Jumanne, 21 Februari 2017

Kwanini HUKUI wala KUONGEZEKA?


 

Image may contain: 1 person, standing


Sehemu ya I


Mungu ana mpango mzuri na maisha yako, naam, kuna mahali anataka kukuinua, tena pakubwa na pazuri tu, ila uko kama umekwama.


Unatamani kazi, mume/mke, gari, nyumba, maisha ya amani na furaha, afya njema, watoto, elimu, shamba, nk. Nisikilize, Mungu anaweza kukuinua na kufikilia maono au malengo yako. Sababu moja kubwa ni kwamba, wote tumeumbiwa KUKUA na KUONGEZEKA. Kudumaa sio mpango wa Mungu.


Kama hatunabudi KUKUA na KUONGEZEKA, shida iko wapi? Mbona husogei? Mbona maisha kama yanarudi nyuma badala ya kwenda mbele? Angalia mambo machache:


Kwanza: Maarifa (Elimu);


Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako” (Mithali 4:13).


Jiulize maswali yafuatayo: Je! Una maarifa ya kutosha kwenye kitu unachotaka kufanya? Ni vyema kujisomea VITABU au kusikiliza MAKALA mbalimbali kwenye eneo unalotaka kukua, lakini ujue, HUTAMALIZA maarifa. Jipange kujifunza.


Sawa, huna maarifa ya kutosha, na wala hutamaliza maarifa yote kwenye eneo unalotaka KUKUA, sasa Je! Umeanza kuchukua hatua zako SAHIHI kuelekea NDOTO/ MALENGO yako? Kuna mambo hutaweza kuelewa hadi utakapoanza kuchukua hatua za kufanya kwa VITENDO. Mungu hakuwafundisha wana wa Israel habari za Jagwani kwa nadharia, habari za kuvuka bahari ya Shamu kwa maneno tu; Aliwafundisha kwa VITENDO. Maarifa mengi sana ya MSAADA mkubwa kwako hayopo kitabuni wala darasani, yapo utakapoanza kuTHUBUTU kuchukua hatua.


Kumbuka huhitaji digirii cha chuo kikuu ndio useme una maarifa ya kutosha, chukua hatua wakati maarifa yanaongezeka, utashanagaa kumbe ULIWEZA ila hukujua tu. Wengi waliofanikiwa hawakuwa na mavyeti makubwa makubwa, sifa yao moja ya kufanana ni UTHUBUTU!

Sehemu ya II
Pili: NGUVU (Mtaji wako);
 
Jiulize, Je! Una NGUVU za kutosha kufikilia MALENGO au MAONO yako?
Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo” (Kumbukumbu la Torati 8:18).
Jambo moja nakuhakikishia leo, huwezi kufanikiwa bila NGUVU. Kama Bwana ni guvu zako, Yeye atakupa nguvu katika NIA na KUTENDA na wala hutakuwa kama ulivyo. Zitake nguvu zake nawe utasonga mbele.
 
Jifunze mambo mawili: Kwanza, kuna nguvu za KUSOGA mbele na Pili, kuna nguvu za kushinda UPINZANI wa MAadui. Kama unafanya jambo jema, upinzani ni LAZIMA! Hutashinda kwa kuwa una MTAJI au MIPANGO mizuri. Sawa, una mtaji wa kutosha na mipango mizuri, Je! NGUVU na kushinda USHINDANI wa adui zako utapata wapi? Kwa maana hii, katika mtaji wako usisahau kwamba NGUVU za Mungu ni mtaji pia; Ukishafanya faida, usimsahau Aliyekupa mtaji.

Usishangae kwamba wamataifa huenda kutafuta mazindiko kwa ulinzi wa biashara zao, unadhani hawajui wafanyalo? Kama wao wanaenda kufanya haya yote ili wafanikiwe, kwanini wewe usitafute NGUVU kwa Mungu wako? Mtafuteni yeye na NGUVU zake; Nguvu za Mungu ni mtaji kwako!
Mtakeni BWANA na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote” (1 Nya. 16:11; Zab. 105:4)
Sehemu ya III
 
Tatu: UTULIVU (Concentration/Attention/Focusing);
 
10Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula;11ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma” (Isaya 55:10, 11).
 
