Jumapili, 20 Agosti 2017

KUSUDI lililo FICHIKA

5Na tazama, Sauli akaja akifuata ng’ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi” (1 Samweli 11:5).
  
Kila mtu amezaliwa na KUSUDI tayari, ila HATMA yako ni wajibu wako kuiFIKILIA kwa bidii zako, KAMA ukiweza KUVUMBUA kusudi lako na KULITIMIZA. Kwa lugha nyingine kusudi limeitwa WITO.
  
Kwa bahati mbaya, majina yetu, kwa watu wengi sana, hayataji KUSUDI ndani yao! Sijui kama unajua kwamba kila KUSUDI lina jina, na hilo jina atapewa AFANYAYE mambo katika kusudi hilo. Kwa mfano, kama wewe unaitwa Mary, na ni nabii, lakini hutabiri, jina lako litakuwa Mary, kwa sababu ulipewa utotoni. Utaitwa Mary hadi kufa kama hutavumbua KUSUDI lako na kulitenda.
  
Lakini, kuna jina ulipewa KABLA ya kuzaliwa, hilo jina LINATAJA kusudi lako. Kwahiyo, kama huyo Mary ataanza KUTABIRI, na watu WAKAKUBALI hiyo huduma yake ya unabii, jina lake litakuwa ‘nabii Mary’. Je! Wewe unaitwa nani?
 
Hebu angali hii,
 
Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa” (Yeremia 1:5).
Ukifuatilia habari za Yeremia, utagundua kwamba jina “Yeremia” alipewa baada ya kuzaliwa, lakini jina “nabii” alipewa kabla ya kuzaliwa. Jina Yeremia ni jina kama kila mtu alivyo na jina, ila jina “nabii” ni jina la KUSUDI la Mungu maishani mwake.
 
Kwenye maandiko utaona watu wachache sana walipewa majina yao ya ‘KAWAIDA’ kabla ya kuzaliwa. Ila ukifuatilia, utaona Mungu akisema KUSUDI la mtu bila jina la kawaida. Haijalishi kwamba ‘jila la kawaida’ ni Yakobo au Esau, Mungu alitaja KUSUDI la hao wawili wakiwa tumboni. Mungu hakusema wataitwa Yakobo na Esau, majina haya walipewa na wazazi wao! (Mwanzo 25:22-26)
  
Hata hivyo, bado sipuuzii UMUHIMU wa ‘kuchagua’ jina LIFAALO. Ndio maana baada ya miaka mingi, Yakobo alibakia na jina lake hadi alipopewa jina jingine na Mungu; akaitwa Israel. Angalia, Jina Israel lilikuja wakati Yakobo AMEFANYA jambo fulani katika lile KUSUDI lake. Angebweteka, angekufa akiitwa Yakobo! Sizungumzii majina, mimi nasema habari za KUSUDI.
 
Ukisoma 1 Samweli 11:5, utaona Sauli akiendelea na shughuli zake za kawaida, japo AMEPAKWA mafuta kuwa mfalme! KUSUDI la Sauli kupakwa mafuta ni kuwa MFALME na kisha kuwaokoa wana wa Israel na Wafilisti. Hadi kwenye sura ya 11, 1 Samweli 5, bado Sauli hakuitwa ‘jina’ mfalme kwa sababu bado alikuwa hajaSIMAMA kwenye KUSUDI hilo.
  
Sauli alipopakwa mafuta, alirudi nyumbani kwakwe na kuendelea na biashara zake za ng’ombe kama kawaida! Mpaka Nahashi, Mwamoni alipokuja kutaka kufanya kazi ya KUWAKOA Israel, ambayo ni kazi ya Sauli, kwa makubaliano ya wana wa Israel kung’olewa jicho la kuume (1 Samweli 11:1-3), ndipo Sauli akakurupuka na kuanza kufanya KUSUDI lake. 
  
