Jumatatu, 25 Mei 2015

SAUTI ya NDANI


 
Kuasi kwake yule mwovu hunena moyoni mwake, Hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake. Kwa maana hujipendekeza machoni pake Kuwa upotovu wake hautaonekana na kuchukiwa. Maneno ya kinywa chake ni uovu na hila, Ameacha kuwa na akili na kutenda mema. Huwaza maovu kitandani pake, Hujiweka katika njia mbaya; ubaya hauchukii” (Zab 36:1-4).
 
Mara nyingi tumesikia watu wakisema habari ya “sauti ya ndani”, wengine wanapenda kusema “amani ya Kristo”, nk. Je! umewahi kujiuliza nini maana na sauti ya ndani? Je! Umewahi kujiuliza ni nani anayeongea ndani yako? Umewahi KUJITATHMINI kwa sauti zizungumzazo ndani yako?
 
Bila shaka watu wengi wanapata shida ya KUPAMBANUA baina ya sauti na sauti, hasa sauti za ndani. Yamkini hata manabii wakubwa na wazee wamepata mtihani huu pia ndio maana nabii Samweli, akiwa mzee, alitaka kumpaka Eliabu mafuta badala ya Daudi, huku sauti ndani yake ikisema “Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake” (1 Sam 16:6) hadi Bwana alipomkemea na kumwambia “Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo. ” (1 Sam 16:7)
 
Lengo la somo hili ni kutaka kujifunza jinsi ya KUJITATHMINI mwenyewe kwa kutumia SAUTI za NDANI tuzisikiazo. Bila shaka mawazo na matafakuri ya mwanadamu katika moyo/nafsi yake huja kama SAUTI ya NDANI. Je! Unajua uwazavyo ni sauti kamili mbele za BWANA? Na je! Unajua UASI hutambulikana MOYONI kabla ya kuwa kitendo au neno? Kwa maana BWANA hutazama moyo, wengi wetu hatutaweza KUJUA aliye mwema kwa matendo yake kwa maana matendo sio bora kuliko HALI ya moyo wa mtu.
 
Nimejifunza njia za Daudi kwa sehemu nikaona NGUVU zake zilikuwa katika MOYO safi. Mara nyingi BWANA alipotazama, Aliona jambo jema na hata alipomlinganisha na watu wengine, BWANA alisema “sawa, wamefanya vyema, ila si kama Daudi baba yao”!  Bila shaka kila mmoja alitenda matendo yake tofauti na mwingine, kwa hiyo kipimo hakikuwa katika matendo yao ila MIOYO yao.
 
Sasa angalia Zaburi ya 36. Daudi anasema “Kuasi kwake yule mwovu hunena moyoni mwake… hujipendekeza machoni pake Kuwa upotovu wake hautaonekana… Huwaza maovu kitandani pake”  na  ubaya hauchukii. Ukitaka kujitathmini moyo wako, jiulize mwenyewe, UNAWAZA nini? Yaani,  sauti gani unazisikia ndani yako? Na kama kuna TAMAA, au mawazo MABAYA, jiulize tena, je! Unachukia ubaya (uovu)?
 
Kumbuka siku zote, hatusemi tunampenda Mungu ila kwa KUCHUKIA uovu. Kama kuna uovu unauwaza moyoni na huuchukii basi jua kwamba Mungu aonacho ndani yako ni “kumchukia Mungu” bila kujali sana usemacho au utendacho kwa KUJIPENDEKEZA (Zab 36:2) ili uonekane mwema machoni pa watu.
 
Pamoja na wema wote wa Daudi, uchamungu wake na unyoofu wa moyo, hakuacha kuomba “Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee BWANA, Mwamba wangu, na mwokozi wangu” (Zab 19:4).
 
Natazama Yuko malangoni na ujira mkononi kumlipa kila mtu sawa na matendo yake.
 
BWANA anakuja.
 
Frank Philip Seth
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Chapisha Maoni