Jumanne, 5 Aprili 2016

SIRI ZA JANGWANI SEHEMU YA PILI BY Frank P. Seth

 



 
Kuna mambo kadhaa ya kukumbuka UPITAPO jangwani:

1.      Ni marufuku kuchoka/kukata tamaa/ kuzimia roho. Kuchoka ni kikwazo cha mavuno yako.
9 Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho” (Wagalatia 6:9). 
Nikiangalia katika Wagalatia 6:9, naona kwamba kuna uwezekano wa kupanda mbegu, yamkini na kupalilia, hata kunyeshea, lakini KUSUBIRI kwa muda mrefu, katika hali ngumu (jangwani), inaweza kuleta hali ya KUKATA TAMAA/KUCHOKA/KUZIMIA MOYO, ambayo hali hii inazimisha UWEZO wako wa kuvuna (kupata majibu ya maombi yako au kupata matarajio yako kule ng’ambo ya jagwa).
 
2.      Manun’guniko ni kivutio cha adhabu badala ya msaada.
 
5Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. 6BWANA akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. 7Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa BWANA, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu” (Hesabu 21:5-7)

Angalia maneno yako unapopita jangwani. Mara nyingi ni rahisi kunung’unika kwa sababu ya adha mbaliambalia unazopitia. Utakuta mtu anaanza tu kusema, “kwa hali hii, mi naona maisha ya wokovu ni magumu sana”, “aheri hata ndoa za wamataifa, naona yangu ni mateso tu”, “yaani pamoja na kumtumikia Mungu bado nateseka kuliko watenda dhambi”, “sasa unafikiri mtu ataishije namna hii?”, “hata Mungu anaona kwamba nimevumilia muda mrefu”, n.k. Haya ni maneno ya mtu aliyechoka na yamkini sasa anajifariji wakati anatafuta namna ya “kuchepuka” apitapo jangwani.
 
3.      Kanuni za kula manna; kila chakula (Neno) huja kwa wakati na kusudi maalumu kukufundisha. Elimu ya jangwani ni muhimu kwa maisha ya Kaanani.

35 Na wana wa Israeli walikula Mana muda wa miaka arobaini, hata walipofikilia nchi iliyo na watu, wakala ile Mana, hata walipofikilia mipakani mwa nchi ya Kanaani” (Kutoka 16:35).

Ukiwa jangwani, bado Mungu atakuletea “chakula cha siku”, hadi uvuke hapo. Kumbuka, manna ilikuwa “chakula cha kuokota”, wana wa Israel hawakutafuta, kazi yao ilikuwa ni kuokota tu, tena kwa KANUNI maalumu. Kila siku ilimpasa mtu kukusanya chakula cha siku moja, na siku ya 6 walikusanya chakula cha siku mbili, kwa sababu siku ya Sabato hawakutakiwa kufanya chochote ila kupumzika.

Kumbuka, siku 6 walikusanya chakula cha siku moja (hapakuwa na kiporo), na aliyekusanya zaidi, ile manna iliharibika! Angalia jambo hili, siku ya Sabato manna hiyo hiyo iliweza kudumu siku 2 bila kuharibika! Na, kwenye Sanduku la Agano ipo manna nyingine hata leo haijaharibika, imefichwa hadi kwenye ufalme ujao; watakaoshinda watapewa huko Mbinguni (Ufunuo 2:17).

Uwe makini na chakula (NENO) Mungu analosema nawe ukiwa jangwani. Huja kwa wakati maalumu na kwa kusudi maalumu, hilo Neno ndilo litakuvusha kwenye jangwa lako salama. Hilo Neno haliji holela, linakuja kwa namna maalumu kwa ajili yako. Omba sikio la “kusikilia” ili usikie litamkwapo.
 
4.      Ukimwangalia nyoka wa shaba utapona; Msaada wako unatoka katika Bwana. Yeye aliyakupitisha hapo jangwani anaDAWA ya kila shida yako.
 
8Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi. 9Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi” (Hesabu 21:8,9).

Pamoja na majanga yote ya jagwani, Mungu hufanya “njia ya kutokea”, na msaada ambao imekupasa KUUJUA na KUTII ili weze KUPONA. Watu wengi waliofia jangwani ni kwa sababu ya kukosa UTII. Kumbuka siku zote, kama yuko NYOKA WA SHABA, kuumwa na NYOKA sio tatizo, dawa ipo. Watu wengi wamekatishwa tamaa kwa sababu katika kupita kwao jagwani wamemkosea Mungu (wakaumwa na nyoka za moto), na wemehukumiwa na wanadamu kwamba kwasababu wamemkosea Mungu wataangabia bila shaka! Hivyo, hawakuona sababu tena ya kuinua macho yao na kumwangalia ‘nyoka wa shaba’ ili wapone. Sikiliza, Inua macho yako sasa, angalia juu, Kristo anakuona ulipo, liitie jina lake UTAOKOKA na KUPONYWA kwa maana “kila aliitiaye jina la BWANA ataokoka”.

Yesu hatishwi na dhambi zako, wala hakuchukii wewe kwa sababu ya hayo makosa yako unayohukumiwa nayo; Amekuja kwa ajili ya mtu kama wewe, yaani “amekuja kwa walioDHAIFU wanaohitaji TABIBU”.
 
5.      Urefu wa jangwa unakutegemea wewe na sio Mungu. Kadri UNAVYOJIFUNZA mapema na KUTII ndivyo utafupisha urefu wa njia yako jangwani.

Wakati wana wa Israel walipotoka Misri, kulikuwa na njia fupi ya kufika Kaanani, ila kulikuwa na maadui, hivyo Mungu akawaepusha na vita kwa kuwapitisha MBALI. Sasa ona mambo mawili: Kwanza, Iliwapasa wazunguke umbali mrefu kwa sababu ya HALI yao wenyewe, kwa maana wangepitia VITA mapema, wengi wangekatishwa tamaa kwa sababu aidha HAWAJUI kupigana vita (maana kule Misri hawakujifunza vita ila kazi za ujenzi, na utumishi) au HAWAKUWA tayari kupigana; Njia yao ikawa ndefu. Pili, Baada ya kumkasirisha Mungu, wakiwa karibu kabisa na kuvuka Yordan, waliambiwa “wageuke” kurudi tena nyuma kuelekea jangwani. Hawakuwa tayari kuvukia ile AHADI kwa sababu ya uhaba wa IMANI yao, baada ya Mungu kusema nao kwa namna nyingi [Soma Hesabu mlango wa 13 na 14]. Hapa tena ni wao wenyewe!

Angalia hapa, “24 lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki. 25Basi Mwamaleki na Mkanaani wakaa katika bonde; kesho geukeni, mkaende jangwani kwa njia iendayo Bahari ya Shamu” (Hesabu 14:24). Hawa watu walifika karibu kabisa na nchi ya ahadi, pale ambapo Musa alimtuma Kaleb na wale wengine 11 ili kuipeleleza nchi, na walitumia siku 40 tu kwenda Kaanani na kurudi. Inamaana baada ya miaka 40 jangwani, walibakiza siku hata hazifiki 40 ili kumaliza safari yao, na kuirithi ile AHADI, wakamkorofisha tena Mungu. Wakageukia jangwa kwa upya! Kwa sababu IMANI yao ilitindika, na kuna MAADUI bado! Ila walibakiza kidogo tu wamalize jangwa. Wakashindwa mahali pa kumalizia!

Angalia vita uliyonayo sasa, umepigana vingi, usichoke sasa, hata hii nayo utashinda tu. Simama, utamwona Mungu, jangwa sio la milele, ni njia tu, utavuka.

6.      Nguvu za kuvuka Yordan zinatoka kwa Mungu pia; Usikorofishane na Mungu, hutafika Kaanani, kwa maana bila yeye huna nguvu za kuvuka Yordan.
 
Kumbuka, Kutoka Misri palihitajika MUUJIZA wa kuvuka bahari ya SHAMU, na baada ya jangwa, palihitajika muujiza mwingine wa kuvuka YORDAN ili kuingia Kaanan. Ukikorofishana na Mungu, hata ukikimbilia kwa njia zako hadi ukingoni (ufukweni) mwa Yordan, utavukaje mto? Bado utagundua kwamba unamhitaji tena Mungu. Kuwa mtulivu jangwani. Mwombe Mungu akupe neema ya kutulia kabisa na kuchukua shule zake zote na KUKUA kiIMANI ili ukivuka hapo uingie hatua zingine za Baraka na kufanikiwa.
 

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni: