Jumatano, 2 Januari 2013

MAASKOFU WASEMA AMANI KWANZA MWAKA 2013

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo


ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema Watanzania wanapaswa kutanguliza ubinadamu zaidi ya imani za kidini ili kudumisha amani iliyojengeka nchini.

Kardinali Pengo alisema hayo usiku wa kuamkia jana alipokuwa akitoa salamu za Mwaka Mpya kwa Watanzania wakati wa Misa ya Mkesha kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph Dar es Salaam.

Alisema amani ndicho kitu pekee kinachopaswa kudumishwa miongoni mwa watu kwa kuishi pamoja kama binadamu na kuweka kando imani za kidini.
Alitaka Watanzania wanapokumbuka matukio yaliyotokea mwaka jana, waangalie mahali walikokosea ili kuepusha kujirudia mwaka huu kutokana na ukweli kuwa mwaka jana baadhi ya matukio yalihatarisha amani.

Huku akitolea mfano matukio ya uchomaji moto makanisa, vurugu za kidini na kupigwa risasi kwa Padri wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Ambrose Mkenda alisema yaliashiria kutoweka kwa amani aliyosema kimsingi haipaswi kuchezewa.

“Tunapoingia mwaka wa 2013, bila kujali imani zetu, tunapaswa kudumisha amani kwa kutanguliza ubinadamu kwa kuwa suala hilo ndilo pekee linalompendeza Mungu, na wala haiwezi kufananishwa na kitu chochote,” alisema Askofu Pengo.

Amani inachezewa Katika hatua nyingine, Padri wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Bikira Maria Parokia ya Mkwawa Iringa, Oscar Mchuchura, amesema amani ambayo Watanzania wanaichezea mataifa mengine yanaililia.

Akitoa salamu za Mwaka Mpya katika Kanisa hilo jana, Mchuchura alisema amani ya Taifa imeingiliwa na nyufa na ipo mbioni kubomoka kutokana na kutawaliwa na tamaa za mali, ardhi na madini.
“Hata chokochoko za kugombea mpaka kati ya Tanzania na Malawi zinatokana na kuwapo kwa mali, inasemekana ndani ya eneo linalogombaniwa kuna mafuta, ndiyo maana unaona wenzetu wameanza kuleta vurugu,” alisema Padri Mchuchura.

Alisema amani iliyopo imekuwa ikipotezwa na baadhi ya watu kwa sababu ya tamaa za vyeo, ubinafsi na kusababisha kutafuta njia zinazotawaliwa na chuki na fitna.

“Tuna machungu na majonzi tunapouanza mwaka 2013, kutokana na matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea, inatupasa tuangalie tuliuaga vipi mwaka 2012 huku tukiwa na dira nzuri mwaka huu,” alisema Padri Mchuchura.

Malasusa na malengo Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa alitaka Wakristo kujifunza kusahau yaliyopita na kuwa na malengo kwa kufanya uamuzi wakati wanaanza mwaka huu ili wafanikiwe kimaendeleo katika maisha.

Dk Malasusa alisema hayo wakati akitoa salamu za Mwaka Mpya katika Ibada iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Azania Front, ambapo neno kuu lilikuwa ni upendo. Alitaka Wakristo kutofikiri wamefika walipo bali wajue bado wana safari ndefu mbele.

“Kila Mkristo ni lazima awe na mpango mkakati wa maisha yake ... Wakristo wengi hatumjui Mungu, hatumwogopi Mungu na hatuna malengo, tunatakiwa kutambua kusudi la Mungu ili tujipange tufanikiwe,” alisema.

Alisema watu wengi wanashindwa kupata maendeleo kutokana na kukumbuka yaliyopita na kutaka Wakristo kujifunza kusahau yaliyopita na kuangalia ya mbele.

“Moja ya matatizo tuliyonayo ni kwamba hatujui tunataka kwenda wapi, ni lazima tuwe na mpango mkakati kwa mwaka huu kwa kuwa Mungu ametuacha ili tutengeneze maisha yetu,” alisema.
Alisema mwaka huu lazima watu wabadilike na kuzaliwa upya kwa kurejea katika misingi halisi ili kila mtu atawale maisha na si maisha yamtawale.

“Tusisubiri ndoto, tutoke na tutende, mwaka huu pia uwe mwaka wa kila mtu kuwa na kiu ya Neno la Mungu na tuwaombee wasio na kiu wakose amani. Pia tuwaombee sana viongozi wetu kwa kuwa tukiomba tutapata moyo wa kuwajali wenzetu,” alisema Dk Malasusa.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni