Jumatano, 4 Julai 2012

KANISA LA KKKT LATATUA KERO YA MAJI SAME

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Pare limekamilisha na na kukabidhi kwa wananchi wa Kata ya Mtii Wilayani hapa mradi wa maji uliogharimu sh233 milioni. Akikabidhi mradi huo juzi, Askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Pare, Mchungaji Charles Mjema alisema kanisa limechukua hatua ya kutekeleza mradi huo kufuatia wananchi wa vijiji vya Mtii, Mafingiro na Vumba kukosa huduma ya maji na kuteseka kwa muda mrefu.

Mjema alionya kuwa huduma ya maji katika mradi huo itolewe kwa haki bila upendeleo wa dini, kabila wala itikadi za kisiasa kutokana na ukweli kuwa kanisa halibagui wanajamii kwa vigezo vya aina hiyo.Aliwataka wananchi kutunza mazingira na kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira katika msitu wa asili wa Shengena kilipo chanzo cha maji hayo.
Akipokea mradi huo kwa niaba ya serikali, Mkuu wa Wilaya ya Same, Hermani Kapufi alisema serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na kanisa hilo katika kuboresha huduma za kijamii hivyo kuomba Taasisi na Mashirika mengine ya kijamii kuiga mfano huo na kuwekeza katika huduma za kijamii.

Kapufi aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kutunza miundombinu ya mradi huo kwa maelezo kuwa utakuwa mradi endelevu na itahamasisha wafadhili kuendelea kuwekeza katika miradi mingine.
”Lazima tutunze miundombinu ya mradi huu kama tunataka udumu, na sitaki kusikia eti mabomba yamefukuliwa, au yamekatwa, akitokea mtu kama huyo nipeni taarifa nitaacha namba yangu ya simu nikishaambiwa haraka tutawashughulikia kisheria” Alisema Kapufi.
Katika salamu zake Mwakilishi wa Wafadhili wa Mradi huo, washiriki wa kanisa hilo Usharika wa Gusrow nchini Ujerumani, Sabine Winkler alisema ameridhishwa na ushirikiano wa jamii na serikali ya Tanzania kwa ujumla katika utekelezaji wa mradi huo hivyo kuahidi kuendelea kutekeleza mradi huo awamu ya pili.

Kukamilika kwa mradi huo wenye bomba la urefu wa km 18, vituo vya maji 21 na tanki lenye ujazo wa galoni 20,000, utawafaidisha wananchi zaidi ya 3,200 kupata maji karibu na makazi yao na kuwaondolea adha ya kutembea hadi kilomita 7 kufuata maji

KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO +255 715 033 671, +255 767 033 671 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Mawazo yako ni muhimu sana tafadhali tumia lugha nzuri na tutairusha na wengine waisome.