Jumanne, 7 Agosti 2012

PENGO ASEMA UGUMU WA MAISHA UNGEANZIA KWA VIONGOZI


ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema ugumu wa maisha unaowakabili Watanzania sasa, ulipaswa kwanza kujionyesha kwa viongozi wa Serikali.

Kardinali Pengo aliyasema hayo juzi katika kipindi maalumu kilichorushwa na Radio Tumaini, kuadhimisha miaka 68 tangu alipozaliwa Agosti 5 mwaka 1944.

“Hali ngumu kwa Watanzania angalau kwa kiasi fulani ingeanzia kwa viongozi wetu, tukaona kuwa wameshiriki na sio hali ngumu huku wengine wanakula raha mstarehe kwa kula nyama choma kuanzia asubuhi hadi jioni”alisema Kardinali Pengo.

“Watanzania wa kawaida hawana hata fedha ya kununulia Aspirini, maskini wanakufa, tofauti kabisa na ilivyo ka viongozi wetu wa sasa ambao hawana uzalendo,” alisisitiza.Kuhusu vurugu na migomo katika shule mbalimbali nchini, kiongozi huyo wa kidini alisema inachangiwa na watoto wa vigogo wailiokula na kushiba kutokana na utajiri wa wazazi wao.

Aliwataka vijana wasiilalamikir Serikali na kuitaka iwasaidie kwa kuwapatia chakula na badala yake, wajitume katika shughuli za kilimo.

“Tusianze kulia kuhusu maisha magumu na tusianze kulalamika na kumuambia Rais kwamba hatuna hata mchicha, sasa yeye azalishe wapi,na ndio maana tunaona Wachina wanakuja na kuzalisha na baadaye kutuuzia tukiwa ndani ya ardhi yetu” alisema Askofu Pengo.

Pia alisema katika siku za hivi karibuni amekuwa hapati usingizi kila anapofikiria mustakabali wa amani ya nchi na mwelekeo wake hasa baada ya baadhi ya watu kuchomeana makanisa na kutukanana ovyo.

Akizungumzia wazazi wake, Kardinali Pego alisema baba yake (Joseph ) alizaliwa Kaskazini mwa Zambia na mama yake Rozalia, ni Mtanzania.
“Kwa kuzaliwa baba yangu ni Mzambia, lakini alipokuwa mdogo kabisa alivuka na kuingia Tanzania enzi hizo palikuwa hakuna mipaka kama ilivyo hivi sasa,” alisema Askofu Pengo.

Alisema baadaye, wazazi hao walifunga ndoa na kufanikiwa
kuwazaa watoto tisa, watano wakiwa wa kiume na wengine wanne wakiwa wa kike

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: