiilibuka kidedea na Chama cha Wananchi (CUF) kupinga, lakini uhasama huo ulizikwa Julai 31 mwaka 2010, baada ya kura ya maoni ya kuunda Serikali hiyo ya umoja wa kitaifa.

Lakini kuanzia juzi usiku hadi jana jioni mji wa Unguja na viunga vyake ulitikiswa na mabomu ya kutoa machozi ambayo polisi waliyatumia kutawanya mamia ya wanaharakati hao wa Kiislam wakiongozwa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI).

Mabomu ya machozi yalipigwa mfululizo juzi usiku na kuendelea kutwa nzima jana, hivyo kuathiri shughuli za biashara, ibada katika makanisa mbalimbali na kusababisha hofu kwa wananchi.

Kwa muda wa saa takriban mbili hivi kati ya saa 3:00 na saa 5:00 asubuhi, helkopta ya polisi ilikuwa ikipasua anga la Zanzibar ambalo lilikuwa limetandwa na moshi uliotokana na mabomu ya machozi pia uchomaji wa matairi ya magari.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa aliwaambia waandishi wa habari kuwa wafuasi hao wamefanya uharibifu mkubwa ikiwa pamoja na kuchoma moto makanisa mawili na kwamba, watu saba akiwamo Imamu wa Msikiti wa Bizeredi, Maalim Mussa Juma wanaotuhumiwa na matukio hayo wamekamatwa na jeshi hilo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Askofu Dickoson Maganga alisema watu wasiojulikana walivamia kanisa lao eneo la Kariakoo Mjini Zanzibar mnamo saa 4.30 usiku na kuvunja ukuta, kuchoma viti vya plasitiki pamoja na gari yake.

Chanzo cha vurugu hizo kinatajwa kuwa ni wanaharakati hao juzi kufanya mkusanyiko na maandamano makubwa ya kushtukiza ambayo yalizistua mamlaka za usalama visiwani humo, lakini baada ya kutawanyika jioni baadhi ya viongozi wa maandamano hayo walitiwa mbaroni.

Baada ya kukamatwa kwao, wafuasi wao walikusanyika makao makuu ya polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Madema, kushinikiza kutolewa kwa viongozi hao wanaoshikiliwa kituoni hapo.

Habari zaidi zinasema kutokana na hali ilivyo, askari polisi walitarajiwa kuongezwa visiwani humo, ili kusaidia kuimarisha hali ya usalama pia kuwadhibiti wahalifu ambao walikuwa wameanza kuelekea nje ya maeneo ya mji.

Tayari kuna taarifa kuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutoka Tanzania bara jana mchana walingia Zanzibar kwa ajili ya kuongeza ulizi katika mji wa Unguja.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza hakuna kiongozi yoyote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) aliyetoa kauli kuhusu hali hiyo.

Kauli ya Polisi
Kamishna Mussa alisema jeshi lake litaendelea kuwasaka na kuwatia mikononi wote waliopanga fujo hizo pamoja na viongozi wote wa JUMIKI.

“Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar ndio iliyohusika na kuwachochea vijana kukusanyika na kufanya uharibifu ikiwemo kuchoma moto gari, kupanga mawe barabarani na kufanya hujuma mbalimbali kinyume cha sheria. Tutaendelea kuwasaka kwa gharama zote,” aliapa Kamishna Mussa.

Alifafanua kwamba kwa sasa mikusanyiko yote ya mihadhara ya kidini na vyama vya siasa, lazima ipate kibali cha polisi vyinginevyo jeshi lake litatumia nguvu za ziada kutawanya mikusanyiko hiyo ili kulinda sheria za nchi, amani na utulivu.

Hata hivyo, kamishna huyo wa polisi alijizuia kuhusisha harakati za Uamsho na chama cha siasa wala kutaja majina ya viongozi ambao tayari wanashikiliwa na jeshi lake.

“Mpaka sasa hivi sina majina yao kwa jumla, lakini tumewakamata viongozi wa Uamsho na tunatendelea kuwasaka lakini jina moja tu ndio ninalo ambalo ni Mussa Abdallah Juma,” alisema Kamishna huyo.

Hali bado tete
Wakati jeshi la polisi litoa onyo hilo, hali ya usalama ilionekana kuwa bado tete huku maeneo kadhaa ya Mji wa Zanzibar hasa Darajani na Michenzani ambako muda wote ni sehemu zenye harakati nyingi za biashara, jana zilikuwa zimebakia bila pilikapilika kutokana na askari waliojihami kufanya doria katika mitaa yote na kulipua mabomu kila penye kikundi cha watu waliokusanyika wakinywa kahawa.

Mitaa hiyo ilikuwa imechafuliwa kwa mawe, matofali na magogo yaliowekwa barabarani ili kuziba njia kwa ajili kuzuia magari yasipite huku mipira ya magari ikiwashwa moto na vijana hao.

Kwa upande wake Askofu Maganga akizungumzia uvamizi kisha uhalifu uliofanywa kanisani kwake alisema:
“Nasikitika sana kwa tukio hili ambalo tayari tumeiarifu polisi ambao jana (juzi), usiku walifika hapa wakishirikiana na kikosi cha kuzima moto na kufanikiwa kuuzima moto huo ambao kwa habati nzuri haujaathiri paa la kanisa letu,” alishukuru kiongozi huyo.