Hebu fikiri kama Nahashi angefanya kimya kimya bila kudai jicho la mtu; Kisha akawaokoa Israel na Wafilisti, na wao wakamtumikia kama walivyoapa! Ndivyo ilivyo hata leo, wengi wetu tumejiapisha (saini mikataba) ya kuwatumikia watu ambao, kwa kweli siko KUSUDI letu liliko. Na, inetughariumu vibaya. Je! Kwa namna hiyo tutafikilia HATMA zetu?

Haya ni  mambo muhimu ya kuzingatia kuhusu kusudi ndani yako:
 
i.               Neno la Mungu
  
“Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri ya BWANA, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana BWANA angaliufanya ufalme wako kuwa imara juu ya Israeli milele. Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye BWANA amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile BWANA alilokuamuru”(1 SAM. 13:13-4).

Nimekutana na watu wengi sana ambao wanasema, “mimi sijui wito wangu”, “mimi sijui kusudi la Mungu maishani mwangu”, “mimi sijui Mungu anataka nifanye nini hasa”, nk.
 
Nikiwatazama hawa watu wote, sio kwamba hawafanyi kitu, wako busy na kazi zao, huduma, nk. Wengine wanafanya kazi chini ya watumishi wengine wa Mungu, nk. Kinachonishangaza, je! Hao watumishi wanaofanya nao kazi pia hawajui kwamba watu waliopo chini yao ndio WENYEWE au ni VISHOKA tu? Nitakwambia jambo, Mungu anaangalia ALIYEKO tayari, potelea mbali kama ni KISHOKA au ni mfanyakazi RASMI! Kazi itafanyika.
 
Nitakupa siri moja, kama watu wangesimama kwenye NAFASI zao vizuri, hakika kusingekuwa na KISHOKA! Ni sawa na mahali ambapo kila mtu ana USAFIRI binafsi, je! Mpiga debe atafanya nini? Bila shaka mahali kama hapo hapatakuwa na wapigadebe!
  
Ndivyo ilivyo hata kwenye ufalme wa Mungu. Walioalikwa (walioitwa) hawapo, wako busy na mambo mengine! Basi, watakusanywa waliopo kwenye njia kuu, waje badala yao (Mathayo 22:1-10). Na, wasipofanya liwapasalo, basi mawe yataamshwa kufanya kazi ipasayo kwenye nafasi zao!
 
8Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. 9Wala msijidhanie mnaweza kujiambia, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu, kwa maana nawaambia kuwa Mungu anaweza kumuinulia Abrahamu watoto kutoka katika mawe haya. 10Hata sasa shoka limekwisha kuwekwa tayari kwenye mizizi ya mti. Kila mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni” (Mathayo 3:8-10). Umewekwa duniani KUZAA matunda, tena matunda fulani mahusus, si alimradi tunda ni tunda tu! la sivyo, ni AHERI ukatwe!
  
Wakati Bwana anaangalia MAVUNO na kuona yameiva, alisema, “Mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watendakazi shambani mwake” (Luka 10:2). Inahitahika MAOMBI ili UWEZE kuingia shambani kufanya SEHEMU yako. Watu hawafanyi kwa sababu ni watendakazi, ila kwa sababu WAPO TAYARI na kuna NGUVU za Mungu za kuwaweka kwenye hilo kusudi. Usipoomba, ujue kwa hakika, utatumika KUSIKO KWAKO na utapata HASARA mwishowe, kwa sababu nani ATAKULIMIA shehemu yako wakati wewe unalima kwa wenzako?
  
Hatua za kukaa kwenye KUSUDI zinaanza na kukaa kwenye NENO pamoja na MAOMBI. Pasipo neno, hakuna imani; Pasipo imani, maombi hayana nguvu hata kama yapo!
  
Hebu soma habari za mti uliopandwa kandokando ya vijito vya maji, UZAAO matunda yake kwa MAJIRA yake, wala jani lake halinyauki, (Zaburi 1:1-6). Mti huu ni mfano wa mtu anayesoma NENO na kulitafakari USIKU na MCHANA! Atakaa MAHALI anapopaswa na ATAZAA sana, na “kila alitendalo litafanikiwa”! Hii inaanza na kusoma na kutafakari neno la Mungu.
  
Kadri UNAJAA neno, utagundua kuna mambo yanabadilika taratibu, NENO litakusafisha, pia na MACHO yako ya rohoni yataondoka tongotongo. Utaanza kuona mambo kwa MTAZAMO tofauti. Hilo neno litakumulikia NJIA ikupasayo kupita! (Zaburi 119:105); Utaanza KUGUNDUA kikupasacho kufanya, taratibu, hilo neno litazungumza na wewe wakati unalisoma. Utapata MWANGA wa kuona LIKUPASALO! Ule mwanga UTAIBUA kusudi lililoFICHIKA ndani yako.
  
Kwa mfano, angalia zile huduma tano, kuna namna ambavyo mwalimu akisoma neno ataona, na mwinjilisti ataona kwa namna nyingine, nabii, mchungaji, mtume, nk, wote wataona kwa namna WALIVYO, japo wamesoma kitu kile kile. Ndio maana mwalimu akisema neno lile lile, hata kama hajajitambulisha, utagundua huyu ni mwalimu, na mwinjilisti akisema, atatambulika tu. Hii ni tofauti ya kuona kulingana na WITO au KUSUDI ndani yako. Lakini pia neno hilo litawajenga MUSULI zao kwa namna tofauti ili waweze KUTIMIZA kusudi ndani yao; kila mmoja kama ALIVYOITWA.
  
Kwa hiyo, kadri unajifunza neno, na kusoma kwa bidii, lile neno litakuchonga wewe illi uzidi KUFANANA na kile kitu Mungu alichokitarajia kwako. Hata hivyo, inaanza na kuwa NDANI ya Yesu (kuwa tawi la mzabibu); Ndipo UKISOMA neno na kufanya kazi sawa na hilo neno UTASAFISHWA “ili” UZAE zaidi. Kuzaa maana yake ni KUTOA MATUNDA yaliyokusudiwa sawa na WITO wako.
  
Kwa bahati mbaya watu wanadhani kuzaa ni kuzaa tu! Ndio maana wale watu walimwendea Yesu wakisema “tulitoa pepo kwa Jina lako”, Naye akawaambia, “ondokeni kwangu ninyi mtendao maovu”. Unadhani ni kwanini? Angalia mfano wa mfalme Sauli, unadhani alizini, aliua, aliiba, nk.? Kosa lake ilikua KUTOA SADAKA ISIVYO SAHIHI! Yaani, hakufuata NENO LA MUNGU ili atende SAWA na WITO wake! Nabii Samweli akamwambia, umefanya upumbavu!
  
21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? 23 nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu” (Mathayo 7:21-23).
 
Sasa zingatia jambo hili, je! Unajua kazi zako (kusudi), nyakati, mahali pa kuishi, nk., Viliumbwa kabla HUJAZALIWA? Yaani uliwekewa MIPAKA tayari. Hebu linganisha vifungu hivi miwili, (Matendo ya Mitume 17:24-28) na (Yohana 15:1-5).
  
24 Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; 25 wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. 26 Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; 27 ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. 28 Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake” (Matendo ya Mitume 17:24-28).

Kisha angalia, “1 Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. 2 Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. 3Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. 4Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. 5 Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote” (Yohana 15:1-5). 
  
Kwenye Matendo ya Mitume wanazungumzia “wanadamu”,  kwenye Yohana wanazungumzia “tawi la mzabibu”. Wanadamu unaowaona kwenye Matendo ya Mitume, wameumbiwa majira na nyakati na mipaka ya makazi tayari. Majira na nyakati, maana yake ni vipindi mbalimbali ambavyo vinaendana na majukumu fulani mahusus. Kwa mfano, wakati wa mvua kuna kupanda; kuna shughuli zake hapo tofauti na wakati wa kiangazi.
  
Ukiangalia Yohana, utaona “tawi la mzabibu”. Inamaana kuna kazi mahusus ya kufanya, ambayo ni KUZAA zabibu sio machungwa! Kuna mahali hilo tawi lipo! A specific location kwenye mzabibu na halisogei hapo! Kazi yake ni kuzaa tu! Na, kazi ya Bwana ni kulisafisha kwa NENO ili lizae zaidi.
  
Sasa angalia jambo jingine,
 
Kwenye Mdo 17:18, tunasoma “Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu”, na BWANA anasema kwenye ,Yoh. 15:5 , “…akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote “.
  
Kuweza kufanya KUSUDI, huanza na KUKAA ndani ya Yesu, na kumsikiliza Yeye (neno la Mungu/biblia). Hakuna mtu atafanikiwa kufanya kusudi la Mungu bila mambo mwili kutokea: 1. Kuwa tawi la Mzabibu (kuokoka), na 2: Kutembea na Bwana [ndani yake tunaishi na tunakwenda (Mdo.17:8)], kwa maana PASIPO yeye HATUWEZI neno LOLOTE! (Yh. 15:5).
  
Kilicho mvuruga mfalme Sauli, ilikuwa ni kufanya HUDUMA pasipo kujua NENO la Mungu la wakati huo! Akafukuzwa kazi.

ii. Je! Unajua Vipawa Vyako?
  
Kwenye mfululizo wa somo hili, tumeona kwamba KUSUDI linaumbwa kabla hujazaliwa. Huji duniani halafu ndio Mungu atafute kazi ya kukupa, umekuja duniani kwa sababu kuna kazi yako maalumu iliyofichika katika ulimwengu wa roho. Hiyo kazi ndio inaitwa KUSUDI au WITO.
  
Sababu za KUFICHA kusudi ndani yako ni ili “umtafute Mungu, hata kwa kupapasa-papasa” na umwone kwakuwa hayuko mbali nawe (Matendo ya Mitume 17:28). Kwa hiyo Mungu amekuwekea tayari KUSUDI na MIPAKA ya makazi yako. Ukitaka kujua, jenga UHUSIANO mzuri Naye, kaa ndani Yake (Yohana 15:5) na tembea ndani Yake (Matendo ya Mitume 17:26), utajua hilo kusudi na wito wako.
 
Watu waliowahi kuniuliza swali kwamba, Je! Nitajuaje wito wangu? Wengi nimewauliza swali pia, Je! Unajua VIPAWA vyako?
Kwa bahati mbaya sana, wengi wa wanaouliza hili swali, hawana uhakika kwamba VIPAWA vyao hasa ni nini!
  
Kwa lugha nyingine, VIPAWA vimeitwa VIPAJI. Sasa uwe makini, sio kila UNACHOWEZA kufanya ni KIPAWA chako. Unaweza kupenda kufanya kitu katika FANI fulani, na ukaweza kweli, lakini sio KIPAWA/KIPAJI chako.
  
Kwa lugha nyingine, unaweza KUTAMANI kipawa na UKAJIENDELEZA kwa kusoma na kufanya KAZI kwa bidii na ukaweza! Sio kosa. Swali ni Je! Unafanya hivyo ili utimize KUSUDI la Mungu?
Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora” (1 Wakorintho 12:13).
  
Lakini, kuna watu wanajikuta WANAWEZA kufanya kitu fulani kwa namna TOFAUTI na wanafanya kwa WEPESI sana kitu hicho; Kwa sababu WAMEPEWA KUWEZA kukifanya. Kimo ndani yao! Hicho ni kipawa/kipaji.
 
Wengi hawajui kwamba hicho wafanyacho ni kipaji kwa sababu wakifanya, wanafanya kwa URAHISI hadi hawaoni kwamba ni kitu MAALUMU sana. Hawatoi jasho kufanya, hawajakitesekea sana! Basi thamani huwa chini sana kwa mwenye KIPAJI chake, ndio maana wengi hawavioni!
  
Ukiwauliza watu wengi wenye VIPAJI fulani vikubwa, watakwambia kwamba kuna MTU aliwaambia kwamba WANAWEZA jambo fulani, wakatiwa MOYO au wakaSAIDIWA kwa namna fulani. Walipoona THAMANI ya VIPAJI vyao, hawakuwa tena kama walivyokuwa! Kipaji kina mwinua yeye alichonacho na kumkutanisha na wakuu!
8 Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa” (Mithali 17:8).
 
Kumbuka, umepewa KIPAJI/KIPAWA kwa sababu ya KUSUDI fulani maalumu. Kipaji ni kama KITENDEA-KAZI cha kutimiza hilo KUSUDI uliloitiwa na Mungu. Je! Unajua VIPAJI vyako? Hapo ndipo KUSUDI lilikoJIFICHA.
  
Bado namtazama mfalme Sauli kujifunza habari za KUSUDI, japo nitatumia na mifano ya watu wengine.
  
Angalia VIPAWA vya Sauli kabla hajaitwa;
1 Basi, kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini, jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu.2 Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, kijana, tena mzuri; wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wote” (1 Samweli 9:1, 2).
 
Wakati wana wa Israeli wanafikiri kuwa na mfalme, ilikuwa ni vipindi vigumu kwa USALAMA wao na nchi yao. Kwenye mataifa mengine kulikuwa na wafalme. Moja ya kazi za wafalme ilikuwa KUPIGANA vita na KUTWAA nyara za vitu, watu na ardhi, kwa sababu za kiuchumi au za kiusalama.
  
Katika hali ya kukosa usalama, wana wa Israeli nao wakatamani wawe na mfalme wao kama mataifa walivyo na wafalme. Walitaka mtu atakayesimama katika nafasi ya juu ya uongozi, ambaye pia atawaoka na adui zao.
 
Basi Mungu akatafuta mtu ambaye ndani yake kuna KIPWA cha KUPIGANA vita. Alipoangalia familia mbalimbali, mtu mwenye SIFA kwa KAZI iliyopo mbele, akamwona mzee Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu. Alipotazama tena, akamwona kijana wake, Sauli!
 
Biblia haituonyeshi Sauli akijifunza vita, bila shaka alipata SHULE ya kupigana kwa baba yake, mzee Kishi. Kwahiyo, wakati Sauli anapakwa MAFUTA, alipewa kazi mbili moja kwa moja: kumiliki watu wa BWANA, na kuwaokoa na mikono ya adui zao! Mungu alijuaje kwamba Sauli anaweza? Aliangalia VIPAWA vyake ndani yake!
 
1 Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema, Je! BWANA hakukutia mafuta [uwe mkuu juu ya watu wake Israeli? Nawe utamiliki watu wa BWANA, na kuwaokoa na mikono ya adui zao; kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa BWANA amekutia mafuta] uwe mkuu juu ya urithi wake” (1 Samweli 10:1).
 
Angalia sifa za Daudi kabla hajapakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli.
 
18Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yu pamoja naye. 19Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo. 20Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli kwa mkono wa Daudi mwanawe. 21 Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa mtu wa kumchukulia silaha zake” (1 Samweli 16: 18-21).
 
Wakati Sauli anashindwa KUTIMIZA kusudi la Mungu kwa sababu ya kushindwa KUTII neno (1 SAM. 13:13-4), Mungu akaona mtu mwingine mwenye SIFA (VIPAWA) (1 Samweli 16: 18-21) kama vya Sauli, lakini MWELEKEVU wa moyo! Daudi, mwana wa Yese, (Zaburi 89:20,21).
 
Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye BWANA amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile BWANA alilokuamuru” (1 Samweli 13:14).
  
Unapoona UNALAUMIWA kwenye nafasi yako ya kazi kwa sababu ya UTENDAJI wako mbovu, halafu ukaona tangazo la nafasi ya kazi (vacancy) la kutafuta mtu mwenye sifa zako, wakati wewe upo kazini, jua wakati wa KUPUNGUZWA kazini umefika!  Sauli hakuweka hilo moyoni wakati nabii Samweli alipompa ‘barua ya’ ONYO! (1 Samweli 13:14).
  
Kwa wanaofuatilia maandiko, watakwambia kwamba tangu nabii Samweli asema kwamba Sauli hafai, kwenye 1 Samweli mlango wa 13; Daudi alipakwa mafuta baadae sana, kwenye 1 Samweli mlango wa 16. Hapo katikati na baada ya hapo, Sauli aliendelea na kazi zake za KUPIGANA na maadui wa Israeli na alishinda vita kama kawaida. Lakini, alikuwa AMESHAFUTWA kazi! Na nafasi yake katika ulimwengu wa roho alikuwepo Daudi tayari kama mfalme (1 Samweli 13:14). 
 
 Katika ulimwengu wa mwili, pale ikulu, Sauli alikuwa mfalme bado, tena mwenye nguvu, ndio maana wakati Mungu anamtuma Samweli kwenda kumpaka Daudi mafuta, alihofia USALAMA wake; Yaani, aliona HATARI ya kutangaza mfalme mwingine (Daudi) wakati mfalme Sauli bado yupo kitini! (1 Samweli 16:1, 2a).
 
1 BWANA akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe.  2Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua” (1 samweli 16:1, 2a).
 
Angalia jambo jingine, Daudi alikuwa na VIPAWA vya KUPIGANA tayari wakati akipakwa mafuta. Lakini alihitaji UJUZI wa kuwa JUU ya watu wa Mungu (Leadership skills). Mungu akampa NAFASI ya kujifunza KAZI za Sauli kwa Sauli wakati Sauli hajui kwamba anamfundisha kazi mrithi wa nafasi yake!
  
Licha ya kupewa AJIRA kule ikulu, ili ajifunze kwa VITENDO, Daudi alipelekwa VITANI pia, tena mstari wa mbele kwa JEMADARI wa vita, mzee Sauli (mfalme), akawa mbeba silaha za Sauli vitani, ili AJIFUNZE jinsi ya kupambana na ADUI za Mungu, japo alikuwa HODARI tayari na KUFAULU mitihani yake ya kupambana na DUBU na SIMBA kule kondeni. Safari hii alitakiwa KUJIFUNZA vita vya aina nyingine (1 Samweli 16: 18, 19 & 21).
  
Kilichompa Daudi nafasi na kazi kule ikulu ilikuwa ni VIPAWA vyake vya kupiga kinubi. Kilichompa kazi ya kuwa mbeba silaha wa mfalme Sauli ni VIPAWA vyake vya kupigana.
  
Angalia tena hapa,
18Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yu pamoja naye. 19Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo [.……..]. 21 Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa mtu wa kumchukulia silaha zake” (1 Samweli 16: 18, 19 & 21).
  
Pamoja na Daudi kupakwa mafuta kama mfalme, bado alihitaji KUNOLEWA VIPAWA vyake ili AWEZE kufanya KUSUDI la Mungu. Ilimchukua miaka zaidi ya 7 kufuzu kuketi kama mfalme wa Israeli. Muda wote alijikuta kwenye MADARASA magumu sana, akifundishwa na walimu mbalimbali, mmojawapo wa walimu wake alikuwa Sauli, ambaye aligeuka kuwa adui yake. Bado Daudi alijifunza kwa unyenyekevu chini ya adui yake, Sauli; akafaulu! Daudi aliweza kuishi kwa miaka kadhaa kama KIJAKAZI wakati anaUPAKO wa kifalme!




KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Mawazo yako ni muhimu sana tafadhali tumia lugha nzuri na tutairusha na wengine waisome.