Ijumaa, 1 Juni 2012

NYUMBA ZA MABONDENI KUANZA KUBOMOLEWA WATU HAMENI!


Kuna taarifa za kuanza  ubomoaji wa nyumba zaidi ya 2,000 zilizojengwa mabondeni kando ya Mto Msimbazi wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam. Lengo la uamuzi huo unaotarajiwa kutekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni wiki mbili zijazo, ni kuhakikisha wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wanahama, ili wasikumbwe tena na mafuriko.
Maeneo yaliyokuwa na mafuriko mwaka jana
Kulingana na maelezo ya Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Gaudence Nyamwihura, ubomoaji huo utaanza na nyumba 217 kati ya 2,000 zilizomo katika tathmini, kuanzia eneo la Magomeni, Kinondoni, Jangwani mpaka Daraja la Sarenda ambapo mto huo humwaga maji yake baharini. Uamuzi wa serikali ingawa umechelewa hadi kusababisha vifo vya watu 41 katika mafuriko ya Desemba mwaka jana, ni mzuri kwa kuwa umelenga kuhakikisha hakuna watu wanaoendelea kuishi mambondeni.

Pia, ni uamuzi utakaoibu maswali ambayo wananchi wamekuwa wakiuliza kutokana na kuona wenzao wakiendelea kuishi katika maeneo hatari ya mabondeni, wakati kuna amri ya serikali, ya kuwataka kuhama.Matarajio yetu na wananchi wote ni kuona maeneo yote yaliyotajwa kuwa ni hatari na wakazi wake kuhamishiwa Mabwepande, yanakuwa wazi baada ya tingatinga la Manispaa kupita na kusawazisha, baadaye kuweka uzio kuzia watu wapya kuhamia.
Kinyume chake, tumeendelea kuona watu katika maeneo hayo ya hatari, jambo ambalo limetushangaza na kuhoji bila majibu, hivi serikali inamaanisha inachokisema au kauli zake ni kutuliza umma wakati wa maafa?

Ukimya wa serikali wakati maisha yanaendelea mabondeni kama kawaida, umekuwa ukitushangaza kwa sababu tulishantangaziwa kuwa eneo la Mabwepande Wilaya ya Kinondoni limetengwa kwa ajili ya waliokuwa wakazi wa mambondeni, na kwamba wamekwishahamia.
Cha kushangaza hata huko Mabwepande walikopelekwa Januari mwaka huu matarajio yao hayakutimizwa. Mbali na kwamba hawajaruhusiwa kujenga nyumba za kudumu, kujengewa wala kukabidhiwa viwanja rasmi ili wajenge nyumba zao wenyewe, wananchi hao hawajui wanachostahili kufanyiwa.

Hali hiyo imewaweka wananchi hao katika sintofahamu ya muda mrefu. Wameendelea kuishi katika mahema ya msaada, baadhi yake yakianza kuchanika. Hawana faragha. Baridi yao, na mvua pia. Kibaya hawafahamu ni lini watapata nyumba za kudumu katika makazi hayo mapya.
Tunaishauri serikali, kama ilivyopima eneo hilo kwa haraka na kuweka miundimbinu ya umeme na maji, ifanye hivyo hivyo kuondoa utaratibu wa kirasimu wa ugawaji wa viwanja kwa waathirika hao, ili wananchi hao wapate nyumba za kudumu haraka iwezekanavyo.

Tunasema haya kwa kuzingatia malalamiko ya wakazi hao juu ya upendeleo katika utoaji wa fomu za kuomba viwanja hivyo, wakidai kuwa hata watu wengine ambao si waathirika wa mafuriko ya Desemba 2011 wamejipenyeza katika kundi hilo na kusababisha kero na hofu kubwa ya kukosa makazi waliyoahidiwa.
Kuchelewa kwa kuhamisha watu wa mabondeni kumezingirwa na mambo mengi ambayo serikali inatakiwa kuyaangalia, likiwamo suala la wakazi ambao wana vibali halali vya kusihi katika maeneo hayo hatari.Ni imani yetu kwamba umefika wakati wa serikali kuacha kuwafumbia macho watumishi wake wasiokuwa waaminifu, ambao walitoa vibali vya watu hao kuishi mabondeni kinyume na sheria.

Tunashauri zitungwe sheria kali zaidi kama zilizopo zimeshindwa kusaidia, ili kuepuka kila mara yanapotokea mafuriko wanakuwapo watu wa kuathirika na serikali inaendelea kuhangaika na uokoaji na kuwatafutia viwanja. Tukifika hatua hiyo, ndio utakuwa mwisho wa maagizo ya watu kuhama mabondeni.
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FACEBOOK Martin Malecela
follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni: