Jumanne, 3 Julai 2012

MGOMO WA MADAKTARI. RAISI AKOLEZA MOTO. VIONGOZI WA DINI WAZUNGUMZA

Rais JK

SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi serikalini bila ya kulipwa mshahara wa Sh3.5 milioni aache kazi, viongozi wa dini, wanasiasa, wabunge na wasomi wamemtaka apunguze jazba.Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana walisema mgogoro wa madaktari na Serikali bado unajadilika huku Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika akienda mbali zaidi na kusema Serikali iache kisingizio cha Mahakama kulizuia Bunge kujadili mgogoro baina yake na madaktari, wakati yenyewe inajadili na kutoa maelezo.

Juzi, katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alisema Serikali haiwezi kuahidi kuwa inao uwezo wa kuwalipa madaktari mshahara huo na posho zote kwani ikifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa Sh7.7 milioni kwa mwezi kitu ambacho hakiwezekani.
Jana, wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao walisema mgogoro huo kati ya Serikali na madaktari bado unajadilika na kusisitiza kuwa hotuba ya Rais Kikwete haijajibu madai ya madaktari
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema ingekuwa jambo jema kama kungekuwa na uwezekano wa mazungumzo kuendelea.
Alisema kauli ya Rais ni upande wa Serikali hivyo, ingekuwa vyema kama madaktari nao wangepata nafasi ya kujieleza

Wanasiasa
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alimtaka Rais apunguze hasira na kuitaka Serikali ikubali kurudi katika meza ya mazungumzo hata kama ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuwapeleka mahakamani madaktari waliogoma.
Alisema kama Serikali haiwezi kulipa kiwango cha mshahara kilichopendekezwa na madaktari, irudi katika meza ya mazungumzo ili kutafuta suluhu ya mgomo huo unaowaumiza zaidi wananchi.

“Warudi kwenye meza ya majadiliano siyo kila mmoja kusema la kwake na kuacha mgomo kuendelea huku, watu wakiteseka hospitalini bila msaada wowote,’’ alisema Machali.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema Serikali haipaswi kuwafukuza madaktari kwa kuwa imetumia gharama kubwa kuwasomesha.
“Ikiwafukuza madaktari italazimika kuwaleta walio nje ya nchi ambao ni gharama kubwa… Serikali itatue mgogoro huu,” alisema.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema Serikali iache kutumia kisingizio cha Mahakama kulizuia Bunge kujadili mgogoro wa madaktari wakati yenyewe ikitoa ufafanuzi.
“Uamuzi wa Serikali kutoa kauli kupitia hotuba ya Rais una mwelekeo wa kukwepa wabunge kujadili hotuba husika ambayo awali, ilielezwa kuwa ingetolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni. Inawanyima haki wabunge wasitimize wajibu wa kikatiba wa Ibara 63 (2) wa kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema, kwa kuwa Bunge litajadili mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kuanzia leo, ni muhimu wabunge wakajadili pia masuala ambayo Rais ameyaeleza kwa taifa na kutimiza wajibu wa kikatiba.
“Hotuba ya Rais imeendeleza kauli za upande mmoja ambazo zimekuwa zikitolewa na Serikali kuhusu mgogoro huo bila taifa kupewa fursa ya kupata maelezo na vielelezo vya upande wa pili, hivyo Serikali imetoa kauli yake hadharani badala ya bungeni au mahakamani.

Viongozi wa dini
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo alisema madaktari hao wanatakiwa kurudi kazini kwa kuwa tayari Serikali imeshasema kuwa haina fedha za kuwalipa na kuongeza kuwa hata kama wana madai yao, wadai wakiwa kazini.
“Asilimia kubwa ya madaktari wamesomeshwa na Serikali… Serikali hiyohiyo inawaeleza kuwa haina fedha za kuwalipa kama wanavyotaka, binafsi nawaomba tu warudi kazini kwa kuwa mgomo wao unawaathiri zaidi wananchi kuliko hata hao viongozi wa Serikali.

