Jumamosi, 9 Julai 2016

  HUDUMU KIVYAKOVYAKO (FREE STYLE) “1 Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. 2Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye. 3Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu” (Yohana 3:1-3).  “3Na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele” (Danieli 12:3). Hebu fikiri, Nikodemo, Farisayo na mkuu wa Wayahudi, yaani Mwalimu wao katika mfumo rasmi (ana ajira kule kwenye dhehebu lake); anakuja GIZANI kujifunza kwa ‘Mwalimu wa mtaani’, asiye na ajira wala idara maalumu, BWANA Yesu, ambaye kwa kweli KAZI zake zinatambulika kwa VIWANGO fulani vya BORA wa kipekee; ila hana CHETI! Sasa jiulize: Kwanza, nani alimwambia Nikodemo kwamba Yesu ni Mwalimu (Rabi)? Jibu ni KAZI zake. Yesu hakuwa na cheti cha kuhitimu mafunzo yao ya Kifarisayo! Pili, Nani alimwambia Nikodemo kwamba Yesu anatoka kwa Mungu? Jibu, MATUNDA ya KAZI zake. Tofautisha KAZI na MATUNDA ya kazi. Kila mtu anaweza kufanya KAZI ila kwa MATUNDA yao tunaweza kuwatofautisha kwamba wametoka wapi. Zingatia MATUNDA zaidi kuliko KAZI maana matunda yatakutangulia hukumuni kabla ya KAZI zako. Ukiona mtu anajivuna na KAZI lakini anapuuza MATUNDA, kuna mambo mawili: kwanza sio MTUMWA (hafanyi kwa ajili ya bwana wake – faida za kiroho sio muhimu kuliko faida za mwilini); na Pili, anatafuta KIBALI kwa hao watu wamwonao kwa sababu ya faida za kipato au cheo au sifa au utukufu. Ukitazama hili, chunguza mambo yako ya gizani (ya siri asiyojua mtu); Hayo ni muhimu kujua aina ya MATUNDA yako, na hayo yatakusimamisha kuliko yale uyatendayo nuruni. Kwa habari hii ya Nikodemo, nataka nikwambie jambo moja la muhimu; fanya kazi yako (HUDUMA) uliyoitiwa (WITO) kwa nguvu na kwa bidii kama vile hakuna anayeona wala kulipa. Najua inawezekana hauko kwenye mfumo rasmi; fanya tu. Utakapozidi sana kufanya, na kumtii Mungu na kumpendeza, japo unafanya “kivyakovyako (free style)”, utagundua wapo WAKUU fulani (akina Nikodemo) wataanza kukunyemelea kwa SIRI gizani (wasikoonekana) wakijifunza kwako taratibu. Na kwa sababu wewe hujui, zidi kufanya kama hakuna mtu anaona hadi siku moja utashangaa kugundua kwamba kumbe walikuwa nyuma yako siku zote! Hivi ndivyo wale wazee (Mafarisayo na wenzao) walimfuatilia BWANA kila hatua na kumsikiliza na kujifunza hadi wakajua kwamba ametoka kwa Mungu! Sasa angalia tena, usishangae, kwa mfano; Siku moja wakipangwawachungaji mbele na kondoo zao wakiwa msururu nyuma yao, na ukaona WATUMISHI wengi sana wako nyuma yako wamejipanga (akina Nikodemo na wenzake). Utaanza kujiuliza na kujitetea, “mimi sio mchungaji na wala sina kanisa”. Ndipo BWANA atajibu kwa mfano na kusema, “hata mimi sikuwa na hicho CHEO cha kichungaji wala sikuwa na HEKALU langu, ila nina kondoo wengi ambao wako kwenye mazizi tofauti”. Na, watu wa namna hii watang’aa kama nyota za Mbinguni milele kwa maana walifanya kazi ya kuwaongoza wengi kutenda mema bila kujali mahali, dini zao na vyeo vyao. Kwa waraka huu nakupa shauri, fanya kazi ya huduma kivyakovyako kama uongozwavyo na ROHO. Kaa chini ya mchungaji wako na ujue umuhimu wake; lakini kumbuka mkiwa shambani mwa BWANA wote ni watenda kazi, kila mmoja akiwa nakiserema chake na wote mtatoa hesabu kwa BWANA mmoja.  Angalizo, usisubiri kupigiwa makofi, kutiwa moyo wala kusifiwa na mtu. Jinsi utakavyozidi kufanya vizuri tarajia vita kuliko shangwe. Na wengi walio hirimu (wakuu waliokutangulia) zako watakutenga kwa sababu ya ubora wako na si kwa udhaifu wako. Kuwa makini. Usikate tamaa. Mungu anakuheshimu kwa sababu unamtumikia, heshima ya wanadamu haitakusaidia sana japo ni LAZIMA uwaeshimu na kuwapenda.    Frank P. Seth  

Chapisha Maoni