Jumatano, 18 Julai 2012

WACHUNGAJI WALIOJIHUSISHA NA DECI WAKUTWA NA KESI YA KUJIBU

WAKURUGENZI watano wa Taasisi ya Kusimamia na Kuendesha Upatu (Deci), wanaokabiliwa na kesi ya kuendesha shughuli za upatu bila kibali wamepatikana na kesi ya kujibu dhidi ya mashtaka yanayowakabili.

Wakurugenzi hao ambao ni wachungaji wa makanisa tofauti ya Pentecoste, walipatikana na kesi ya kujibu jana wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilipotoa uamuzi, baada ya kusikiliza mashahidi wa upande wa mashtaka.

Licha ya kudaiwa kuendesha shughuli za upatu bila kibali, wanakabiliwa na shtaka la kukusanya fedha kutoka kwa wananchi. Washtakiwa hao ni Jackson Mtares, Dominic Kigendi, Samuel Mtares, Timotheo Ole Loitingye na Arbogast Francis.

“Ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka unatosheleza kuwafanya washtakiwa kuwa na kesi ya kujibu, ambao hawana namna nyingine zaidi ya kujitetea wao wenyewe dhidi ya mashtaka,” alisema Hakimu Stuart Sanga katika uamuzi wake.

Wakati wa usikilizaji kesi hiyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Prosper Mwangamila, uliwaita mahakamani mashahidi 16 na vielelezo kadhaa kuunga mkono ushahidi wao.
Baada ya uamuzi huo washtakiwa waliomba mahakama iwapatie muda wa kuwasiliana na mawakili wao kupanga jinsi watakavyojitetea na idadi ya mashahidi, ambao wanakusudia kuwaita kuwatetea.

Hakimu Sanga aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 20 itakapotajwa na kupangiwa tarehe ya washtakiwa kuanza kujitetea.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa katika tarehe tofauti mwaka 2007 na Machi 2009 katika Makao Makuu ya Deci, Mabibo Dar es Salaam walikusanya fedha kutoka kwa wananchi wakiwaahidi kuwa watapata faida ya riba kubwa, katika mpango huo waliouita kupanda na kuvuna.

Washtakiwa hao zaidi wanadaiwa kuwa katika tarehe hizohizo walikubali kupokea fedha kutoka kwa wananchi wakati wakijua kuwa, walikuwa wakitenda kinyume cha sheria kwa kuwa hawakuwa na leseni ya kuendesha shughuli hizo.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Mawazo yako ni muhimu sana tafadhali tumia lugha nzuri na tutairusha na wengine waisome.