“Tunajua tulikotoka ila hatujui tunakokwenda, kama ni kuboreshwa kwa sekta nzima ya afya, Serikali imesema itatekeleza hilo, haiwezi kuyatekeleza kwa siku moja, haya mambo yanajadilika.
Alisema kama Serikali itakuwa na makosa yake, itayajibu mbele za Mungu... “Madaktari watekeleze wajibu wa kazi yao kwa uwezo wa Serikali iliyopo madarakani.”
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Kagera, Dk Methodius Kilaini alisema kanisa hilo haliwezi kuunga mkono mgomo huo.

Alisema pamoja na kuwa madaktari wana madai yao, jukumu lao kubwa ni kufuata maadili ya kazi yao ambayo hayawaruhusu kugoma.
Katibu Mkuu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania, Askofu David Mwasota alisema madaktari wanatakiwa kutenganisha siasa na maadili ya kazi yao.

“Hata kama Serikali ina makosa yake lakini, wao kuendelea kugoma si jambo zuri kwa jamii na hata mbele za Mungu, watumie njia nyingine kudai madai yao, lakini waendelee kutoa huduma. Madaktari ni watu muhimu, kurudisha viungo vya binadamu katika hali ya kawaida si kazi ndogo, warudi kazini kuokoa mamia ya Watanzania maskini.”
Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Mkoa wa Arusha Abdulkarim Jonjo alisema ipo haja kwa Serikali kukaa meza moja na madaktari hao.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mjini Kati, Thomas Laizer alisema mgogoro wa madaktari umalizwe kwa mazungumzo.
Alisema Serikali inapaswa kuwa wazi inapozungumza na madaktari kwa kueleza ni mambo gani yanawezekana na kwa muda gani ili, kuondoa migogoro.
Akizungumza juzi katika ibada maalumu katika kanisa la KKKT Kimandolu, alisema ili kuondoa hisia kuwa Serikali inahusika na tukio la kutekwa Dk Ulimboka ni lazima iundwe tume huru.
“Nadhani ili kuondoa haya maneno ambayo si jambo dogo, Serikali inapaswa kuunda tume huru kuchunguza tukio hili, kwani inawezekana waliohusika ni watu wengine tu wenye nia mbaya na Serikali lakini ili ukweli ujulikane ni muhimu kuwepo tume huru,” alisema Askofu Laizer.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum aliwataka madaktari kutii agizo lililotolewa na Mahakama kwa kurudi kazini.
“Rais ameshaeleza wazi kwamba Serikali haina fedha za kuwalipa kama wanavyotaka, warudi tu kazini na kuweka masilahi ya Watanzania mbele na kuacha kutanguliza masilahi binafsi,” alisema Sheikh Salum.

Wanaharakati
Mkurungezi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema hotuba hiyo ya Rais haina jipya zaidi ya kurudia maelezo yake ya awali alipokutana na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Nilitarajia kuwa hotuba itakuwa tofauti lakini sivyo. Amerudia maelezo yaleyale aliyoyasema Machi 12 (mwaka huu) alipokutana na wazee katika Ukumbi wa Diamond Jubilee,” alisema Bisimba.
Wakili Peter Jonathan alisema kama kweli Serikali inataka kurudisha imani kwa Watanzania kuhusu tukio la Dk Ulimboka ni lazima ijisafishe kwa kuunda tume huru nje ya Serikali.
“Watafute hata Jaji mstaafu, si lazima atoke Tanzania kuongoza tume huru ikibidi tuchukue hata nje ya nchi ili wakitoa taarifa iweze kuaminiwa na jamii na hiyo ndiyo dhana sahihi ya utawala bora,” alisema.

Mjumbe wa Chama cha Watabibu wa Tiba Asili (ATME), Boniventure Mwalongo ameitaka Serikali kuacha kutumia nguvu kushughulikia madai ya madaktari badala yake ipanue wigo wa majadiliano ili kutatua tatizo hilo.
“Nimesikiliza hotuba ya Rais lakini, haijaonyesha kama kuna jawabu la mgomo hivyo wapanue wigo wa majadiliano ili kumaliza mgogoro huu,” alisema Mwalongo.

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Mawazo yako ni muhimu sana tafadhali tumia lugha nzuri na tutairusha na wengine waisome.