Jumatano, 5 Machi 2014

Muziki wa Injili Tanzania Wafunika Muziki wa Bongo Fleva Katika Soko


Kwa Tanzania na Afrika Mashariki huwezi kuwataja waimbaji wa nyimbo za Injili wanaotesa bila kuyataja baadhi ya majina kutokana na mvuto na ubora wa kazi zao sokoni.
Miongoni mwao ni Rose Mhando, Bahati Bukuku, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Christina Shusho, Siana Ulomi, Martha Mwaipaja, Jane Miso, Jennifer Mgendi na chipukizi, Edison Mwasabwite. 

Kwa mvuto wa kazi zao, kila duka linalouza kazi za muziki wa Injili ni vigumu kupita saa mbili kabla mmoja wao hajauza kazi yake. 

Wakati hali ikiwa hivyo kwa muziki wa Injili, baadhi ya wasanii wa Bongo Fleva, taarabu na muziki wa dansi, hali ni tofauti kwani soko kwa upande huo limekuwa gumu. Nyimbo za Injili zinaonekana kuanza kuufunika muziki mwingine kiasi cha kupigwa katika kumbi mbalimbali za starehe kwa hoja kuwa muziki wake unachezeka, una mvuto, hivyo kupendwa na wengi.

Rose Muhando
Huyu ndiye kiboko yao, wanamuziki wa Bongo Fleva wanamfahamu kwa jinsi anavyowapiga bao katika uuzaji wa kazi zake, si tu katika CD na video, Rose pia ni kinara wa mauzo katika miito ya simu. Diamond ambaye anasifika kwa kuuza miito ya simu, akikutana na Rose anakaa chini kwani mapema mwaka huu alimwacha mbali kwa kuingiza sh milioni 29 ndani ya miezi mitatu, huku Diamond akiingiza sh milioni 21. Albamu zake za ‘Mteule Uwe Macho’, ‘Kitimutimu’, ‘Jipange Sawasawa’ na ‘Utamu wa Yesu’ bado zinaendelea kufanya vizuri pamoja na kuwa wasanii wengine wanaingiza albamu mpya kila kukicha, lakini pia yupo njiani kuachia Kung’uta Yesu hivi karibuni. 

Bahati Bukuku
Huyu anatajwa kushikilia nafasi ya pili ya mauzo ya CD na video katika maduka mbalimbali ya kazi za sanaa. Pamoja na kutotoa kazi mpya mara kwa mara, albamu yake moja ilimfanya kuwa mwimbaji namba mbili katika mauzo na matamasha nchini. Katika tamasha lolote la Injili, haliwezi kukamilika bila kupigwa nyimbo zake ama kualikwa, albamu zake za ‘Nyakati za Mwisho’, ‘Nimesamehewa Dhambi’, na mpya aliyoizindua Septemba, 2013 iitwayo ‘Dunia Haina huruma’ zimemfanya kuendelea kuwika katika soko la muziki huo. Bukuku ni mwanamuziki mwenye mafanikio mengi ambapo kwa sasa amejikita pia katika ujasiriamali, maisha yake asilimia 70 yapo katika kulima na kuwekeza. Mwimbaji huyo anamiliki nyumba nne alizojenga mwenyewe, mbili zikiwa Tabata Migombani, moja Bunju na nyingine Mbezi Beach. Pia anamiliki mashamba manne huko Kitunda, Bunju, Kibaha na Mbeya, mashamba hayo yana takriban ekari mbili hadi tano. Aidha, ana makarashi mawili ya kusaga dhahabu mkoani Geita na anamalizia kujenga hoteli yenye vyumba 38 mkoani Geita, Hoteli hii itaitwa ‘Double B Hotel’.


Upendo Kilahiro
Mwanadada huyu licha ya kutokuwa na albamu kwa sasa, bado ameendelea kutamba katika muziki wa Injili kutokana na sauti yake kuwa tamu na nyororo. Kwa Kilahiro, muziki wa Injili unamlipa kwani ameweza kuanzisha chuo cha ushonaji kiitwacho, New Day Africa Foundation, ambacho wanafunzi wake wanasoma bure kwa muda wanaochukua ujuzi chuoni hapo. Kilahiro anayetamba na nyimbo za ‘Unajibu Maombi’ na ‘Usinipite’, ni msanii namba tatu kwa mauzo ya nyimbo za Injili hapa nchini. Sifa nyingine ya mwanadada huyu ni kwamba, akiwa katika harakati zake za uimbaji, watu wengi hasa raia wa Afrika Kusini akiwemo mwanamama Rebeka Malope, aliwahi kumuomba abadili uraia wa Tanzania na kuchukua uraia wa nchi hiyo ili aweze kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi akiwa nchini humo, lakini Upendo alikataa. Kutokana na msimamo wake huo, Malope alimuomba Upendo kuwa msemaji wake katika ukanda wa Afrika Mashariki, kazi anayoifanya mpaka sasa.

Upendo Nkone
Ana albamu za ‘Mungu Baba’, ‘Hapa Nilipo’, ‘Zipo Faida’ na mpya aliyoitoa mwaka jana iitwayo ‘Nimebaki na Yesu’, zinafanya vizuri huku albamu zote zikiendelea kununuliwa kwa wingi. Kila anapoachia wimbo mpya, huendelea kuzifanya zile za zamani ziwe nzuri zaidi. Mbali ya kuuza kazi zake, pia ni mwanamuziki anayeongoza kwa kufanya matamasha ndani na nje ya Bongo. Mara kwa mara hufanya ziara nchini Kenya ambako anakubalika na kuheshimika, lakini pia ni fundi wa kushona nguo, ambapo anamiliki ofisi aliyoajiri watu kwa kazi hiyo.
Christina Shusho
Huyu anazo sababu zaidi ya 100 za kuwa mwanamuziki anayeuza katika muziki wa Injili. Sababu kubwa ya kwanza ikitajwa kuwa ni sura yake inapokaa kwenye ‘kava’ inampa mteja hamu ya kutoa pesa yake kununua CD. Sababu ya pili ni sauti yake na namna anavyotengeneza video zake, tungo zake zinazogusa maisha ya kawaida na kiroho zimekuwa kivutio kikubwa. Mwimbaji huyo anamiliki kipindi cha runinga, lakini Shusho pia kwa mwaka jana alishinda tuzo ya mwimbaji wa mwaka 2013 kwa nchi za Afrika Mashariki katika tuzo za Africa Gospel Music Awards.

Masanja Mkandamizaji
Anafahamika kwa jina la ‘Masanja Mkandamizaji’ huku jina lake halisi likiwa ni Emmanuel Mgaya, yeye ameweza kushika kasi baada ya kuokoka na kujiita mchungaji mtarajiwa. Masanja Mkandamizaji anatamba na albamu yake ya ‘Hakuna Jipya’, ambayo ndani yake kuna mfumo wa uchekeshaji. CD za msanii huyo zimefanya vizuri sana sokoni.

Waliochipukia
Martha Mwaipaja na Siana Olomi nao wanaingia kwenye kundi hilo, lakini wanapishana kidogo kutokana na sababu mbalimbali zilizotolewa na wafanyabiashara wa kazi hizi. Waimbaji hao ni kama wanachipukia kwenye soko la kazi hizi, lakini wamekuwa wakichuana na wakongwe kina Flora Mbasha na Jennifer Mgendi, ambao wamekuwa katika muziki huo kwa muda mrefu.
Edson Mwasabwite
Anaingia akiwa mpya kabisa tena chipukizi kwa kupanda juu baada ya albamu yake ya ‘Ni kwa Neema tu na rehema’ ikiendelea kuwabamba mashabiki wa nyimbo za Injili. Albamu ya Mwasabwite imefanya vizuri sokoni na itaendelea kufanya vizuri kwa mwaka huu kutokana na wimbo wake uliobeba albamu.

Waliochemsha
Wafanyabiashara wa kazi hizi wanasema, Jennifer Mgendi na Flora Mbasha waliwahi kuwa vinara wa mauzo, lakini walipoanza kujichanganya na biashara nyingine, iliwapunguzia mashabiki ambao walianza kununua kazi za waimbaji wengine.
Flora Mbasha
Japo mwimbaji huyu amefanya matamasha ya kimataifa nchini Marekani na kwingineko pamoja na kumiliki studio, likichomuangusha ni kujihusisha na kampeni mbalimbali zikiwamo za vyama vya siasa.

Jennifer Mgendi
Msanii huyu kujiingiza katika uigizaji wa filamu, zinatajwa kuwa ni sababu zilizomrudisha nyuma.

Boni Mwaitege
Huyu amepotea katika soko baada ya kukaa kimya tangu alipotoa albamu ya ‘Mama ni Mama.’ Ukimya wake unaelezwa kuwa umesasabisha hata uuzaji wa nyimbo zake kuwa doro.

kwa hisani ya papa sebene

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni: