Jumatano, 12 Oktoba 2016

AWAMU TATU za UKRISTO 
1 Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. 2Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. 3Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. 4Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno” (Matendo ya Mitume 8:1-4).
 
Kuna awamu tatu muhimu za ukristo ambazo ukiwa dunuani imekupasa kuzipitia na kutoa hesabu yake. Hatua hizi ni: kuzaliwa, kukua na kuzaa.
 
i.                    KUZALIWA
Ukristo unaanza na kuzaliwa kwa mara ya pili, kwa kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Kwa tafsiri nyingine, hii inaitwa “kuzaliwa kwa maji na kwa Roho” (Yohana 3:1-6). Hili huwa zoezi rahisi tu kama ukiamua leo, “Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu” (Warumi 10:10).
 
ii.                 KUKUA
Mtoto azaliwapo, hunyeshwa maziwa safi (yasiyoghoshiwa/yasiyotiwa maji) ili aweze kukua vizuri. “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpatekuukulia wokovu” (1 Petro 2:2). Hii ni hatua ya muhimu sana ya Mkristo ya KUTAMANI kujifunza neno la Mungu ili aweze kukua.
 
Kiwango tofauti cha KUTAMANI maziwa hupelekea watoto wa kiroho kukua kwa KASI tofauti. Ndio maana ndani ya kanisa utakuta watu wawili, mmoja anamiaka kumi kanisani lakini bado analishwa maziwa tu wala hajakua popote. Mwingine ana mwaka mmoja lakini ameshakomaa kiasi cha kuanza kuzaa! Hii yote ni UAMUZI wa mtoto husika, je! Unatamaini MAZIWA?
 
iii.               KUZAA
Kazi ya kondoo ni KUZAA kondoo wengine. Kazi ya mchungaji ni kulisha kondoo ili wakue, tena kwa kusudi maalumu. Kondoo asipozaa huyo huondolewa kundini mapema kwa maana hana faida kwa mchungaji, tena yamkini, huharibu na kondoo wengine.
 
Angalia tena kwa namna hii, kama BWANA Yesu ni mzabibu, na sisi ni matawi; maana yake tuko kwake tayari, yaani tumevuka hatua ya kuzaliwa na tunaendelea kukua, lakini kuna hatua ya kuzaa matunda inakuja hapo. Akiona tawi LISILOZAA, Yeye hulikata! Na lile lizaalo hulisafisha ili liweze kuzaa zaidi (Yohana 15:1, 2). Lengo la kubaki kwenye mzabibu ni kuzaa!
 
Ukiangalia Matendo ya Mitume 8:1-4, utaona jinsi ambavyo kanisa liliongezeka kwa ‘kondoo kuzaa kondoo’ kwa sababu baada ya kufanyika WANAFUNZI wa Yesu (wakristo), chini ya mitume, ilibidi watawanywe kwa nguvu ili wakazae huko waendako. Mitume (wachungaji) wakabaki Yerusalemu, kondoo (waumini) wakaenda kuhubiri injili na kuzaa matunda (waumini wengine) huko walikokwenda.
 
Ni jambo lililozoeleka kwa nyakati hizi kwamba kazi ya kuzaa kondoo ni ya mchungaji (viongozi wetu wa kiroho), kisha kuwatunza na kuhangaika tena kuandaa mikutano na seminia za kiroho ili kuzaa tena na kukuza wachanga. Wakrito (kondoo) wamekaa tu kanisani wanaingia na kutoka jumapili kwa jumapili; hawazai kitu! Hii sio sawa.
 
Kumbuka, “shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni” (Mathayo 3:10). Bwana akikutazama anakuombea kwa BABA kwamba upewe mwaka huu tena kama utazaa au la, na anakuwekea mbolea (unapata mafundisho mbalimbali na huduma zingine za kiroho), ili uzae; lakini usipozaa utakatwa tu kwa maana unaiharibu nchi. Tena sio kuzaa tu, unatakiwa kuzaa matunda MAZURI.
 
Angalia jambo hili, mitume walizaa wakristo wengi kwa KUSHUHUDIA habari za Yesu. Walijiita mashahidi. Yaani, WALISEMA yale waliyoona na kusikia kwa Bwana, hayo wanawaambia na wengine ili waamini (Matendo 22:15). Je! Wewe umewashuhudia wangapi?
 
Watu wengi wamejifariji kwamba kutoa SADAKA inatosha. Angalia, kutoa sadaka ni muhimu, lakini je! Wewe ni SHAHIDI wa BWANA? Kama wewe ni kondoo, ni vyema, ila swala ni KUZAA sio kutoa sufi (sadaka) tu, kuzaa ni LAZIMA!
 
Kila mtu anajua kwamba mti unafaida nyingi, kwa mfano: kuni, mbao, kivuli, nk. Lakini mwenye shamba anataka MATUNDA kwanza! Tunajua unavipawa vingi na unatoa sadaka nyingi kanisani kwako, je! Umezaa kondoo? Hili ni swali la kujiuliza na ni changamoto kwa kila mtu. Kumbuka, matunda ni ya kila msimu na yanatakiwa yawe mazuri na ya mengi. Ndio maana tawi lizaalo husafiswa ili lizae ZAIDI. Bwana anataka matunda zaidi; yaani kuongezeka katika kuzaa mwaka hadi mwaka.
 
Jitathmini umri wako wa kiroho. Kila siku unalishwa tu pale kanisani kwako. Je! Hukui tu? Utazaa lini? Je! Unajua una MUDA ambao ukifika ni LAZIMA uzae? Ndio maana ule mti ulipewa MUDA wa kuzaa kabla ya kukatwa. Jitahidi kuweka jambo hili kwenye maombi na matendo kwa maana hukuitwa kupiga pambio, kusikiliza neno na kuandika notsi tu pale kanisani kwako; leta matunda yako kwa mamana UNADAIWA. Au unasubiri ulazimishwa kwa adha kama lile kanisa la mwanzo?
 
Frank P. SethKAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Chapisha Maoni