Jumamosi, 9 Aprili 2016

UNAFANYA NINI UNAPOFANIKIWA? (Sehemu ya I)



Swali “UNAFANYA nini UNAPOFANIKIWA?” sio la kupuuza hata kidogo. Mara nyingi nimesikia watu wakisema, “ukitaka kujua tabia ya mtu, mpe pesa nyingi au cheo kikubwa” Nimetathmini sana maisha yangu binafsi, na nikatazama maisha ya wetu wengine na kuona jambo hili, “maisha baada ya mafanikio yanaweza kuwa baraka itakayokuinua kwenye baraka zingine, au laana itakayokuangamiza wewe mwenyewe”.

Kama hukujua, mafanikio yanaweza kuwa uangamivu, angalia hapa, “32Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza” (Mithali 1:32).

Ukiangalia wakati wana wa Isarael wanatoka UTUMWANI kwenye nchi Misri kwenda nchi ya ahadi, iliyojaa MAZIWA na ASALI, utaona onyo ambalo Musa aliwapa, akisema,  “11 Jihadhari, usije ukamsahau BWANA, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. 12Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; 13na makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; 14basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; 15aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, 16aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako. 17Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo. 18Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo” (Kumbukumbu la Torati 8:11-18).

 Unafanya nini unapuvuka ngazi fulani ya maisha, na kuingia ya juu zaidi, unapofika mahali ambapo “umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; 13na makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka”, (Kumb. 8:12b-13), Unafanya nini? Angalia tabia yako ya sasa na ya zamani, kisha jiulize, wewe ni yule yule au ni mwingine? Je! Hofu yako kwa Mungu ni ile ile au imebadilika? Jitihada zako katika mambo ya Mungu imeathiriwa vipi na mafanikio yako? Unapojiuliza maswali haya na kujijibu mwenyewe angalia usijipandelee wala kujihesabia haki kupita kiasi. Ni muhimu kijiuliza na kujijibu na kuchukua hatua, wewe mwenyewe.

Sasa angalia tena jambo hili, unajua kwamba mafanikio yako hayakuja kwa nguvu zako mwenyewe tu; unajua ulipomlilia Mungu wakati wa mateso na vita vyako na Akakuvusha, Yeye ndiye aliyekupa “nguvu za kupata utajiri” (Kumb. 8:18). Mbona leo umesahau?

Ukitaka kujua kwamba umemsahau Mungu, kumbuka wakati “ule” Alipokuwa Ngao na Kigao kwako. Kila ulipokuta magumu ulimgeukia kwa KUFUNGA na KUOMBA, sasa umepata pesa na mafanikio, hayo ndio sasa yamekuwa ngao na kigao kwako. Unakinga KIFUA kwa sababu  unajua unakazi nzuri, biashara nzuri, watu wanakujua, unajina kubwa mjini, nk. Wala hukumbuki kumshirikisha tena Mungu mipango yako! Je! Hukumsahau Bwana Mungu wako wewe? Mbona humgeukii tena katika MAHITAJI yako ila unatafuta faraja na msaada kwa miungu mingine?

Frank P. Seth.
KAMA UNA MAONI YOYOTE NIANDIKIE HAPO CHINI AU TUMA UJUMBE KWENYE NO 0784 477775 au Whatup 0784 477775 AU FB Martin Malecela follow me in Twetter martmalecela au tembelea page yetu na ulike martmalecela.blogspot.com

Hakuna maoni: