“UNIKUMBUKE babaa unapowazuru wengine naomba unikumbuke, usinipite Yesu
unapowazuru wengine naomba usinipite.”
Haya ni baadhi ya maneno yaliyomo katika moja ya nyimbo zilizomtambulisha
vema mwimbaji galacha wa nyimbo za Injili nchini, Christina Shusho.
Mwimbaji huyo ambaye anaaza kwa kusema kuwa amefanikiwa kujijengea sifa kwa
mashabiki wa nyimbo za Injili ndani na nje ya mipaka ya nchi kutokana na nyimbo
zake kubeba ujumbe mzito kwa jamii, lakini ukiwa katika msingi wa neno la
Mungu.
Umahiri wake katika kuimba nyimbo hizo za Injili umemuwezesha kutambulika
vema na kujinyakulia tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi, ambapo yeye ni kati
ya wasanii waliopata tuzo za muziki za Afrika Mashariki na Kati (EMAS).
Mwimbaji huyo alishaibuka na tuzo ya msanii bora wa kike wa nyimbo hizo
akiingia na wimbo wake wa Unikumbe. Shusho, mama wa watoto watatu, anasema ni
heshima kubwa kwa Mungu na kwake hasa kwa kuwa alishindanishwa na wanamuziki
wenye vipaji vikubwa vya uimbaji wa nyimbo za Injili.
“Kidogo nilipata hisia za woga iwapo ningeshinda hasa kutokana na ushiriki wa
Alice ambaye ni mwimbaji mzuri wa nyimbo za Injili, lakini pia shindano
lilifanyika nchini kwao hivyo nilihisi kuwa alikuwa na mashabiki wengi zaidi,
lakini Mungu ni mwema nikapata mimi hiyo tuzo, hivyo nina kila sababu ya
kumshukuru Mungu,” anasema.
Shusho anasema ushindi huo umemfanya ajisikie kumheshimu na kumnyenyekea
zaidi Mungu kwa kumpeleka kila hatua, lakini pia anaona fahari kuwa watu wa
ndani na nje ya Tanzania wanatambua kipaji chake na kazi aliyopewa.
“Naona ushindi huu mbali na kumheshimu Mungu zaidi, lakini pia naona nimepewa
jukumu zaidi kwa maana ya kukitumia kipaji changu nilichopewa kwa kuimba zaidi
ya hapa na kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia uimbaji wa Injili,” anasema.
Shusho anasema msingi wa uimbaji wake umeanzia nyumbani kwao baada ya
kuzaliwa katika familia ya Kikristo ambayo ilipenda kuomba na kusali na alikuwa
akihudhuria Shule ya Jumapili ambapo watoto walikuwa wakifundishwa dini, na huko
ndiko alikoanzia kuimba.
Anasema alipokuwa akiendelea kukua alijiona kuwa na wito na akaona ajaribu
kuimba mwenyewe na kugundua ana kipaji na wito wa kuimba nyimbo za Injili, hivyo
alianza kutunga nyimbo zake. Anaeleza kuwa mwaka 2003 aliamua kuingia studio
baada ya kupata msukumo na alitengeneza muziki wake mwenyewe.
“Unajua kuna wengine wanaimba nyimbo za Injili, lakini ukiusikiliza uko
katika hali ya ama kumjibu mtu au kumshambulia mtu baada ya kuapa jambo fulani
mimi ni tofauti naimba kumsifu na kumuabudu Mungu,” anasema.
Hadi sasa Shusho ameshatoa albamu nne ambazo ni Kitu Gani, Unikumbuke, Nipe
Macho, na Kwa Kanisa la Kristo ambapo anasema kuwa albamu ya Unikumbuke
aliyoizindua mwaka 2008 ndiyo iliyomtambulisha vyema kwa mashabiki wa muziki wa
Injili.
Mwanadada huyo mwenye mvuto wa sura na tabasamu la bashasha anaelezea kuwa
muziki wa Injili unakua na kukua huko kunatokana na kuwa zamani kwaya ndizo
zilizokuwa zikijulikana lakini tofauti na sasa nyimbo za Injili zimepenya na
unakuta zikitambulika katika matamasha na mashindano makubwa ya nyimbo za
Injili.
Shusho anasema kuimba kwake
nyimbo za Injili kumemuwezesha kupata faida
mbalimbali ikiwemo jamii kumtambua na kukifahamu kipaji alichonacho, pili kazi
zake kutambulika na kukubalika, tatu anajiona kutumika vizuri na kwamba anaamini
Mungu anaona anavyofanya vyema kazi yake na nne imemuwezesha kufahamika ndani na
nje huku akisema kuwa Mungu amempa maono ya mambo ya mbeleni.
Shusho amepata tuzo ya EMAS, Meya Cup iliyotolewa nchini Kenya, Tuzo za
Muziki wa Injili (Gospel Music Awards) iliyotolewa hapa nchini ambapo aliibuka
mshindi wa Msanii Bora wa Muziki wa Injili na tuzo ya Kenya Groove Music Awards
akiibuka msanii bora wa nje.
Akizungumzia mtindo wa muziki wa Injili hivi sasa anasema kila mtu amepewa
staili yake ya uimbaji lakini waimbaji wanapaswa kukumbuka kila watu wana
utamaduni wao kwa hiyo ni vema wakaimba kwa kuzingatia mazingira ya nchi.
“Kama nilivyosema nyimbo zangu ziko kwa mtindo wa kusifu na kuabudu ndio
maana naimba taratibu na hivyo ni rahisi mtu kusikiliza nyimbo zangu hata akiwa
anasikiliza katika redio wakati anaendesha gari njiani au amerudi nyumbani
anataka kutulia lakini akisikiliza nyimbo za Injili, mimi najiamini na naamini
staili yangu ni njema zaidi,” anasema.
Mbali na kuwa mwimbaji wa nyimbo za Injili, Shusho anasema anapenda kupendeza
na kuonekana maridadi na ndio maana pia anajishughulisha na masuala ya ubunifu
wa mavazi na pia ananunua bidhaa au vitu kutoka nje.
Lakini pia Shusho ni mtangazaji wa runinga ya Sibuka akiendesha kipindi
kinachojulikana kama Gospel Hits huku akieleza kuwa lengo lake ni kuanzisha
kipindi chake cha runinga ambacho atakiita ‘Christina Talk Show’ na kwamba
kitakuwa kikijadili masuala mbalimbali ya kijamii bila kubagua kabila au dini
kwani lengo ni kuisaidia jamii ya Watanzania.
Mwimbaji huyo ameolewa na amebahatika kupata watoto watatu anasema amesoma
hadi kidato cha nne kisha akasomea masuala ya teknolojia ya mawasiliano (IT)
katika Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC), lakini
matarajio yake ni kujiunga na Chuo Kikuu kwa ajili ya kupata elimu zaidi.
Watanzania wana kila sababu ya kumuunga mkono mwanamuziki huyu ambaye amepata
bahati ya kipekee kuchaguliwa kuchuana na waimbaji wengine kutoka barani Afrika.
Shusho ameingia katika kategori mbili ya mwanamuziki bora wa Afrika Mashariki na
mwanamuziki bora wa kike barani Afrika, tuzo hizo zitatolewa Julai 7, mwaka huu,
jijini London nchini Uingereza.
namna ya kupiga kula soma maelakezo hapa chini
bonyeza hapa
http://africagospelawards.com/nominate.html na fuata maelekezo hapa chini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Mawazo yako ni muhimu sana tafadhali tumia lugha nzuri na tutairusha na wengine waisome.