Alisema kundi la watu ambalo lilikuwa likitoa maneno ya kashfa na kutishia maisha ya waumini waliokuwa wakifanya ibada usiku huo, lilikatisha ibada hiyo pamoja na kusababisha uharibifu wa mali ya kanisa hilo yenye thamani ya zaidi ya Sh 100 millioni.

Kauli ya JUMIKI
Kutokana na hali hiyo, jumuiya hiyo jana ilitoa taarifa yake kwa vyombo vya habari ikikanusha kuhusika na kuchochea watu kuchoma kanisa wala kuharibu mali za watu.

Hata hivyo, Katibu wa Jumuiya hiyo, Abdallah Said alisema katika taarifa hiyo kwamba jeshi la polisi linapaswa kubeba lawama kwa yote yaliotokea kutokana na kuvunja sheria na kuwakamata viongozi bila ya utaratibu wa busara.

“Uislamu ni dini ya amani na inahimiza ushirikiano na utulivu na hatuwezi kuwatuma watu kwenda kuvunja makanisa na kuharibu mali, kwa sababu ndani ya imani zetu tunajua hilo ni kosa na jambo ambalo halifai katika maamrisho ya dini yetu,” alisema Sheikh Abdallah.

Taarifa hiyo ilisema pia kwamba jumuiya hiyo imekuwa wazi katika kudai maslahi ya Zanzibar na sio vinginevyo na kuahidi kufanya hivyo kwa njia za amani, na iwapo watakuwa wamekosea basi wapo tayari kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Ni lazima polisi wajue kwamba tupo tayari kufanya kazi kwa misingi ya kisheria na hata kwa kujisalimisha tupo tayari, lakini ukamataji bila kufuata busara na sheria haukubaliki. Tunachokitaka ni kura ya maoni haraka na hilo tutaendelea kulidai,” alisisitiza katibu huyo wa JUMIKI.

Wakati viongozi wa Uamsho wakiendelea kutafutwa na jeshi la polisi, nyumba ya kiongozi aliyeongoza maandamano juzi Sheikh Farid Hadi Ahmed inadaiwa kuvunjwa milango usiku wa manane alipokuwa akiswakwa jeshi hilo.

Hata hivyo, taarifa hizo hazikuthibitishwa iwapo ni polisi waliofanya kitendo hicho au la, wanafamilia wanasema waligongewa milango na kutakiwa wafungue baada ya kutofungua walisikia kishindo kikubwa cha kusukumwa milango katika eneo la Mbuyuni Mjini Unguja.

Vijana katika mitaa ya Zanzibar jana walionekana wakiwa na hamasa kubwa wakidai kuendelea kuungana na viongozi wao kudai haki ya Zanzibar, pamoja na kutaka Zanzibar huru kutoka ndani ya mikono ya Muungano.

“Sisi tunachokitaka Zanzibar yetu watupige mabomu, watuue, watukamate lakini tunataka Zanzibar yetu na hatusikii lolote,” walisikika baadhi ya vijana.

Hada jana jioni vurugu katika badhi ya maeneo hususan Kwelekwe na njia ya Baa ya Amani zilikuwa zikiendelea na gari moja lilichomwa moto karibu na ofisi ya CCM.

Moto ukiwaka katikati ya mtaa mjini Zanzibar jana baada ya vurugu za wanaharakati kupinga muungano na kudai Zanzibar ijitawale. Picha na Salma Said


Matukio kabla
Zanzibar imekuwa ikitawaliwa na matukio ya ghasia ambayo licha ya mihadhara hiyo ya Kiislam ilikuwa ni uhasama wa kisiasa kati ya vyama vikuu vya CUF na CCM, hatua ambayo iliwahi kusababisha mauaji ya Januari 27, mwaka 2001.

Lakini, uhasama huo wa kisiasa ambao ni wa kihistoria ulizikwa baada ya kura hiyo ya maoni na uchaguzi mkuu wa 2010 hatua ambayo imemfanya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa SMZ huku baadhi ya mawaziri pia wakitoka katika chama hicho.

Hata hivyo, wanaharakati hao wa Kiislam wameanza upya kuilipua Zanzibar wakishinikiza visiwa hivyo viwe taifa huru kwa kujitenga katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Zitto ataka tume ya uchunguzi
Katika hatua nyingine Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amemtaka Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aunde kikosi kazi maalum kwa ajili ya kudhibiti
vurugu hizo na kuanza mazungumzo na pande zote kwa kuwa, "Hiki sio kitendo cha kudharau
kabisa."

Alifafanua kwamba waliochoma nyumba za ibada wasakwe na kufikishwa mbele ya sheria mara
moja na kuongeza, "Tusiruhusu hata kidogo wapuuzi wachache kutuingiza katika vurugu za
kidini ili kufikia malengo yao ya kisiasa."
Source Mwananchi
http://www.mwananchi.co.tz/component/content/article/37-tanzania-top-news-story/23346-zanzibar-yalipuka.html

Hakuna maoni: