Jumanne, 21 Februari 2017

MASIHI ANAPOKOSEA


 
Bila shaka tunajua neno hili alilosema BWANA Yesu, “Mkinitumikia, Baba yangu atawaheshimu”. Tafakari hapo kwa muda; BWANA hakusema “mkiwa wakamilifu” ila “mkinitumikia”. Ahadi ya kuheshimiwa ipo kwa WATUMISHI, hata kama sio WAKAMILIFU.
 
Yamkini wapo wengi, masihi (wapakwa mafuta), wanatumika huku na kule, lakini wanamapungufu ya dhahiri; Bado Mungu anawaheshimu! Kwa sababu wamekubali KUTUMWA naye. Hao wanaitwa WATENDA KAZI pamoja na Bwana. Kumbuka, sio kila mtenda kazi ni mteule! Usichanganye kazi na utakatifu. Mungu hamtumii mtu kwa sababu ni mtakatifu, Anamtumia mtu kwa sababu yuko tayari kutumika! Ukitaka kwenda Mbinguni, hicho ni kibarua kingine cha binafsi kabisa; tafuta utakatifu pia.
 
Ndipo wengi watasema sikuile, “tulitenda kazi pamoja nawe, tulitoa pepo, nk., BWANA atasema SIKUWAJUA”! Inamaana walikubali KUTENDA kazi, kutumwa, nk., na Mungu aliwapa HESHIMA kwa maana ni AHADI kwa watu “wanaomtumikia”…Heshima itaendelea maadam wapo kazini …Sasa, wakiwa KAZINI, ukiwavunjia heshima yao, hata kama wamestahili kutukanwa, jua unacheza na MUNGU aliyewatuma. Kuwa makini.
 
Mfalme Daudi alijua siri hii. Akiwa na sababu zote za kumdhuru Sauli, hakuthubutu kunyoosha mkono wake kumgusa. Kumbuka, wakati huo Sauli (masihi) anataka kumuua Daudi, lakini Daudi anaogopa kumpiga kwa sababu na NAFASI yake kama masihi hata kama ana MAKOSA kibinadamu na anastahili adhabu; Ni masihi, usimguse! Daudi,Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA, neno hili, kuunyosha mkono wangu juu yake, kwa maana yeye ni masihi wa BWANA” (1 Samweli 24:6).
 
 
Ukisoma 2 Samweli 1:1-16, utaona hadithi nzima, jinsi Daudi alichukulia serious suala la masihi wa Bwana. Kwenye hadithi hii, Sauli anakufa kwa sababu “alimwomba mtu amuue” baada ya kujeruhiwa sana vitani. Pamoja na kwamba aliomba mwenyewe auwawe, na hapakuwa na namna kwamba angepona, Daudi alimkasirikia sana mtu aliyemuua (aliyemmalizia) Sauli; akaamuru naye auwawe kwa upanga!  Yaani Daudi anamshangaa jamaa kapata wapi ujasiri! “Daudi akamwambia, Jinsi gani hukuogopa kuunyosha mkono wako umwangamize masihi wa BWANA?”  (2 Samweli 1:14).
 
 
Mtume Paulo naye alijua siri hii pia, “Paulo akasema, Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa, Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako(Matendo ya Mitume 23:5).
 
Haya ni maagizo ya Mungu tangu zamani hata leo. Sawa, masihi nao wanamakosa kama wanadamu, ila BWANA anasema MSIWAGUSE! Kila mtu kwa bwana wake ataanguka au kusimama, wewe ni nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? (Warumi 14:4).
 “Usimtukane Mungu, wala usimlaani mkuu wa watu wako(Kutoka 22:28).
Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu (1 Mambo ya Nyakati 16:22; Zaburi 105:15).
 
 
Frank P. Seth

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni: