“Basi,
iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa
kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya
dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema,
na kupata neema ya kutusaidia wakati
wa mahitaji” (Waebrania
4:14-16).
Katika mfululizo wa somo hili la
kuushinda ulimwengu, tumeweza kuona kanuni ya kuushinda ulimwengu, ambapo kuna
mambo matatu (kuwa ndani ya Kristo, kuwa mtendaji wa Neno, na Kujilinda). Pamoja na mambo hayo, pia
tumeona baadhi ya tabia za washindi ambazo ni (unyenyekevu na kumtegemea
Mungu).
Katika somo hili, kuna mambo ya kujiuliza,
Je! Katika ulimwengu tunashinda nini? Kuna mambo matano ya kuangalia hapa,
kwenye Waebrania 4:14-16 kama ifuatavyo: mambo yetu ya udhaifu, majaribu,
wakati
wa mahitaji, na kutimiza wito wetu (yaani kwa
mfano, Bwana Yesu alifanikiwa kutimiza wito wake kama kuhani mkuu na mpatanishi
kati ya Mungu na mwanadamu).
Ukiyatazama mambo hayo matano, na
kuyagawa katika mambo mawili makubwa, unaweza kusema kushinda dhambi na
kutimiza
wito wetu tulioitiwa. Shetani akishindwa kukuua (kwa maana yeye
alikuwa muuji tangu mwanzo, na kazi yake ni kuiba, kuchinja na kuharibu), basi
atakushawishi utende dhambi kwa kuitumia tamaa yako mwenyewe (mtu hujaribiwa na
tamaa yake mwenyewe), na Ibilisi akishindwa hapo, basi atakupoteza kwenye
malengo yako ili ushindwe kufanya mambo ya muhimu katika wito wako. Kama kuna
janga kubwa ni kulima mashamba ya
watu wakati lako limejaa nyasi; hivi ndivyo inavyokuwa kwa watu wengi ambao kwa
kweli ni wachamungu sana, ila hawajui nafasi zao katika mwili wa Kristo, bali
wao hufanya kilicho mbele yao au chenye maslahi ya dhahiri, kumbe! Hatukuitwa
kufanya kitu chochote ila KILE Mungu alichotuitia kufanya. Huko nako ni
kushindwa sana, yaani kushindwa kufanya mapenzi ya Mungu kwa wakati wake, hata
kama hatutendi dhambi.
BWANA alijaribiwa katika mambo YOTE
kama ilivyo sisi leo ila hakutenda dhambi (Waebrania 4:14-16) na kwa sababu hii
basi, anaweza kutusaidia kwa habari ya “mambo
yetu ya udhaifu” ambayo mengine ni magumu hata mchungaji wako akiyajua
ataishia kukutenga tu. BWANA anaweza, ndio maana maandiko yamesema TUMTWIKE
Yeye fadhaha zetu (1 Petro 5:7). Begani mwa Yesu kuna nafasi ya kutosha kubeba,
sio shida zako tu ila na kukubeba wewe mwenyewe, kwa maana Yeye ni mchungaji na
sisi ni kondoo; Mchungaji wa kondoo haoni shida kubeba kondoo begani mwake na
kwenda kumtibu huko mbele. Kumbuka siku zote, ni wajibu wako KUJIWEKA mbali, au
kujiepusha na DHAMBI IKUZINGAYO UPESI (Waebrania 12:1), na hii inatofautiana
kati ya mtu na mtu, “ukijua mambo yako ya
udhaifu”, imekupasa kuchukua hatua, japo kuna rehema na neema, ikibidi, kukimbia hata kwa jinsi ya mwili. Ndio
maana BWANA alisema “jicho lako
likikukosesha, aheri uling’oe na kulitupa” (Marko 9:47), hii inaonesha
NAFASI yako katika USHINDI wako, na ndio maana ukisoma kitabu cha Ufunuo wa
Yohana utaona majina ya watakaourithi Ufalme wa Mbinguni wanaitwa “washindi”, na huu ushindi waliupata
DUNIANI yaani huku kwenye dhiki nyingi na mahitaji ya kila namna, ila
walishinda.
Nafikiri imezoeleka sana kusikia watu
wakisema “akipata shida, atarudi”, “akibwanwa, atalia”, “anajifanya mjanja kwa
sababu anavyo, akiishiwa nitampata tu”, nk. Kama kuna mahali Ibilisi ameweka
“nyavu” zake ni kwenye mahitaji yako. Anajua utakuja tu. Hii ni kanuni ya
wavuvi wengi. Wavuvi hawakimbizi samaki, ila wanaweka “chambo”; samaki mwenye
njaa (mhitaji) akija na njaa zake anakuwa mawindo mepesi! Ndio maana imekupasa
kujua mitego hii, ukiona MAHITAJI yako (matumizi ya kawaida, cheo, pesa,
chakula, kihisia, nk.) yanakufikisha mahali pa kutenda dhambi, jua hilo sio
hitaji tena ila ni JARIBU! Jipange vyema, ukishinda utaitwa “mshindi”; lakini
ukipata mahitaji yako na kuanguka,
haikufai kitu hata kama ungepata ulimwengu wote kwa maana hapo umepoteza nafsi
yako tayari.
Kumbuka siku zote, kuna rehema na
neema, sawa, ila imekupasa kuchukua hatua za kukikariba Kiti cha neema, kwa ujasiri,
ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia
wakati wa mahitaji (Waebrania 4:16). Kweli Yesu anaweza
kubeba mizigo yako, ila haji kuichukua ila wewe ndio “unamtwika” (1 Petro 5:7). Ukisubiri hapo chini, utaangamia kwa
kukosa maarifa. Mungu anataka kuonekana kwako na kukuinua, ila imekupasa “KUMTAFUTA kwa BIDII” (Mithali 8:17;
Yeremia 29:12-14) japo hayuko mbali nawe, ndipo utamwona!
Frank Philip.
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775
AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni