Jumatano, 2 Januari 2013

KADINALI PENGO AZUNGUMZIA KUPIGWA RISASI PADRI ZANZIBAR


Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la  Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo 



ASKOFU wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la  Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo amelaani kitendo cha kupigwa risasi kwa Padri wa kanisa hilo, Parokia ya Mpendaye mjini Zanzibar, Ambrose Mkenda na kusema kitendo hicho hakileti matumaini mema kwa amani ya nchi katika siku za usoni.
Desemba 24 mwaka 2012, Padri Mkenda alipigwa risasi na watu wasiofahamika nje ya nyumba yake na kufikishwa katika Hospitali ya Muhimbili ambako alitolewa risasi mbili.
Jana, Pengo akizungumza katika ibada ya kuukaribisha Mwaka Mpya iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Jijini Dar es Salaam, alisema tukio hilo na vurugu za kuchomwa makanisa ni ushahidi wa wazi kuwa watu hawaitaka amani nchini.
“Padri wetu Zanzibar wakati anapigwa risasi hakuwa anatoka kwenye vilabu vya pombe wala hakuwa katika majumba ya watu, alikuwa anatoka kutimiza majukumu yake ya kiuchungaji lakini akapigwa risasi nje ya nyumba yake, tunakwenda wapi?” alihoji Pengo.
Kadinali Pengo alisema vurugu za kidini zinazoendelea kujitokeza nchini hivi sasa hazileti dalili njema kwa amani ya nchi.
“Hata hao wanaofikiri kuwa wakibaki pekee yao na dini zao watakuwa salama hawapo sahihi kwani kuna nchi hivi sasa zipo katika vurugu ingawa zina imani moja ya dini,” alisema Pengo.
Alisema, “Angalieni nchi kama Tunisia, Algeria na nchi nyiingine hazipo salama ingawa zina imani moja ya dini.”
Alisema wanaochochea vurugu za kidini watambue kuwa hata kama dini nyingine itaondoka na wao kubaki pekee yao hawatabaki  salama.
Kadinali  Pengo aliwataka Watanzania kuwa macho na tofauti ambazo zinaweza kuleta vifo katika jamii kwani tofauti za kidini zisiwe sababu ya kutukanana, kukashifiana kwani dini zote zinatoka kwa baba mmoja hivyo haoni sababu za kujengeana chuki.
Pengo alisema mamlaka ya Serikali siyo kusimamia msingi wa dini yoyote na inachaguliwa na watu wote hivyo kazi yake ni kuwahakikishia watu wa dini zote usalama wao na mali zao na iwapo itashindwa na kuwabagua watu kulingana na imani zao ni wazi kuwa itakuwa imepoteza mwelekeo.
“Watu wa imani zote za dini wanapaswa kulindwa na Watanzania wametakiwa kuliombea Taifa lao ili liweze kudumu katika imani na mataifa mengine yaweze kuiga kutoka kwetu,” alisema Pengo na kuongeza kuwa Taifa linahitaji maombi zaidi kipindi hiki kuliko wakati mwingine.
Padri huyo alitolewa risasi mbili kinywani na hali yake inaendelea vizuri na hadi juzi kulingana na taarifa za Jeshi la Polisi Zanzibar, watu wawili walikuwa wakishikiliwa na jeshi hilo kuhusiana na shambulizi hilo na katika ghasia zilisababisha kuchomwa kwa makanisa Zanzibar na Dar es Salaam watu kadhaa kesi zao zipo mahakamani.
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: