“Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe” (Mathayo 26:39).
Kwenye maisha kuna MITIHANI mingi, na utakutana na mitihani karibia kila siku. Lakini, kama mtihani haukufikishi mahali pa kumkosea Mungu, mtihani huo bado hauna sifa ya kuitwa JARIBU. Na, kama ni jaribu, lakini halikuondoi kwenye KUSUDI la Mungu kwenye maisha yako, hilo sio jaribu la kutisha.
Kumbuka, ni vigumu kupima JARIBU kwa kutumia amri 10 tu za Mungu. Kwa mfano, Bwana alipojaribiwa na Ibilisi kwa kuambiwa “geuza jiwe liwe mkate”, hakuna mahali UMEKATAZWA kwenye neno (amri za Mungu), kwamba kugeuza jiwe liwe mkate ni KOSA. Je! Tatizo lilikuwa wapi? Tatizo liko kwenye KUSUDI na RATIBA ya Mungu kwa wakati huo.
Ni vyepesi sana kusikia maneno haya na kufikiri ni mepesi tu, “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile” (Yohana 5:19).
Kutembea kwenye KUSUDI ni zaidi ya kutimiza amri 10 za Mungu, ni zaidi sana ya kutii amri za nchi, ni zaidi sana ya kutii amri za kanisa lako, ni zaidi sana tu. Unapofika mahali pa kufanya ZAIDI au PUNGUFU ya kusudi la MUNGU kwenye maisha yako, yaani, kuvuka MPAKA wa neno lilonenwa juu ya maisha yako (Yeremia 1:5), umeingia katika uwanja ambao sio salama sana, hata kama utasifiwa na watu wengi.
Ukitazama majaribu yote matatu BWANA aliyojaribiwa na Ibilisi nyikani (Luka 4:1-13), utagundua kwa jinsi ya kibinadamu, hayana shida, kwa maana inawezekana ikawa ni namna nyingine ya kuonesha “MATENDO MAKUU YA MUNGU”, Je! Baba anataka nini SASA? Bwana Yesu alipotazama, hakumwona Baba “akifanya huo muujiza kwa namna hiyo”, Akagundua ni JARIBU la Ibilisi tu, Akashinda kwa kujua RATIBA ya Mbingu na kwa kufuata UONGOZI wa neno, Akashinda; Alisema, “Imeandikwa!”
Kuna mambo mengi yanahitaji UZOEFU wa kuisikia sauti ya Roho Mtakatifu (Luka 12:12) na kupata NENO la kukumulikia njia yako (Zaburi 119:105) katika mambo unayopitia, ili kupata UONGOZI sahihi wa NJIA ikupasayo kupita (Zaburi 119:11). Pengine popote upitapo, hata kama hakuna mtu anaweza kukuhukumu mkosaji, utakuwa UMEPUNGUA katika njia za BWANA, na hiyo itaATHIRI kusudi lako.
Hebu tuangalie kidogo maana ya KUSUDI
Kusudi la Mungu ni lile jambo MAHUSUS (specific), ambalo uliumbwa ili ulifanye. Mara nyingi, jambo hilo huibuka kama kipaji, matamanio ya moyo wako au ndoto isumbuayo.
Hata hivyo, kuna kusudi la JUMLA (general purpose) na kusudi MAHUSUS (specific purpose). Kwa mfano, kama umeoa, kuna kusudi la Mungu kwako kama baba wa familia na mume, hilo ni kusudi la jumla la wanaume wote ambao ni mume na baba. Pamoja na kusudi hilo la jumla, kuna kusudi jingine mahusus ambalo ni lako binafsi. Kwa mfano, wewe ni mwimbaji. Kwahiyo, tofauti ya mbaba mmoja na mwingine itakuwa katika kusudi mahusus.
Mfano mwingine. Kuokoka ni kusudi la jumla, ambalo linajumuisha kundi kubwa la watu. Katika hilo kundi, kuna makusudi mahusus kwa kila mmoja. Je! Kusudi lako mahusus ni lipi? Ni kazi yako kujua na kulitimiza. Mwombe Mungu na JICHUNGUZE kulitambua kwa maana limo NDANI yako, Unatembea na kusudi hilo ndani yako.
Kama kuna kitu cha kwanza, Ibilisi angependa usijue, ni KUSUDI lako. Atakuletea kila “rangi” na “utamu” wa dunia hii, ilimradi tu umejisahau. Kwa mfano, ulidhani Ibilisi alipomjaribu Hawa pale Eden, unadhani alitaka Hawa “anogewe” tu na tunda? Unadhani “alimhurumia” sana na njaa? Lengo la KWANZA la adui lilikuwa ni KUMTOA KWENYE KUSUDI la Mungu; wala agenda haikuwa kula tunda! Kama mpaka leo unashangilia “matunda” mbalimbali yanayokujia, angalia KUSUDI la Ibilisi, utagundua agenda ya Ibilisi sio tunda, ila KUUA kusudi la Mungu maishani mwako.
Sasa turudi kwenye JARIBU. Kama kuna jambo linaKUSUKUMA (jaribu lina tabia ya kusukuma/kuvuta/kushawishi mtu kwa nguvu), na jambo hilo linakufanya aidha UMKOSEE Mungu au ushindwe kutimiza KUSUDI lako, hilo jambo linaitwa JARIBU baya.
Nataka ujue jambo hili, huwezi kuishi bila KUKOSEA, yaani, huwezi kuwa mkamilifu kama alivyo Mungu. Utajaribiwa na utakosea au kushindwa mara nyingi tu, hiyo haimsumbui Mungu, wala dhambi sio tishio sana kwa Mungu, ila kama UKIPOTEZA KUSUDI la Mungu alilokuumbia kulifanya, hiyo ni SHIDA kubwa!
Nataka ujue jambo hili, lengo hasa la Ibilisi sio utende dhambi, ila kukondoa kwenye KUSUDI la Mungu. Kwa maana hii, kama Ibilisi ataweza kukushawishi (kukujaribu) na ukafeli mtihani (ukaangukia majaribuni), lakini ukaweza tena KUSIMAMA na KUTIMIZA KUSUDI la Mungu, maana yake, wewe ni MSHINDI.
Siku ya MWISHO hutaulizwa ulishindwa au ulishinda majaribu mangapi, ila utaulizwa utimilifu wa KUSUDI la Mungu! Hata hivyo, kufanya dhambi, yaani kushindwa majaribu katika hatua ya kwanza, kutakupelekea kushindwa hatua ya pili, ambayo ni kushindwa kutimiza KUSUDI la Mungu.
#Frank_P_Seth
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Mawazo yako ni muhimu sana tafadhali tumia lugha nzuri na tutairusha na wengine waisome.