Kwa ukaribu zaidi ni damu ya muhudumu wa rest house Bi. Bernadeta Alfred aliyelipukiwa na bomu lililowekwa kwenye kifurushi alichokifungua ili kubaini kilichokuwa ndani. |
Hali tete. |
Kishindo kikubwa kilitokea na kutoa sauti kubwa na moshi huku kikisambaza misumari mingi midogomidogo na kujeruhi vibaya mhudumu huyo hasa sehemu za miguuni na usoni. |
MHUDUMU wa nyumba ya kupumzikia
wageni wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, jijijini hapa,
amejeruhiwa vibaya baada ya kulipukiwa na bomu lililokuwa limewekwa kwenye
korido la nyumba hiyo.
Tukio hilo lilitokea jana (Jumatatu), kati ya saa 1:45 na saa 2:20 usiku, katika eneo la Makongoro
wilayani Ilemela wakati mhudumu huyo Bernadetha Alfred (25) alipofungua
kifurushi cha mzigo alichodhani kimesahaulika kwenye eneo hilo, kabla ya
kumlipukia.
Kwa mujibu wa Katibu wa Dayosisi
hiyo, Mollel Rogart, kifurushi hicho kilichokuwa kwenye mfuko mweusi wa
nailoni, kilikuwa juu ya kreti (tupu) za soda, karibu na eneo la kulia chakula
lililopo katika nyumba hiyo.
“Ule mfuko ulikaa pale siku tatu
ndiyo usiku huo mhudumu wetu akakichukua kukiangalia akidhani ni mzigo wa mtu
umesahaulika.” Alieleza Katibu huyo na kudai kuwa kifurushi hicho kilimlipukia
mara tu alipokifungua na kujeruhi vibaya katika sehemu mbalimbali za mwili.
“Bernadetha kajeruhiwa sehemu
mbalimbali za mwili ikiwemo miguuni na usoni na siwezi kusema kwamba chanzo cha
mlipuko huo ni mambo ya kidini japo ulinzi wetu haukuwa mkali kiasi cha
kudhibiti watu walioingia na vitu.” Alisema
Kamanda wa polisi mkoani Mwanza,
Valentino Mlowola akithibitisha tukio hilo, alisema kwamba uchunguzi wa
awali uliofanywa na kikosi maalum kutoka Dar es salaam umebaini kuwa bomu hilo
limetengenezwa kienyeji.
“Bado tunaendelea na uchunguzi wa
tukio hilo ili tubaini ni nani kafanya ili kama ni mtu au kikundi kimehusika
tuchukue hatua haraka. Natoa wito kwa wananchi kutochukua vitu ambavyo hawa
uhakika navyo, wanapoona vitu vya aina hiyo, watoe taarifa kwetu.” Alisema
Kamanda Mulowola.
Mlowola alieleza kuwa, Bernadetha
aliyejeruhiwa vibaya katika sehemu mbalimbali za mwili, alikimbizwa katika
Hospitali ya rufaa ya Bugando ambako anaendelea na matibabu.
Kamanda huyo alieleza kwamba,
mabomu (yakiwemo ya kienyeji) yako katika mifumo mbalimbali hivyo wananchi
hususan wahudumu wa sehemu za mikusanyiko wawe na tahadhari na vitu
vinavyoonekana kusahaulika na wasisite kuwajulisha polisi vinapoonekana hivyo.
Mlipuko huo uliozusha hofu kwa
waumini mbalimbali wakiwemo wa Kanisa hilo, umetokea ikiwa ni wiki moja baada
ya maadhimisho ya ‘Huduma ya Mtoto’ kwa makanisa mbalimbali ya Kikristu jijini
hapa yaliyofanyika kwenye kanisa hilo, yakitanguliwa na maandamano kutoka
uwanja wa furahisha hadi KKKT.
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni