Jumamosi, 15 Julai 2017

NGUVU katika KUJIKUBALI


 
 
14 Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi. 15 Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda. 16Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema. 17Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu 18 Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati. 19Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. 20Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. 21Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya. 22Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, 23 lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu. 24Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? 25Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi” (Warumi 7:14-25).
 
Kama kuna kitu Ibilisi ameweza wengi, ni kuwashawishi kwamba “wameshindwa na watashindwa kwa sababu ya MADHAIFU yao” au kuwaambia, “hawastahili kwa sababu bado hawajakamilika” au “kikwazo chao ni udhaifu wao!”  
 
Nakuletea ujumbe huu leo, ukisubiri hadi uwe MKAMILIFU ili ndio ufanye KUSUDI la Mungu kwenye maisha yako, utasubiri milele.
 
Kusidi la Adui KUKUZOMEA kila mara ni kukuvunja IMANI na UJASIRI wa kufanya chochote, na pasipo imani hutafanikiwa sana. Sio katika HUDUMA tu, ila katika kila utiayo mkono wako kutenda, hutafanikiwa.
  
Kweli, bado hatujakamilika, ila tuko mikononi mwa Mfinyanzi. Kadri tunatenda kazi, tunafinyangwa na KUBADILISHWA na kukua UTUKUFU hadi UTUKUFU! Hatukui kwa sababu sisi ni wakamilifu, ila kwa kuwa ALIYETUITA ni MWAMINIFU na atahakikisha kwamba “yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu” (Wafilipi 1:6).
  
Angalia tena, “yeye aliyeanza kazi njema”, Sasa wewe u nani unayesubiri uwe MKAMILIFU ili “UANZISHE” kazi njema mwenyewe? Je! Si Bwana aliyekwisha anzisha kazi njema ndani yako? Mbona upo katika kusitasita kwa sababu Ibilisi anakuonesha madhaifu yako na HUMTAZAMI yeye Aliyekuita?
  
Ukiangalia Warumi 7:14-25, utaona kabisa Paulo anasimulia VITA katika mwili wake; Udhaifu anaopambana nao. Lakini ni Paulo yule yule ambaye ameandika zaidi ya nusu ya Agano Jipya! Ni Paulo yule yule aliyesema “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda” (2 Timothy 4:7). Lakini pia ni Paulo huyu huyu aliyesema “sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda! (Warumi 7:15). Je! Alianza lini KUPIGA mbio hadi amemaliza mwendo kwa ushindi wakati ni dhaifu hivi? Je! Ni baada ya kufikilia utimilifu wa Kristo (Waefeso 4:13) ndipo alipoanza kazi?
 
Nisikilize, Ibilisi atakuja na HADITHI za kale, kukuonesha kila MAKOSA yako na MADHAIFU yako, kisha atakwambia HUSTAHILI chochote na wala hutaweza chochote. Sawa, ni kweli UMEKOSEA sana, umefanya DHAMBI nyingi, lakini mwambie Ibilisi, “UBORA wangu haupo katika ukamilifu wangu, ila upo katika UKAMILIFU wa Mungu aliyeniita ambaye ni MWAMINIFU. Mungu alinijua kabla sijazaliwa na aliweka KUSUDI lake ndani yangu kabla sijazaliwa na NITALITIMILIZA na KULIMALIZA!”
 
Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa” (Yeremia 1:5).
 
Hebu fikiri Baba anamwambia Bwana Yesu, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye” (Mathayo 3:17). Hapo bado kabisa Bwana hajafanya muujiza hata mmoja, bado Hajafufua wafu, bado Hajapanda msalabani, bado Hajapambana na Herode na kumwita Mbweha! (Luka 13:32); Bado hajafika mahali pa kubanwa hadi anatamani kukimbia mapenzi ya Mungu (anataka kikombe kimwepuke) (Mathayo 26:42)! Sikiliza, Mungu alipendezwa Naye hivyo hivyo!
  
Bwana anamtazama Petro, anaona atakavyopepetwa na Ibilisi kama ngano (Luka 22:31), anaona jinsi ambavyo Petro atamkana mara tatu (Mathayo 26:34), Bwana anaona! Kisha anamtazama Petro, anamwita wewe ni Kefa, yaani jiwe (Yohana 1:42), na katika mwamba huu nitalijenga kanisa langu wala milango ya Kuzimu haitaliweza! (Mathayo 16:18). Huyu ni Petro yule yule aliyefeli practical ya kutembea juu ya maji (kwa sababu ya imani haba) mbele za Bwana na mitume wenzake! (Mathayo 14:30) Petro huyu huyu!
 
Nisikilize, Bwana anasema, “1 Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. 2Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. 3Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia” (Yohana 15:1-3). Kama tawi linasafishwa ili liweze kuzaa zaidi, inamaa hili tawi lilianza kuzaa lakini bado linahitaji kusafishwa! Halikuwa KAMILIFU wakati likianza kuzaa matunda! Linazidi kusafishwa muda baada ya muda!
  
Pamoja na kwamba ni tawi chafu, bado lipo kwenye Mzabibu (ndani ya Yesu), naye Bwana anashughulika na hilo tawi kwa NENO lake mara kwa mara kuendelea kulisafisha ili lizae zaidi.
 
Hata wewe hapo, unajijua hujakamilika, ila imekupasa kuanza KUZAA matunda sawa na WITO wako, kwa maana lipo KUSUDI lako ambalo ni LAZIMA uzae tu! Kazi ya kusafisha ni ya BABA; Kadri unavyorudi kwake na matunda, yeye Atakusafisha, ndio kazi Yake! Wewe kazi yako ni kuzaa matunda tu!
 
Nimesikia wapendwa WAKISENGENYA wengine kwa madhaifu yao, na kuwashangaa, kwamba, “kwanini wanafanya KAZI NJEMA wakati wao ni wadhaifu?” Je! Wamesahau kwamba wenzao ni wadhaifu “kule” ila wao nao ni wadhaifu kwa “kuwasengenya wenzao”? Je! Nani amzuie mwingine mkono afanyapo kazi ya Bwana kwa kumhukumu udhaifu wake? Je! Wewe usengenyaye unahaki juu ya mzinzi? Na wewe Mwongo je, una haki juu ya muuaji?
 
 “Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha” (Warumi 14:4).
 
Neema na Amani ya Kristo na vizidi kwenu tangu sasa na hata milele. Amen.

Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu” (Warumi 10:10).
 
 
Hivi unajua ni kwanini hata sasa hujapiga hatua yoyote ya maana katika kukua katika Kristo na kumtumikia? Unajua ni kwanini unajitahidi kufunga na kuomba na kukemea dhambi autabia fulani halafu kesho yake unafanya hiyohiyo halafu unabaki kujishangaa na kujifariji kwa maneno yasiyo na maana? Hivi unajua ni kwanini hata katika mambo yako ya kawaida ya kiuchumi na maisha upo kama umefungwa kamba mguuni?
 
 
Jibu la maswali hayo yote ni rahisi, “kwa kinywa hukiri na kupata wokovu”! Kweli unaamini moyoni mwako, kweli unapenda kumtii Mungu moyoni mwako, lakini usipochukua hatua nyingine ya kukiri, huwezi kuokoka kwenye hiyo hali inayokusumbua kamwe.
 
 
Hebu chukua hatua ya imani, kiri (tamka) mbele za mtu au hiyo hali inayokusumbua, sema maneno ya imani, hata unapoona ni ngumu sana, tamka kwa ujasiri maneno ya imani usoni mwake, kama nabii Elisha alivyotamka mbele ya mto Yoridan, akausemesha mto!
 
Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi BWANA, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka” (2 Wafalme 2:14).
 
 
Ukianza kufanya hivyo kwa ujasiri, utagundua yule mtu, au ile hali inaanza kukutii na wewe unapata ushindi dhidi yake. Lakini ukijifungia ndani unakemea tu mwenyewe, na ukitoka kukabiliana na jaribu lako unafumba kinywa, utakuwa umekosea kanuni ya muhimu ya “kupata wokovu”! Kumwamini Mungu ni vyema, kwa maana unapata HAKI ya kushinda, lakini wakovu unapatikana kwa KUKIRI unachokiamini!
 
 
Sasa angalia Ibilisi anachofanya ili ushindwe kupata wokovu. Anakuletea AIBU!
 
 “Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu” (Marko 8:38).
Hivi unadhani kumwonea haya (aibu) Yesu na maneno yake inamaanisha kuonea haya neno lililopo moyoni mwako? Unadhani ukiamini moyoni mwako na kufumba kinywa umevuka mahali? Kweli imani huja kwa kusikia, na imani inakaa kwenye nafsi yako, na, ndani ya moyo wako unapokea HAKI kwa sababu ya ile imani ndani yako, lakini imani pasipo matendo imekufa! Ipo nafsini mwako, lakini imekufa, haitaweza KUZAA kwa maana umeshindwa KUCHUKUA hatua nyingine ya KUKIRI au KUTENDA hata ukapata wokovu!
 
 
Humsumbui Ibilisi kwa kusoma biblia nzima, kila siku unakazana na milango 20 na kusikiliza mahubiri ya watumishi mashuhuri duniani, kama hujafikia hatua ya KUKIRI, hasa kutamka hayo maneno mbele ya JARIBU lako, hutaweza kupata wakovu bado! Wala haimsumbui sana Ibilisi kama unajua kila elimu ya Mungu kwa usahihi, Je! Unaweza KUKIRI kwa UJASIRI mbele ya JARIBU lako?
 
 
Kumbuka neno hili, Kinachukufanya ushindwe KUMRI YESU ni AIBU! Unamwonea aibu Yesu mbele ya huyu mtu au jaribu lako! Hutavuka kwa kukimbia na kujitenga mbali, anza kutokeza kwa ujasiri, mkiri Yesu usoni mwake, songa mbele kwa ujasiri! Ibilisi ndiye anapaswa kukimbia kwa kukemewa! Sio wewe unamkimbia Ibilisi! Imani yako iko wapi?
 
Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia” (Yakobo 4:7). Kabla Ibilisi, mshitaki wetu, hajakimbia baada ya kukemewa, anakuchungulia kwanza kama unamtii Mungu. Akiona humtii, anapeleka mashitaka kama alivyofanya kwa Ayubu! Usiogope mashitaka ya Adui, toba yako itakupa ujasiri wa kusimama tena mbela za Adui yako na kumkemea kwa ujasiri. Kwa maana, ukitubu unasafishwa ghafla! Na wala dhambi zako hazitakubukwa tena mbele za Mungu. Mwambie Ibilisi, “Mungu hakumbuki hiyo kitu..”
 
 
Je! Umeshindwa kujikubali kwamba wewe ni mwana wa Mungu? Kama hujajikubali mbele za hao watu kwamba umeokoka (katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi), nani atakayekukubali? Dalili ya kwanza ya kushindwa kujikubali ni AIBU juu ya hicho kitu unachodhani umekikubali. Yaani, umemkubali Yesu ila wewe hujajikubali ndio maana unajikunyata na kujificha, wala hutamki hata neno moja au hata jina la Yesu kwa sababu ya aibu usoni mwa ADUI za Mungu!
 
 
Sasa angalia, haijalishi jana tu ulifanya nini, anza kukiri leo! Wakati wanakushangaa na kukukejeli kwamba “hata wewe unaweza kuniambi hivi wakati jana tu..” wewe jibu, “Ndio, ilikuwa jana, saa ya wokovu ni sasa, mimi sio yule wa jana, nimetubu nasonga mbele…” Watarudi tena kuuliza swali hilo hilo kama uko serious, wakija mara kadhaa na wewe ukawajibu kwa UJASIRI maneno yale yale, utashangaa kitakachotokea, “utapata wokovu”!
 
 
Jambo jingine, yale maneno uliyotamka ni roho! Hayatakaa kimya, yataendela kutamka masikioni “mwao”, ndani ya nafsi zao! Miaka mingi hayatakaa kimya, hata wakiendelea na tabia yao mbaya na kufuata watu wengine, kila wakienda katika hali kama hiyo tena kwa mtu mwingine, yale maneno uliyowatamkia yatawarudia, siku moja wataamua kuokoka, kumbe! Ulimshuhudia Yesu kwao hata katika hali hiyo nao wakaokoka! Injili ni kumshuhudia Yesu! [Yaani mfanye adui ya Mungu akikukumbuka, akumbuke neno la Mungu ulilomwambia, sio uovu mliofanya naye].
 
 “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima” (Yohana 6:63).
 
 
Katika somo hili sehemu ya kwanza, tuliona kikwazo cha kusonga mbele, ambacho Adui anakushawishi kwamba “huwezi au hutaweza kwa sababu wewe sio mkamilifu”, yaani anatumia hali yako ya sasa au iliyopita kukudanganya kwamba hutaweza kushinda kesho! Siri ipo katika KUANZA hivyo hivyo bila AIBU. JIKUBALI ukiwa katika hali yako hiyo hiyo, anza kuchukua hatua. Kadri unachukua hatua moja ndogo ya imani, unasafishwa na BABA (Yohana 15:1-3), na unaongezeka kufanya kazi njema (kuzaa matunda zaidi), ukichukua hatua ndogo tena ya pili, utaendelea kukua. Usisikilize adui zako wakikuzomea, pambana, songa mbele, siku moja hao wakujaribuo watakaa kimya mbele zako na watajua kwamba kweli kuna wokovu dunia!

Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia” (Warumi 1:16).
 
 Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu” (2 Timothy 1:8)
 
Kwanini mtume Paulo alisisitiza kwamba “haionei haya Injili”? Na, akamwonya mtoto wake wa kiroho Timotheo kwamba, “usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu na wala usinionee haya mimi (Paulo)”?
 
Nitakuonesha jambo. Unakumbuka pigo la utasa alilopigwa Mikali, mke wa kwanza wa Daudi? (2 Samweli 6:23) Mikali alipigwa utasa kwa sababu alipomtazama mumewe akicheza na vazi lake kufunuka mbele ya vijakazi wake, akaona kama “mfalme kajidhalilisha sana mbele za watu kwa ajili ya kucheza mbele za Bwana”! Au, “mfalme ANANIAIBISHA mimi jinsi anavyocheza mbele za hao vijakazi wangu!” (kwa maana Mikali alikuwa malkia). Mikali AKAMDHARAU Daudi! (2 Samweli 6:16) Japo dharau hiyo lilikuwa MOYONI, Mungu alisikia, aliona, Akampiga Mikali kwa utasa hata kufa kwake!
 
14Daudi akacheza mbele za BWANA kwa nguvu zake zote; na Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani. 16Ikawa, sanduku la BWANA lilipoingia mji wa Daudi Mikali, binti Sauli, akachungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi akiruka-ruka na kucheza mbele za BWANA; akamdharau moyoni mwake. 20Ndipo Daudi akarudi ili awabarikie watu wa nyumbani mwake. Na Mikali, binti Sauli, akatoka nje aende kumlaki Daudi, naye akasema, Mfalme wa Israeli alikuwa mtukufu leo namna gani, akijifunua mwili wake mbele ya vijakazi vya watumishi wake, mfano wa watu baradhuli mmojawapo, ajifunuavyo mwili wake mbele ya watuasipokuwa na haya! 21Daudi akamwambia Mikali, Ilikuwa mbele za BWANA, aliyenichagua mimi juu ya baba yako, na juu ya nyumba yake, ili kuniweka niwe mkuu juu ya watu wa BWANA, juu ya Israeli; kwa hiyo mimi nitacheza mbele za BWANA. 22Kisha nitakuwa hafifu zaidi, nami nitakuwa mnyonge machoni pangu mimi mwenyewe; lakini kwa wale vijakazi uliowanena, kwao nitaheshimiwa. 23Basi Mikali, binti Sauli, hakuwa na mtoto hata siku ya kufa kwake” (2 Samweli 6:14, 16, 20-23).
 
Paulo, mtume, akamwonya Timotheo kwamba, asije akafika mahali kaanza kuuonea aibu USHUHUDA wa Bwana wetu na wala simwonee aibu yeye, Paulo, mtumishi wa Bwana. Umewahi kusikia mtu amefika mahali pa kujionea aibu mbele za watu kwa sababu ameokoka? Au, anajisikia aibu kwa sababu mkewe/mumewe anamtumikia Mungu na watu wanajua? Yaani, kila akifikiri kwamba “watu fulani” wanamtazama mke/mume wake kama “mtumishi”, yeye anasikia AIBU (HAYA)! Hichi ndicho Paulo alimwambia Timotheo, “usinionee aibu mimi mtumwa wa Kristo”; Ndicho kilimgharimu Mikali!
 
Tatizo ni nini hasa? Kama tulivyoona kwenye mfululizo wa somo hili, sehemu ya I & II, hii ni shida ya kushindwa “kujikubali”. Umeokoka, sawa, je! Unajikubali kuwa hivyo? Unajisikia FAHARI mbele za watu kuokoka? Nini hasa kusudi lako la kuokoka? Je! Ulimfuata Bwana kwa sababu ya “ile mikate”? (Marko 8:8) au “unyasi kutikiswa na upepo”? (Mathayo 11:7) au “kuangalia maonesho ya miujiza”? (Mathayo 16:4) au “kwa sababu ulikuwa na shida”? (Kumbukumbu la Torati 8:11-16) au “kwa sababu uliogopa zile nyoka za moto kule jangwani”? (Hesabu 21:6) au “kumpenda Bwana”? (Danieli 3:17,18) Hutaweza kujibu wewe, ila matendo yako yataonesha “ukiisha kuvuka Yordani”, mali zako na pesa zako zitakapoongezeka, utakapopata mke/mume mzuri, na kujenga nyumba nzuri, taabu yako kwisha, na kila kitu chako kitakapoongezeka sana (Kumbukumbu la Torati 8:11-16), ndipo tutajua kwamba unampenda Mungu kweli.
 
17Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. 18Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha” (Daniel 3:17, 18). Shedrak, Meshak na Abednego walimaanisha kwamba, “kuliko tuabudu sanamu, aheri tufe”!
 
Je! Hujaona watu wanabadilika kutegemeana na “mazingira” fulani? Wakiwa kanisani ni tofauti na wakiwa kazini! Wakiwa na wapendwa lugha yao ni tofauti na wakiwa na watu wengine! Hiyo inaweza isiwe shida, chungulia ndani yako, je! Unafanya hivyo kwa sababu unaonea AIBU ushuhuda wa BWANA? Je! Unajionea AIBU mbele za hao watu?
 
Kabla hujaenda mbali, kumbuka habari za mfalme Sauli, alivyofanya mambo “yasiyopaswa” kwa sababu aliwaogopa hao watu aliokuwa nao! Alidhani heshima yake kwao ni muhimu sana kuliko kumheshimu Mungu, ufalme wake ukararuliwa ghafla! (1 Samweli 15:24).
 
“24 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya BWANA, pia na maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao (1 Samweli 15:24).
 
Chunga AIBU yako mbele za hao watu, siku utakapoJIKUBALI, utashangaa! Kumwonea BWANA aibu kwako kutatoweka. Utaanza kujisikia FAHARI mbele za hao watu kwamba umeokoka, tena UTATAMANI kila mtu ajue kwamba umeokoka. Utaanza kujisikia furaha na fahari kumtumikia Mungu wala hutakosa tena UHURU mbele zao. Ukifika hapo utakuwa umefanikiwa kujikubali.
 
#Frank_P_Seth

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Mawazo yako ni muhimu sana tafadhali tumia lugha nzuri na tutairusha na wengine waisome.