Shetani hawezi kumzuia Mungu kufanya jambo lolote, ila anaweza kuharibu UTULIVU wako wa ndani ili upoteze MWELEKEO (UELEKEVU) kwa Mungu na UKOSE kupokea mambo yako mazuri kutoka kwa Mungu.
Kwa maana macho ya BWANA hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake. Kwa hayo umetenda upumbavu; kwani tangu sasa utakuwa na vita” (2 Mambo ya Nyakati 16:9).
 
Kwa mfano, umewahi kujiuliza wakati unakaribia kuchumbiwa ndio majamaa ya hovyo na waume za watu wanakuja hapo kati yenu kuharibu utulivu wako? Karibia na mitihani ndipo mchumba anaibuka, ili ufeli? Karibia na kupata mavuno ya taabu yenu baada ya ndoa ya miaka 10 ndio anaibuka mwanume/mwanamke anakuchanganya hadi unafikiri ndio unaanza mapenzi leo? Karibia unapata peromesheni kazini ndio unaletewa pesa za bure nyingi ila chafu? Umebeba mimba kwa taabu na maumivu, Karibia unajifungua baada ya taabu nyingi ndio visirani vinaibuka kila upande ili mimba iharibike? nk. Ukiona haya yote, jua Ibilisi hawezi kuzui BARAKA zako ila anaweza kuondoa UTULIVU wako wa ndani ili USIPOKEE mambo yako mazuri.
 
Nitakwambia jambo, Shetani hana ugomvi na Mungu kila saa, na wala si kweli kwamba anaogopa upako wako au uchamungu wako; adui atakuja kukuzonga tu. Kama BWANA alikaa nyikani siku 40, akiwa amejaa Nguvu za Mungu na Ibilisi akaja KARIBU na akamjaribu, itakuwa wewe? Kama Ayubu na CV yake bora kabisa, akiwa mbele za Bwana, na Ibilisi naye anasonga karibu, hata anapata UJASIRI wa kupiga-stori na Mungu, unadhani unamtisha Shetani wewe?
 
Siri ipo katika kutii kanuni za NENO la Mungu, Ndio maana mara zote, pale nyikani, Akijaribiwa, Bwana Yesu alisema, “imeandikwa….” Akashinda majaribu yake. Kwa Ayubu pia, wakati mkewe anajaribu kuondoa UTULIVU wa mumuwe kwa maneno yake mengi ya ushawishi, Ayubu anasimama kwenye UJUZI wake wa mambo ya Mungu, na anajibu kwa UZOEFU wa siku nyingi wa kumjua Mungu wake na sio kwa “hali halisi” ya sasa ya majaribu mazito (soma Ayubu 1).
 
Neno la Mungu litakuvusha. Usitarajie ushindi mzuri kwa kutumia janja-janja za mitaani. Hapo Adui atakuzungusha milima yote hadi utakaposema, “Yatosha, nimezunguka mlima huu muda mrefu, sasa nasonga mbele”..ndipo utakapopata upenyo, maana hapo ndipo BWANA ataanza nawe safari ya kuelekea njia zako za KUKUA na KUONGEZEKA; Ila kwa KANUNI za kimungu.
 “Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali(Timotheo 2:5).

Sehemu ya IV
 
Nne: KIPAJI MAALUMU

Kikwazo kikubwa kinachosumbua watu ni kudhani wanaofanya mambo maalumu ni watu maalumu na wenye vipaji maalumu, kumbe! Hata wewe unaweza na tena umewazidi wengi. Mbona huchukui hatua?
28 Naye Eliabu, mkubwa wake, alisikia hapo alipoongea na watu; na hasira yake Eliabu ikawaka juu ya Daudi, akasema, Mbona wewe umeshuka hapa? Na kondoo wale wachache umemwachia nani kule nyikani? Mimi nakujua kiburi chako, na ubaya wa moyo wako; maana umeshuka ili upate kuvitazama vita. […..…..] 33Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake” (1 Samweli 17: 28, 33).
 
            Usidanganyike na vigezo vya watu waliojiwekea juu ya hatua fulani za maendeleo. Wengi sana waliofanikiwa wamevunja HOFU zao na kuanza kufanya mambo wakajikuta wameweza, againt all odds! 
 
Fikiri Eliabu, kaka yake mkubwa na Daudi, ana uzoefu wa kutosha sana kutoa tathmini ya Daudi kwa maana anamjua vyema tangu utotoni. Wameishi nyumba moja, anajua UWEZO wake, kumbe! Hakujua “uwezo wake WOTE”! Mfalme Sauli naye akimtazama Daudi kwa vigezo vya KIJESHI, haoni kitu chochote cha kutia matumaini, anaona “kijana tu”! tena mweroro. Anajaribu kuangalia VIGEZO vya kijeshi vya Goliath anagundua kwamba Goliath ana vigezo vya kutosha tena vya kutisha. Hivi ndivyo ambavyo wengi wetu TUMEJITATHIMI au KUTATHMINIWA na watu wengine na tumekatishwa tamaa kwa sababu TUMESIKILIZA sauti zao.
 
Sikwambii kusikiliza USHAURI wa kitaalamu ni kitu kibaya; Imekupasa kusikiliza ushauri, hasa kwa watu waliokutangulia, lakini leo nakwambia neno hili, kama Sauli alivyokuwa mtu wa vita siku nyingi, na hakuweza kuona UWEZO WOTE wa Daudi, ndivyo na wewe utakavyokutana na wataalamu, wakakuona wewe ni “kijana tu”, kumbe! Iko nguvu kubwa na UWEZO wasioujua hadi utakapodhihirika pale utakapoamua kuchukua hatua za kuthubutu. Kumbuka sehemu ya kwanza ya somo hili, UTHUBUTU wa KUCHUKUA hatua ndio utakaoonesha kwamba UNAWEZA.
 
Zingatia jambo hili, watu wengi waliofanya mageuzi duniani, sio wale tu “wanaofikiri nje ya box” bali hata wale “walioko nje ya box” pia. Nitakupa mifano michache. Bill Gates na mapinduzi yake yote ya Computer software, hakuwa “computer scientist”. Angalia akina Steve Jobs na kampuni yake ya Apple, hakuwa “computer scientist”; list ni ndefu. Wengi walioambiwa hawafai ndio viongozi wa mageuzi katika nyanja mbalimbali; wala wengine hawana digirii kwenye maeneo hayo ila wako mbele! Watu waliwaona ni “kijana tu”!
 
Weka nia na usihangaike na njia, NIA inajua NJIA ilipo alimradi kuna ONO moyoni mwako, songa mbele; Thubutu, chukua hatua. KUJARIBU na KUSHINDWA ni sehemu ya yale MADARASA ya muhumu ya kupanda na kuongezwa.
 
Kufeli inauma kama ilivyo KUADHIBIWA, lakini ukweli ni kwamba, hakuna aliyefanikwa asiye na NIDHAMU fulani katika eneo fulani; Je! Kuna hatua za kujenga nidhamu zisizo na maumivu? Kufeli na kurudia tena majaribio ya ulichofeli ni dalili kwamba umekomaa kinidhamu! Inauma, inapouma jua UNAJENGEKA. Huhitaji kipaji maalumu ili kufanya jambo maalumu, unahitaji KUJARIBU na NIDHAMU.
 
Kabla hujamaliza, hakikisha unaangalia video hii YouTube, utagundua hapo ulipo una VINGI tayari vya kukufanya UANZE njia yako ya KUKUA na KUONGEZEKA: https://www.youtube.com/watch?v=AJvEoLPLIg8 na https://www.youtube.com/watch?v=nknzSWDcUgA
Mungu awe na roho yako, AMEN.

---------END---------
 
Frank P. Seth




KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Mawazo yako ni muhimu sana tafadhali tumia lugha nzuri na tutairusha na wengine waisome.