Alhamisi, 30 Agosti 2012

ASKOFU WA MPANDA AFARIKI NI PASCHAL KIKOTI

ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, Askofu Paschal Kikoti (55), amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.

Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda, Padre Patrick Kasomo amewaeleza waumini katika kanisa kuu la Jimbo la Mpanda kuwa, Askofu Kikoti alipatwa na shinikizo la damu Jumapili asubuhi Agosti 27,2012 akakutwa hana fahamu.

Aliwaeleza waumini hao kuwa Askofu Kikoti alipatwa na ugonjwa huo saa moja asubuhi moja asubuhi wakati akioga, akaanguka akiwa bafuni akapoteza fahamu.

Kwa mujibu wa Padre Kasomo, mapadre na masista walibaini kuwepo kwa tatizo hilo walipotoka kwenye ibada ya misa ya kwanza saa mbili na nusu asubuhi.

Amesema, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lilitafuta ndege siku hiyo hiyo,ikaenda kumchukua Askofu Kikoti jimboni Mpanda na kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza.

Padre Kasomo amesema, Askofu Kikoti aliaga dunia jana saa 2:30 usiku. Baada Padre Kasomo kutoa taarifa hiyo waumini wa kanisa hilo walianza kulia na baadhi yao walipoteza fahamu.

Marehemu Askofu Paschal Kikoti alizaliwa Mkoani Iringa katika Parokia ya Nyabula mwaka 1957 , alipewa daraja la upadre tarehe 29/6/1988 mkoani humo.

Novemba 4, 2000 alisimikwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo la Kanisa Katoliki la Mpanda.
Hii ilikuwa mara ya pili kwa askofu huyo kuanguka kwa ugonjwa wa moyo.

Mara ya kwanza ilimkuta katika kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Immaculata wakati akisimikwa kuwa askofu wa Kanisa Katoliki la Mpanda.

 Mwili wa Askofu Kikoti unatarajiwa kuzikwa Jumamosi wiki hii ndani ya Kanisa Kuu la Mpanda.

RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI

RAIS Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kutokana na kifo cha Askofu wa Kwanza wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Askofu William Kikoti.
 
Kifo cha Askofu Kikoti kilitokea usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza alikokuwa amelazwa kwa matibabu kutokana na ugonjwa wa shinikizo la damu.
 
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Baba Askofu William Pascal Kikoti wa Jimbo Katoliki la Mpanda akiwa bado na umri mdogo wa miaka 55 wakati ndiyo kwanza utumishi wake ulikuwa ukihitajika zaidi,” alisema Rais Kikwete katika salamu zake na kuongeza:
 
“Ni dhahiri kwamba kifo cha Baba Askofu Kikoti kimeacha pengo kubwa la kiuongozi siyo tu kwa Kanisa Katoliki hapa nchini, bali pia Jumuiya ya Waumini wa Kanisa hilo kote duniani”.
 
Rais Kikwete alisema anatambua jitihada kubwa za Askofu Kikoti enzi za uhai wake katika kuwatumikia waumini wa Kanisa lake, na hususan wa Jimbo Katoliki la Mpanda, tangu alipopata Daraja la Upadri mwaka 1988, kuteuliwa kwake kuwa Askofu wa Kwanza wa Jimbo Katoliki la Mpanda mwaka 2000, na hatimaye alipowekwa Wakfu na Kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo hilo mwaka 2001.
 
“Kutokana na msiba huo mkubwa, ninakutumia wewe Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania salamu zangu za rambirambi, na kupitia kwako kwa Kanisa Katoliki na kwa waumini wote wa kanisa hilo hapa nchini hususan wa Jimbo Katoliki la Mpanda, kwa kumpoteza mmoja wa viongozi muhimu na wa ngazi ya juu wa kiroho, marehemu Baba Askofu William Pascal Kikoti”, alisema Rais Kikwete.
 
Alisema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipumzishe mahala pema peponi Roho ya Marehemu. Aliwahakikishia wote waliofikwa na msiba huo kuwa yuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo kwa kutambua kuwa yote ni mapenzi yake Mola.
 
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela
Chapisha Maoni